NOVEMBA 21, 2023; JUMANNE: JUMA LA 33 LA MWAKA

Kutolewa Bikira Maria Mt. Hekaluni
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: 2 Mak 6:18-31
Eliyazari, mmoja wa waandishi wakuu, mtu wa umri mkubwa na sura njema, alishurutishwa kufunua kinywa chake kulishwa nyama ya nguruwe. Lakini akaitema ile nyama, akasogea mwenyewe kwenye mahali pa kuteswa, akiona afadhali kufa kwa heshima kuliko kuishi kwa unajisi. Akatenda kama yampasavyo mtu aliyekaza nia yake kuvikataa vitu visivyo halali kuonjwa hata kwa kutaka kujiokoa maisha.
Basi, wale waliosimamia dhabihu hiyo haramu, kwa kuwa wamejuana naye kwa miaka mingi, walimchukua kando wakamsihi alete nyama yake mwenyewe, iliyo halali ya kuliwa, na kufanya kana kwamba anaila nyama ya dhabihu, kama mfalme alivyoamuru. Hivyo atajiponya na mauti, na kutendewa nao kwa hisani kwa sababu ya urafiki wao wa tangu zamani. Lakini yeye aliikaza nia yake madhubuti, nia iliyostahili umri wake na jadi yake, na mvi zake stahivu, na mwendo wake wa adili tangu utoto wake katika kuzishika amri takatifu zilizotolewa na Mungu.
Akakataa kabisa, na kuwaambia wampeleke kuzimuni upesi, akisema: haipatani na miaka yetu kudanganya, isije vijana wengi wadhani ya kuwa Eliyazari, katika mwaka wake wa tisini, ameiacha dini yake kwa dini ya kigeni; na hivyo, kwa sababu ya udanganyifu wangu, watapotoshwa na mimi mwenyewe nitajipatia unajisi na aibu katika uzee wangu. Na hata nikiepukana na adhabu ya wanadamu sasa, lakini sitaweza kuepukana na mikono ya Mwenyezi, nikiwa hai au nimekufa. Basi, nikitoa maisha yangu sasa kwa ushujaa, nitajionesha kuwa nimeistahili miaka yangu mingi, na kuwaachia vijana mfano wa kufa mauti ya fahari kwa hiyari na kwa uthabiti, kwa ajili ya amri takatifu zenye heshima.
Alipokwisha kusema hayo, alipaendea mara mahali pa kuteswa. Nao waliokuwa wakimwonesha urafiki walibadili nia zao kwa mabaya kwa sababu ya maneno yake waliyoyaona kuwa ya kiwazimu. Naye alipokuwa kufani kwa ajili ya mapigo yake, aliugua akasema, kwake Bwana ajuaye yote ni dhahiri ya kuwa, ingawa ningaliweza kuepukana na mauti, lakini ninavumilia maumivu makali mwilini mwangu; hata rohoni mwangu ninayavumilia kwa furaha kwa sababu ya kicho changu kwake.
Hivyo alikufa; na kwa kufa kwake aliacha mfano wa unyofu na ukumbusho wa wema, si kwa vijana tu, ila kwa jamii yote ya taifa lake.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 3:1-6

 1. Bwana, watesi wangu wamezidi kuwa wengi,
  Ni wengi wanaonishambulia,
  Ni wengi wanaoiambia nafsi yangu,
  Hana wokovu huyu kwa Mungu.
  (K) Bwana ananitegemeza.
 2. Na Wewe, Bwana, U ngao yangu pande zote,
  Utukufu wangu na mwinua kichwa changu.
  Kwa sauti yangu namwita Bwana,
  Naye aniitikia toka mlima wake mtakatifu. (K)
 3. Nalijilaza nikalala usingizi, nikaamka,
  Kwa kuwa Bwana ananitegemeza.
  Sitaogopa makumi elfu ya watu,
  Waliojipanga juu yangu pande zote. (K)

INJILI: Lk 19:1-10
Yesu alipoingia Yeriko alipita katikati yake. Na tazama, palikuwa na mtu, jina lake Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye ni tajiri. Huyu alikuwa akitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani, asiweze kwa sababu ya umati wa watu, maana ni mfupi wa kimo. Akatangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu apate kumwona, kwa kuwa atakuja kuipitia njia ile.
Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako. Akafanya haraka, akashuka, akamkaribisha kwa furaha. Hata watu walipoona, walinung’unika wote, wakisema, Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi. Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang’anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne. Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu. Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.

TAFAKARI:
SHAUKU YA KUMWONA YESU HUJENGWA KATIKA IMANI: Leo tunakutana na watu wenye imani na walio na hamu ya kumwona Yesu. Eliyazari alisimama imara katika imani, na akakataa kupotoshwa kwa kufanya yaliyo haramu. Alisema, “Sitaweza kuepukana na mikono ya Mwenyezi Mungu nikiwa hai au nikiwa nimekufa.” Huu ni ujasiri mkuu wa kukubali kuwa Mungu ndiye mweza yote na haepukiki. Haifai kumridhisha mwanadamu huku unamuudhi Mungu. Zakayo naye katika Injili akitamani kumwona Yesu, aliisahau hadhi yake, heshima na utajiri, akaukwea mti. Hebu waza, wakati wa andamano la Ekaristi, ukimwona Waziri ameupanda mti ili amwone Yesu kwenye Ekarosti Takatifu. Inakuwaje sisi huona haya kumtangaza na kumkiri Yesu? Mbona wewe wataka kumweka Yesu pembeni, huna haja hata ya kwenda kanisani? Tujifunze kutoka kwa Zakayo. Tusione haya kumtangaza Kristo, tukiwaza watakayoyasema watu. Hili ni elezo tosha kuwa sharti tuzisake baraka kwa vyovyote vile.

SALA: Yesu mwema tujalie moyo wa unyenyekevu hasa tunapojaliwa uwezo au cheo katika maisha. Amina.