Select Page

Masomo ya Misa Ijumaa Kuu

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 29/03/2024

2024 MACHI 29 : IJUMAA KUU
Rangi: Nyekundu
Zaburi: Tazama sala ya siku

Somo 1. Isa 52:13-53 : 12

Tazama, mtumishi wangu atatenda kwa busara, atatukuzwa na kuinuliwa juu, naye atakuwa juu sana. Kama vile wengi walivyokustaajabia, (uso wake ulikuwa umeharibiwa sana zaidi ya mtu ye yote, na umbo lake zaidi ya wanadamu), ndivyo atakavyowasitusha mataifa mengi; wafalme watamfumbia vinywa vyao; maana mambo wasiyoambiwa watayaona; na mambo wasiyoyasikia watayafahamu. Ni nani aliyesadiki habari tuliyoileta? Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani? Maana alikuwa mbele zake kama mche mwororo. Na kama mzizi katika nchi kavu; Yeye hana umbo wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani. Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao. Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu. Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa. Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi sote kama kondoo tumepotea; Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na Bwana ameweka juu yake maovu yetu sisi sote. Alionewa, lakini alinyenyekea, wala hakufunua kinywa chake; Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, Na kama vile kondoo anyamazavyo mbele yao wakatoa manyoya yake; naam, hakufunua kinywa chake. Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; Na maisha yake ni nani atakayeisimulia? Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wagu. Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya; Na pamoja na matajiri katika kufa kwake; Ingawa hakutenda jeuri, Wala hapakuwa na hila kinywani mwake. Lakini Bwana aliridhika kumchubua; Alimhuzunisha; Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi, Ataona uzao wake, ataishi siku nyingi; na mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mikononi mwake; Ataona mazao ya taabu ya nafsi yake, na kuridhika. Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki atawafanya wengi kuwa wenye haki; Naye atayachukua maovu yao. Kwa hiyo nitamgawia sehemu pamoja na wakuu, naye atagawanya nyara pamoja nao walio hodari; kwa sababu alimwaga nafsi yake hata kufa. Akahesabiwa pamoja na hao wakosao. Walakini alichukua dhambi za watu wengi, na kuwaombea wakosaji.

Wimbo wa Katikati. Zab 31:2-6, 12-13a, 15-16,17, 25

“1. Nimekukimbilia Wewe, Bwana
Nisiaibike milele.
Kwa haki yako uniponye,
Mikononi mwako naiweka roho yangu;
Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli. (K)

 

 

(K) Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.

2. Kwa sababu ya watesi wangu nimekuwa laumu,
Naam, hasa kwa jirani zangu;
Na kitu cha kutisha kwa rafiki zangu;
Walioniona njiani walinikimbia. (K)

3. Nimesahauliwa kama mfu asiyekumbukwa;
Nimekuwa kama chombo kilichovunjika.
Maana nimesikia masingizio ya wengi;
Hofu ziko pande zote. (K)

4. Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana,
Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu.
Nyakati zangu zimo mikononi mwako;
Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia. (K)

5. Umwangaze mtumishi wako
Kwa nuru ya uso wako;
Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako.
Iweni hodari, mpige moyo konde,
Ninyi nyote mnaomngoja Bwana. (K)”

Somo2. Ebr 4:14-16; 5 : 7-9

Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hatuna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji. Yeye, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu; na, ingawa ni mwana, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata; naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii.

Yn 18:1-19 : 42 (Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo)

” M = Msomaji
W = maneno ya Watu mbali mbali
+ = maneno ya Yesu

M. Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristu yalivyoandikwa na Yohane.

Yesu anakamatwa.
M. Wakati ule Yesu alitoka pamoja na wanafunzi wake kwenda ng’ambo ya kijito Kedroni; palipokuwapo bustani; akaingia yeye na wanafunzi wake. Naye Yuda, yule aliyetaka kumsaliti, alipajua mahali pale; kwa sababu Yesu alikuwa akienda huko mara nyingi pamoja na wanafunzi wake. Basi Yuda, akiisha kupokea kikosi cha askari na watumishi waliotoka kwa wakuu wa makuhani na Mafarisayo, akaenda huko na taa na mienge na silaha. Basi Yesu, hali akijua yote yatakayompata, akatokea, akawambia,
+ Ni nani mnayemtafuta?
M. Wao wakamjibu,
W. Ni Yesu Mnazareti.
M. Yesu akawaambia,
+ Ni mimi.
M. Yuda naye aliyemsaliti alikuwa amesimama pamoja nao. Basi alipowaambia, Ni mimi, walirudi nyuma, wakaanguka chini. Basi akawauliza tena,
+ Mnamtafuta nani?
M. Wakasema,
W. Yesu Mnazareti.
M. Yesu akajibu,
+ Nimekwisha kuwaambieni ya kwamba ni mimi; basi ikiwa mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao.
M. Ili litimizwe lile neno alilolisema, Wale ulionipa sikumpoteza hata mmoja wao. Basi Simoni Petro alikuwa na upanga, akaufuta, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio la kuume. Na yule mtumwa jina lake ni Malko. Basi Yesu akamwambia Petro,
+ Rudisha upanga alani mwake; je! Kikombe alichonipa Baba, mimi nisikinywee?
Yesu mbele ya Anasi na Kayafa, Petro anamkana Yesu.
M. Basi wale askari na yule jemadari na wale watumishi wa Wayahudi walimkamata Yesu, wakamfunga. Wakamchukua kwa Anasi kwanza; maana alikuwa mkwewe Kayafa, yule aliyekuwa Kuhani Mkuu mwaka ule. Naye Kayafa ndiye yule aliyewapa Wayahudi lile shauri ya kwamba yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu. Wakamfuata Yesu, Petro na mwanafunzi mwingine. Na, mwanafunzi huyo alikuwa amejulikana na Kuhani Mkuu, akaingia pamoja na Yesu katika behewa ya Kuhani Mkuu. Lakini Petro akasimama nje mlangoni. Basi yule mwanafunzi mwingine aliyejulikana na Kuhani Mkuu akatoka, akasema na mngoja mlango, akamleta Petro ndani. Basi yule kijakazi, aliyekuwa mngoja mlango, akamwambia Petro,
W. Wewe nawe, je! hu mwanafunzi mmojawapo wa mtu huyu?
M. Naye akasema,
W. Si mimi.
M. Na wale watumwa na watumishi walikuwa wakisimama, wamefanya moto wa makaa; maana ilikuwa baridi; wakawa wakikota moto, Petro naye alikuwapo pamoja nao, anakota moto. Basi Kuhani Mkuu akamwuliza Yesu habari za wanafunzi wake, na habari za mafundisho yake. Yesu akamjibu,
+ Mimi nimesema na ulimwengu waziwazi; siku zote nalifundisha katika
sinagogi na katika hekalu, wakusanyikapo Wayahudi wote; wala kwa siri mimi sikusema neno lolote. Ya nini kuniuliza mimi? Waulize wale waliosikia ni nini niliyowaambia; wao wanajua niliyoyanena.
M. Basi aliposema hayo, mtumishi mmojawapo aliyesimama karibu alimpiga Yesu kofi akisema,
W. Wamjibu hivi Kuhani Mkuu?
M. Yesu akamjibu,
+ Kama nimesema vibaya, ushuhudie ule ubaya; bali kama nimesema vema, wanipigia nini?
M. Basi Anasi akampeleka hali amefungwa kwa Kayafa, Kuhani Mkuu. Na Simoni Petro alikuwa akisimama huko, anakota moto. Basi wakamwambia,
W. Wewe nawe, je! hu mwanafunzi wake mmojawapo?
M. Naye akakana, akasema,
W. Si mimi.
M. Mtumwa mmojawapo wa Kuhani Mkuu, naye ni jamaa yake yule aliyekatwa
sikio na Petro; akasema,
W. Je! mimi simekuona wewe bustanini pamoja naye?
M. Basi Petro akakana tena, na mara akawika jimbi.

Yesu mbele ya Pilato.
M. Kisha wakamchukua Yesu kutoka kwa Kayafa mpaka Praitorio, nayo ikawa alfajiri; lakini wao hawakuingia ndani ya ile Praitorio, wasije wakanajisika, bali wapate kuila Pasaka. Basi Pilato akawatokea nje, akasema,
W. Ni mashitaka gani mnayoleta juu ya mtu huyu?
M. Wakajibu wakamwambia,
W. Kama huyu asingekuwa mtenda mabaya, tusingemleta kwako.
M. Basi Pilato akawaambia,
W. Haya! Mtwaeni ninyi, mkamhukumu kwa ile torati yenu!
M. Wayahudi wakamwambia,
W. Sisi hatuna ruhusa ya kuua mtu.
M. Ili litimie lile neno lake Yesu alilolisema, akionyesha ni mauti gani atakayokufa. Basi Pilato akaingia tena ndani ya Praitorio, akamwita Yesu, akamwambia,
W. Je! Wewe ni Mfalme wa Wayahudi?
M. Yesu akamjibu,
+ Wewe wasema hivi kwa nafsi yako, au watu wengine walikuambia habari zangu?
M. Pilato akajibu,
W. Ama! Ni Myahudi mimi! Taifa lako na wakuu wa makuhani ndio waliokuleta
Kwangu. Umefanya nini?
M. Yesu akajibu,
+ Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa.
M. Basi Pilato akamwambia,
W. Wewe u mfalme basi?
M. Yesu akajibu,
+. Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu.
M. Pilato akamwambia,
W. Kweli ni nini?
M. Naye akiisha kusema neno hilo akawatokea Wayahudi tena, akawaambia,
W. Mimi sioni hatia yoyote kwake. Lakini kwenu kuna desturi ya mimi kuwafungulia mtu mmoja wakati wa Pasaka; basi, mwapenda niwafungulie Mfalme wa Wayahudi?
M. Basi wakapiga kelele tena kusema,
W. Si huyu, bali Baraba.
M. Naye yule Baraba alikuwa mnyang’anyi. Basi ndipo Pilato alipomtwaa Yesu, akampiga mijeledi. Nao askari wakamsokotea taji la miiba, wakamtia kichwani, wakamvika vazi la zambarau. Wakawa wakimwendea, wakisema,
W. Salamu! Mfalme wa Wayahudi!
M. Wakampiga makofi. Kisha Pilato akatokea tena nje, akawaambia,
W. Mtu huyu namleta nje kwenu, mpate kufahamu ya kuwa mimi sioni hatia yoyote kwake.
M. Ndipo Yesu alipotoka nje, naye amevaa ile taji ya miiba, na lile vazi la zambarau. Pilato akawaambia,
W. Tazama, mtu huyu!
M. Basi wale wakuu wa makuhani na watumishi wao walipomwona, walipiga kelele wakisema,
W. Msulibishe! Msulibishe!
M. Pilato akawaambia,
W. Mtwaeni ninyi basi, mkamsulibishe; kwa maana mimi sioni hatia kwake.
M. Wayahudi wakamjibu,
W. Sisi tunayo sheria, na kwa sheria hiyo amestahili kufa, kwa sababu alijifanya kuwa Mwana wa Mungu.
M. Basi Pilato aliposikia neno hilo akazidi kuogopa. Akaingia tena ndani ya ile Praitorio, akamwambia, Yesu,
W. Wewe umetokapi?
M. Lakini Yesu hakumpa jibu lolote. Basi Pilato akamwambia,
W. Husemi nami? Hujui ya kuwa mimi nina mamlaka ya kukufungua, nami nina mamlaka ya kukusulibisha?
M. Yesu akamjibu,
+ . Wewe hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu, kama usingepewa kutoka juu, kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako yuna dhambi iliyo kubwa zaidi.

Yesu anahukumiwa kufa.

M. Na tangu hapo Pilato akatafuta kumfungua; lakini Wayahudi wakapiga makelele
wakisema,
W. Ukimfungua huyu, wewe si rafiki yake Kaisari; kila mtu ajifanyaye kuwa mfalme humfitini Kaisari.
M. Basi Pilato, aliposikia maneno hayo, akamleta Yesu nje, akaketi juu ya kiti cha hukumu, mahali paitwapo Sakafu ya Mawe, au kwa Kiebrania, Gabatha. Nayo ilikuwa Maandalio ya pasaka. Yapata saa sita. Akawaambia Wayahudi,
W. Tazama, Mfalme wenu!
M. Basi wale wakapiga kelele,
W. Mwondoshe! Mwondoshe! Msulibishe!
M. Pilato akawaambia,
W. Je! nimsulibishe mfalme wenu!
M. Wakuu wa makuhani wakamjibu,
W. Sisi hatuna mfalme ila Kaisari.
M. Basi ndipo alipomtia mikononi mwao ili asulibiwe; nao wakampokea Yesu.

Yesu anasulibiwa.

M. Akatoka, hali akijichukulia msalaba wake, mpaka mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, au kwa Kiebrania, Golgotha. Wakamsulibisha huko, na wengine wawili pamoja naye, mmoja huku na mmoja huku, na Yesu katikati. Naye Pilato akaandika anwani, akaiweka juu ya msalaba, imeandikwa, YESU MNAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI. Basi anwani hiyo waliisoma wengi katika Wayahudi; maana mahali pale aliposulibiwa Yesu palikuwa karibu na mji; nayo iliandikwa kwa Kiebrania, na Kirumi, na Kiyunani. Basi wakuu wa makuhani na Wayahudi wakamwambia Pilato,
W. Usiandike, Mfalme wa Wayahudi; bali ya kwamba yule alisema, Mimi ni mfalme wa Wayahudi.
M. Pilato akajibu,
W. Niliyoandika nimeyaandika.

Askari wanagawanya mavazi ya Yesu.

M. Nao askari walipomsulibisha Yesu waliyatwaa mavazi yake, wakafanya mafungu manne, kwa kila askari fungu lake; na kanzu nayo. Basi kanzu ile haikushonwa, ilikuwa imefumwa yote pia tangu juu. Basi wakaambiana,
W. Tusipasue, lakini tuipigie kura, iwe ya nani.
M. Ili litimie andiko lile linenalo, Waligawanya nguo zangu, na vazi langu wakalipigia kura. Basi ndivyo walivyofanya wale askari.

 

Yesu na mamaye.
M. Na penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa Klopa, na Mariamu Magdalene. Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake,
+ Mama, tazama, mwanao.
M. Kisha akamwambia yule mwanafunzi,
+ Tazama, mama yako.
M. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake.

Yesu anakufa

M. Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko litimizwe, akasema,
+. Naona kiu.
M. Kulikuwako huko chombo kimejaa siki; basi wakatia sifongo iliyojaa siki juu ya ufito wa hisopo, wakampelekea kinywani. Basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema,
+. Imekwisha.
M. Akainama kichwa, akaisalimu roho yake.

Yesu anatobolewa ubavu.
M. Basi Wayahudi, kwa sababu ni Maandalio, miili isikae juu ya misalaba siku ya sabato, (maana sabato ile ilikuwa siku kubwa), walimwomba Pilato miguu yao ivunjwe, wakaondolewe. Basi askari wakaenda, wakamvunja miguu wa kwanza, na wa pili, aliyesulibiwa pamoja naye. Lakini walipomjia Yesu na kuona ya kuwa amekwisha kufa, hawakumvunja miguu; lakini askari mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; na mara ikatoka damu na maji. Naye aliyeona ameshuhudia, na ushuhuda wake ni kweli; naye anajua ya kuwa anasema kweli ili ninyi nanyi mpate kusadiki. Kwa maana hayo yalitukia ili andiko litimie: Hapana mfupa wake utakaovunjwa. Na tena andiko lingine lanena: Watamtazama yeye waliyemchoma.

 

Yesu anazikwa
M. Hata baada ya hayo Yusufu na Arimathaya, naye ni mwanafunzi wa Yesu (lakini kwa siri, kwa hofu ya Wayahudi), alimwomba Pilato ruhusa ili auondoe `mwili wake Yesu. Na Pilato akampa ruhusa. Basi akaenda, akauondoa mwili wake Yesu. Na Pilato akampa ruhusa. Basi akaenda, akaondoa mwili wake. Akaenda Nikodemo naye, (yule aliyemwendea usiku hapo kwanza), akaleta mchanganyiko wa manemane na uudi, yapata ratili mia. Basi wakautwaa mwili wake Yesu, wakaufunga sanda ya kitani pamoja na yale manukato, kama ilivyo desturi ya Wayahudi katika kuzika. Na pale pale aliposulibiwa palikuwa na bustani; na ndani ya bustani mna kaburi jipya, ambalo hajatiwa bado mtu yeyote ndani yake. Humo basi, kwa sababu ya Maandalio ya Wayahudi, wakamweka Yesu; maana lile kaburi lilikuwa karibu.”

TAFAKARI

“KIFO NI UFUNGUO WA MAISHA MAPYA
Leo Mama Kanisa anatuingiza katika simanzi nzito kwa mateso na kifo cha Yesu Kristo. Kibinadamu mtu akikata pumzi tunajua hapo ndo mwisho wake. Lakini kwa Mkristo tunaamini ni mwanzo wa maisha mengine ya umilele aidha ya furaha mbinguni (kama aliishi vyema na kufa bila dhambi) au mateso kidogo toharani (kama kuna madoa ya kutakaswa kidogo) au ya mateso milele motoni (kama alikufa na dhambi ya mauti-kumkataa Mungu hadi dakika ya mwisho). Tunavaa utu mpya baada ya kifo, (rej. 1Kor 15:42-44) “…unazikwa mwili wa kawaida na unafufuliwa mwili wa kiroho.” Somo la kwanza limemzungumzia Kristo kama mtumishi mwenye busara na somo la pili likatueleza kuwa aliingia katika mbingu kama kielelezo kwetu. Injili imetuonesha wazi kuwa Yesu alidhamiria kutukomboa kupitia mateso “kikombe alichonipa baba nisikinywe?” Kristo amekufa ili nasi tupate uzima wa mpya.”

SALA: Ee Bwana utujalie tufe kifo chema.

Masomo ya Misa Alhamisi Kuu

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 28/03/2024 Alhamisi Kuu

2024 MACHI 28 ALHAMISI: JUMA KUU
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku

Somo 1. Kut 12:1-8, 11-14

Bwana akanena na Musa na Haruni katika nchi ya Misri, akawaambia, mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu; utakuwa ni mwezi wa kwanza wa mwaka kwenu. Semeni na mkutano wote wa Israeli, mkawaambie, Siku ya kumi ya mwezi huu kila mtu atatwaa mwana-kondoo, kwa hesabu ya nyumba ya baba zao, mwana-kondoo kwa watu wa nyumba moja; na ikiwa watu wa nyumba ni wachache kwa mwana-kondoo, basi yeye na jirani yake aliye karibu na nyumba yake na watwae mwana-kondoo mmoja, kwa kadiri ya hesabu ya watu, kwa kadiri ya ulaji wa kila mtu, ndivyo mtakavyofanya hesabu yenu kwa yule mwana-kondoo. Mwana-kondoo wenu atakuwa hana hila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi. Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni. Nao watatwaa baadhi ya damu yake na kutia katika miimo miwili na katika kizingiti cha juu, katika zile nyumba watakazomla. Watakula nyama yake usiku ule ule, imeokwa motoni, pamoja na mkate usiotiwa chachu; tena pamoja na mboga zenye uchungu. Tena mtamla hivi: mtakuwa mmefungwa viuno vyenu, mmevaa viatu vyenu miguuni, na fimbo zenu mikononi mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; ni pasaka ya Bwana. Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; mimi ndimi Bwana. Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lo lote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri. Na siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu ya Bwana; mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele.

Wimbo wa Katikati. Zab 116:12-13, 15-18

“1. Nimrudishie Bwana nini
Kwa ukarimu wake wote alionitendea?
Nitakipokea kikombe cha wokovu;
Na kulitangaza jina la Bwana. (K)

“(K) Kikombe kile cha baraka tukibarikicho,
Je,! Si ushirika wa damu ya Kristo?”

2. Ina thamani machoni pa Bwana
Mauti ya wacha Mungu wake.
Ee Bwana, hakika mimi ni mtumishi wako,
Mtumishi wako, mwana na mjakazi wako.
Umevifungua vifungo vyangu. (K)

3. Nitakutolea dhabihu ya kushukuru;
Na kulitangaza jina la Bwana,
Niotaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana,
Naam, mbele ya watu wake wote. (K)”

Somo 2. 1 Kor 11:23-26

Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa ninyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Na vivi hivi baada ya kula akikitwaa kikombe, akisema, kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu. Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo.

Injili. Yn 13:1-15

Basi, kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, hali akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye aliwapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo. Hata wakati wa chakula cha jioni, naye Ibilisi amekwisha kumtia Yuda, mwana wa Simoni Iskariote, moyo wa kumsaliti; Yesu, hali akijua ya kuwa Baba amempa vyote mikononi mwake, na ya kuwa alitoka kwa Mungu naye anakwenda kwa Mungu, aliondoka chakulani; akaweka kando mavazi yake, akatwaa kitambaa, akajifunga kiunoni. Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwatawadha wanafunzi miguu, na kuifuta kwa kile kitambaa alichojifunga. Hivyo yuaja kwa Simoni Petro. Huyo akamwambia, Bwana! Wewe wanitawadha miguu mimi? Yesu akajibu, akamwambia, Nifanyalo wewe hujui sasa; lakini utalifahamu baadaye. Petro akamwambia, Wewe hutanitawadha miguu kamwe. Yesu akamwambia, Kama nisipokutawadha, huna shirika nami. Simoni Petro akamwambia, Bwana, si miguu yangu tu, hata na mikono yangu na kichwa changu pia.

Yesu akamwambia, Yeye aliyekwisha kuoga hana haja ila ya kutawadha miguu, bali yu safi mwili wote; nanyi mmekuwa safi, lakini si nyote. Kwa maana alimjua yeye atakayemsaliti; ndiyo maana alisema, Si nyote mlio safi. Basi alipokwisha kuwatawadha miguu, na kuyatwaa mavazi yake, na kuketi tena, akawaambia, Je! Mmeelewa na hayo niliyowatendea? Ninyi mwaniita Mwalimu, na, Bwana; nanyi mwanena vema, maana ndivyo nilivyo. Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi. Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo.

TAFAKARI

YESU CHAKULA CHA UZIMA: Wakati wa Ibada ya Misa Takatifu maneno yanayotumika wakati wa mageuzo ndiyo yaliyojitokeza kwenye somo la pili. “Huu ndio mwili wangu, hii ndiyo damu yangu, fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.” Kristo alituachia Sakramenti ya Mwili wake ili tuendeleze sadaka ya ukombozi. Leo ni Alhamisi Kuu, tunakumbuka siku ambayo Kristo alisimika mambo makuu 3. Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu na Amri kuu ya Mapendo. Tendo la Kristo kuwatawadha mitume wake miguu ni unyenyekevu wa hali ya juu. Ulimwengu wa leo umekosa hili, wengi wanaoneshana ubabe, kutumia nguvu hadi vita visivyokoma na malumbano kila mara. Japo Kristo aliwaosha wote lakini alisema “si nyote mlio safi” hapa anatutaka tujitafakari dhambi zetu na kuziungama. Kila mmoja ajiulize, ‘mimi ni safi?’ Tunaalikwa tutawadhane miguu, tuoneshane kujaliana. Je tunampokeaje Yesu wa Ekaristi? Ni inavyostahili au sivyo? Tuangalie tusije kumpokea Yesu wa Ekaristi ikawa ndio hukumu yetu. Tuwaombee viongozi wetu wa Kanisa ili wadumu daima katika kuendeleza fumbo hili.

SALA: Ee Yesu uliye chakula cha uzima, utupe daima uzima wako.

Masomo ya Misa Machi 27

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 27/03/2024

2024 MACHI 27 JUMATANO: JUMA KUU
Mt. Ruperto, Askofu
Rangi: Urujuani
Zaburi: Juma 2

Somo 1. Isa 50:4-9

Bwana Mungu amenipa ulinzi wa hao wafundishwao, nipate kujua jinsi ya kumtegemea kwa maneno yeye aliyechoka, huniamsha asubuhi baada ya asubuhi; huniamsha, sikio langu lipate kusikia kama watu wafundishwao. Bwana Mungu amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi wala sikurudi nyuma. Naliwatolea wapigao mgongo wangu, na wang’oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate. Maana Bwana Mungu atanisaidia; kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume, nami najua ya kuwa sitaona haya. Yeye anipatiaye haki yangu yu karibu; ni nani atakayeshindana nami? Na tusimame pamoja; ni nani aliye hasimu yangu? Na anikaribie basi. Tazama, Bwana Mungu atanisaidia; ni nani atakayenihukumu kuwa mkosa?

Wimbo wa Katikati. Zab 69:8-10, 21-22, 31, 33-34

1. Kwa ajili yako nimestahimili laumu
Fedheha imenifunika uso wangu.
Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu,
Na msikwao kwa wana wa mama yangu.
Maana wivu wa nyumba yako umenila,
Na laumu zao wanaokulaumu zimenipata. (K)

(K) Kwa wingi wa fadhili zako unijibu, ee Bwana.

2. Laumu imenivunja moyo,
Nami ninaugua sana.
Nikangoja aje wa kunihurumia, wala hakuna;
Na wa kunifariji, wala sikumwona mtu..
Wakanipa uchungu kuwa chakula changu;
Nami nilipokuwa na kiu wakaninywesha siki. (K)

3. Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo,
Nami nitamtukuza kwa shukrani.
Walioonewa watakapoona watafurahi;
Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe.
Kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji,
Wala hawadharau wafunga wale. (K)”

“Mwana wa Adamu aenda zake, kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa. ”  

Mt. 26:24

Injili. Mt 26:14-25

Wakati huo mmoja wa wale Thenashara, jina lake Yuda Iskariote, aliwaendea wakuu wa makuhani, akasema, Ni nini mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu? Wakampimia vipande thelathini vya fedha. Tokea wakati huo akawa akitafuta nafasi apate kumsaliti. Hata siku ya kwanza ya mikate isiyotiwa chachu, wanafunzi wake wakamwendea Yesu, wakamwambia, Ni wapi utakapo tukuandalie uile Pasaka? Akasema, Enendeni mjini kwa mtu fulani, mkamwambie, Mwalimu asema, Majira yangu ni karibu; kwako nitafanya Pasaka pamoja na wanafunzi wangu. Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, wakaiandaa Pasaka. Basi kulipokuwa jioni aliketi chakulani pamoja na wale Thenashara. Nao walipokuwa wakila, alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu atanisaliti. Wakahuzunika sana, wakaanza kumwuliza mmoja mmoja, Ni mimi, Bwana? Akajibu akasema, Yeye aliyetia mkono wake pamoja nami katika kombe, ndiye atakayenisaliti. Mwana wa Adamu aenda zake, kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa. Yuda, yule mwenye kumsaliti, akajibu, akasema, Ni mimi, Rabi? Akamwambia, Wewe umesema.

TAFAKARI

RUSHWA HUFIFISHA UTU: Tupo katika Juma Kuu ambapo tunaelekea kwenye mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kristo katika utume wake yapo mengi aliyowaeleza wale mitume wake kwa lengo la kuwaachia utume huo kuendelezwa. Kwa Kristo kukamatwa, kuteswa, kifo na ufufuko kulichangiwa na mtu wake wa karibu, vijana wa leo watasema, ‘Yuda alimzunguka Yesu’ kuna usemi usemao, “kikulacho ki nguni mwako.” Kuna mwanamuziki aitwae Mr Nice aliimba wimbo hivi, “Kikulacho kumbe ki nguoni mwako, rafiki ndiye adui yako, ninakula nae ninacheka nae kumbe mwenzangu anaona gere.” Yuda alikuwa rafiki wa karibu sana na Yesu, alikubali kupokea rushwa ili amsaliti Yesu kwa Makuhani. Hapa tunajifunza kusipende kudanganyika kwa vitu au mali ya aina yoyote kwa gharama ya maisha yetu au ya wenzetu. Tamaa ya mali imeangamiza wengi.

SALA: Ee Bwana utuepushe na taama ya mali.

Masomo ya Misa Machi 26

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 26/03/2024

2024 MACHI 26 JUMANNE: JUMA KUU
Mt. Ludger Askofu 
Rangi: Urujuani
Zaburi: Juma 2

somo 1. Isa 49:1-6

Nisikilizeni enyi visiwa; tegeni masikio yenu, enyi kabila za watu mlio mbali sana; Bwana ameniita tangu tumboni; toka tumbo la mama yangu amenitaja jina langu. Naye anifanya kinywa changu kuwa kama upanga mkali; katika kivuli cha mkono wake amenisitiri; naye amenifanya kuwa mshale uliosuguliwa; katika podo lake amenificha; Akaniambia; wewe u mtumishi wangu, Israeli, ambaye katika wewe nitatukuzwa. Lakini nikasema, Nimejitaabisha bure, nimetumia nguvu zangu bure bila faida; lakini hakika hukumu yangu ina Bwana, na thawabu yangu ina Mungu wangu. Na sasa Bwana asema hivi, yeye aliyeniumba tangu tumboni niwe mtumishi wake, ili nimletee Yakobo tena, na Israeli wakusanyike mbele zake tena. Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu ili kuziinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia.

wimbo wa katikati. Zab 71:1-6, 15, 17

1. Nimekukimbilia Wewe, Bwana,
Nisiaibike milele.
Kwa haki yako uniponye, uniopoe,
Unitegee sikio lako, uniokoe. (K)

(K) Kinywa changu kitasimulia wokovu wako.

2. Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu,
Nitakakokwenda siku zote.
Umeamuru niokolewe,
Ndiwe genge langu na ngome yangu.
Ee Mungu wangu, uniopoe mkononi mwa mkorofi,
Katika mkono wake mwovu, mdhalimu. (K)

3. Maana ndiwe taraja langu, Ee Bwana Mungu,
Tumaini langu tokea ujana wangu.
Nimekutegemea wewe tangu kuzaliwa,
Ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu,
Ninakusifu Wewe daima. (K)

4. Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako.
Mchana kutwa; maana sijui hesabu yake.
Ee Mungu, umenifurahisha tokea ujana wangu;
Nimekuwa nikitangaza miujiza yako hata leo. (K)

Injili. Yn 13:21-33, 36-38

Pale alipokuwa na mitume wake mezani Yesu alifadhaika rohoni, akashuhudia akisema, Amin, amin, nawaambieni, Mmoja wenu atanisaliti. Wanafunzi wakatazamana, huku wakiona shaka ni nani amtajaye. Na palikuwapo mmoja wa wanafunzi wake, ameegama kifuani pa Yesu, ambaye Yesu alimpenda. Basi Simoni Petro akampungia mkono, akamwambia, Uliza, ni nani amtajaye? Basi yeye, hali akimwelekea Yesu kifua chake, akamwambia, Bwana, ni nani? Basi Yesu akajibu, Ndiye mtu yule nitakayemtowelea tonge na kumpa. Akatowelea tonge, akalitwaa akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskariote. Na baada ya hilo tonge Shetani alimwingia. Basi Yesu akamwambia, Uyatendayo yatende upesi. Wala hakuna mtu katika wale walioketi chakulani aliyeijua sababu ya kumwambia hivyo. Kwa maana wengine walidhania, kwa kuwa Yuda huchukua mfuko, ya kwamba Yesu alimwambia kama, Nunua tunavyohitaji kwa sikukuu; au kwamba awape maskini kitu. Basi huyo, akiisha kulipokea lile tonge, akatoka mara hiyo. Nako kulikuwa ni usiku. Basi huyo alipokwisha kutoka, Yesu alisema, Sasa ametukuzwa Mwana wa Adamu, naye Mungu ametukuzwa ndani yake. Mungu naye atamtukuza ndani ya nafsi yake; naye atamtukuza mara. Enyi watoto wadogo, bado kitambo kidogo nipo pamoja nanyi; mtanitafuta; na kama vile nilivyowaambia Wayahudi ya kwamba, Mimi niendako ninyi hamwezi kuja; kadhalika sasa nawaambia ninyi. Simoni Petro akamwambia, Bwana, unakwendapi? Yesu akamjibu, Niendako huwezi kunifuata sasa; lakini utanifuata baadaye. Petro akamwambia, Bwana, kwa nini mimi nisiweze kukufuata sasa? Mimi nitautoa uhai wangu kwa ajili yako. Yesu akamjibu, Je! Wewe utautoa uhai wako kwa ajili yangu? Amin, amin, nakuambia, Jimbi hatawika hata wewe utakapokuwa umenikana mara tatu.

TAFAKARI

MUNGU ANAHESHIMU UHURU WETU: Maisha ya jumuiya humaanisha ni maisha yaliyoshirikishwa kutokana na kifungo cha upendo. Katika jumuiya mnakutana watu toka makabila mbalimbali na kila mtu ana hulka zake hivyo kwamba kupitia upendo basi wote mnafungamanishwa. Yesu naye alianzisha jumuiya ya kwanza ya mitume wake ambao aliwapata toka sehemu mbalimbali na kila mmoja alikuwa na tabia tofauti na mwenzake na aliishi nao kwa namna ambayo hakuwaingilia katika uhuru wao, alipenda kila mmoja aishi wito wake kwa uhuru kamili. Kitendo cha Yesu kumpa Yuda Iskariote tonge ni alama ya kumwacha huru, asikilize nafsi yake na aamue mwenyewe. Yuda Iskariote aliziba masikio ya usikivu kwa Mungu. Hata sisi katika maisha yetu Mungu anatuacha huru. Mfano mwizi akitaka kuiba, si ajabu mbwa akambwekea, lakini yule mwizi atamfukuza huyu mbwa na kuendelea kuiba. Nasi kuna nyakati tunaziba masikio yetu kwa sauti ya Mungu inayotutaka tuache mienendo yetu mibaya lakini hatushtuki. Tunapewa matonge na tunaendelea kula bila aibu kama Yuda.

SALA: Ee Bwana uyazibue masikio yetu yapate kusikiliza matakwa yako.


Masomo ya Misa Machi 25

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 25/03/2024

2024 MACHI 25 JUMATATU: JUMA KUU
KUPASHWA HABARI YA KUZALIWA BWANA
Rangi: Urujuani
Zaburi: Juma 2

Somo 1. Isa 42:1-7

Tazama mtumishi wangu nimtegemezaye; mteule wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa naye; nimetia roho yangu juu yake; naye atawatolea mataifa hukumu. Hatalia, wala hatapaza sauti yake, wala kuifanya isikiwe katika njia kuu. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima; atatokeza hukumu kwa kweli. Hatazimia, wala hatakata tamaa, hata atakapoweka hukumu duniani; na visiwa vitaingojea sheria yake. Mungu Bwana anena, yeye aliyeziumba mbingu, na kuzitanda; yeye aliyeitandaza nchi na mazao yake; yeye awapaye pumzi watu walio juu yake; yeye awapaye roho wao waendao ndani yake. Mimi, Bwana, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa; kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa.

Wimbo wa Katikati. Zab 27:1-3, 13-14

“1. Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
Nimwogope nani?
Bwana ni ngome ya uzima wangu,
Nimhofu nani? (K)

(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.

2. Watenda mabaya waliponikaribia,
Wanile nyama yangu,
Watesi wangu na adui zangu,
Walijikwaa wakaanguka. (K)

3. Jeshi lijapojipanga kupigana nami,
Moyo wangu hautaogopa.
Vita vijaponitokea,
Hata japo nitatumaini. (K)

4. Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana
Katika nchi ya walio hai.
Umngoje Bwana, uwe hodari,
Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana. (K)”

Injili. Yn 12:1-11

Siku sita kabla ya Pasaka, Yesu alifika Bethania, alipokuwapo Lazaro, yeye ambaye Yesu alimfufua katika wafu. Basi wakamwandalia karamu huko; naye Martha akatumika; na Lazaro alikuwa mmojawapo wa wale walioketi chakulani pamoja naye. Basi Mariamu akatwaa rali ya marhamu ya nardo safi yenye thamani nyingi, akampaka Yesu miguu, akamfuta miguu kwa nywele zake. Nayo nyumba pia ikajaa harufu ya marhamu. Basi Yuda Iskariote, mmojawapo wa wanafunzi wake, ambaye ndiye atakaye kumsaliti, akasema, Mbona marhamu hii haikuuzwa kwa dinari mia tatu, wakapewa maskini? Naye aliyasema hayo, si kwa kuwahurumia maskini; bali kwa kuwa ni mwivi, naye ndiye aliyeshika mfuko, akavichukua vilivyotiwa humo. Basi Yesu alisema, Mwache aiweke kwa siku ya maziko yangu. Kwa maana maskini mnao sikuzote pamoja nanyi; bali mimi hamnami sikuzote. Basi watu wengi katika Wayahudi walipata kujua ya kuwa yeye yuko huko; nao wakaja, si kwa ajili yake Yesu tu, ila wamwone na Lazaro, ambaye Yesu alimfufua katika wafu. Nao wakuu wa makuhani wakafanya shauri la kumwua Lazaro naye; maana kwa ajili yake wengi katika Wayahudi walijitenga, wakamwamini Yesu.

TAFAKARI

UNAFIKI HUONDOA LADHA YA MAISHA: Mtaalamu mmoja aitwaye Lawrence Durrell aliandika hivi, “Sio kwamba upendo ndio hauoni, bali wivu ndio hauoni” kwa maana hii alipenda kumaanisha kuwa wivu hukuziba usione mazuri ya wengine. Yuda Iskariote (mfuasi wa Kristo) alijawa na jicho la wivu na alipoona alichotenda Mariam kwa Yesu hakufurahi na kwa kinafiki anajifanya kuwaonea huruma na kuwapenda maskini jambo ambao haikuwa hivyo. Yesu anamshushua na kumpa ukweli hadharani kuwa alichokuwa anasema si kweli kwamba aliwapenda na kuwaonea huruma maskini na ya kuwa alichokuwa anasema sicho alichomaanisha. Yesu alisema “mwache aiweke kwa siku ya maziko yangu.” Tuelewe, kamwe haitokaa itokee Simba amsindikize mbuzi malishoni, ukiona hivi ujue ni kwa muda tu, ni kwa kujifanya tu, baada ya hatua kadhaa mbuzi huyu ataliwa tu. Na watu wanafiki ndivyo walivyo, tunao katika jamii zetu, wanajifanya kuishi na sisi kwa uelewano kumbe yaliyo ndani ya fikra zao hatuyajui, tutaliwa tu. Mtenda wema kukaa meza moja na mnafiki ni ngumu.

SALA: Ewe Roho Mtakatifu, tunaomba utuepushe na roho ya unafiki.