Antoni wa Padua alikuwa padri na mtawa wa shirika la Ndugu Wadogo maarufu hasa kwa mahubiri yake yaliyomstahilia heshima ya kutangazwa Mwalimu wa Kanisa.
Kwa vipawa vyake vya pekee upande wa akili, elimu, busara, ya kitume na sala hasa alichangia sana maendeleo ya shirika lake.
Ni mmojawapo kati ya watakatifu wanaoheshimiwa zaidi katika Kanisa Katoliki, pia kwa sababu ya miujiza mingi inayosemekana kupatikana kwa kukimbilia maombezi yake.
Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 13 Juni.
Waamini wengi wanapenda picha zinazomuonyesha akiwa na maua meupe pe, yakimaanisha usafi wa moyo wake, na akimshika mtoto Yesu mikononi kadiri ya tukio la ajabu lililosimuliwa na vyanzo mbalimbali.