Mt. Adrea Avelino, Mtawa
Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: 1 Mak 1:10-15, 41-43, 54-57, 62-64
Kulichipuka chipukizi chenye dhambi, ndiye Antioko Epifani, mwana wa mfalme Antioko, ambaye alikuwa amewekwa amana kwa Warumi. Naye alitawalishwa katika mwaka wa mia thelathini na saba wa enzi ya Wayunani.
Siku zile walitokea wahalifu sheria katika Israeli, wakashawishi wengi, wakisema, twende tufanye maagano na mataifa wanaotuzunguka, maana tangu tulipofarakana nao misiba mingi imetupata. Jambo hilo likapendeza machoni pao, hata watu fulani wakafanya hima kwenda kwa mfalme, naye akawapa ruhusa kuzifuata kawaida za mataifa. Wakafanya kiwanja cha michezo Yerusalemu kama kawaida ya mataifa, wakajifanya kana kwamba hawakutahiriwa wakajitenga na agano takatifu. Hivyo walijiunga na mataifa na kujiuza wafanye uovu.
Mfalme Antioko akaziandikia milki zake zote, kwamba wote wawe taifa moja, kila mtu aache sheria zake za asili. Watu wote wa mataifa wakaikubali amri ya mfalme, hata wengi katika Israeli walifuata ibada yake, wakitoa dhabihu kwa miungu ya uongo na kutia unajisi Sabato.
Siku ya ishirini na tano ya Kislevu, mwaka wa mia arobaini na tano, waliweka chukizo la uharibifu juu ya madhabahu, na katika miji ya Uyahudi kila upande walijenga vimadhabahu vya miungu, wakavukiza uvumba milangoni pa nyumba na njiani. Na vitabu vya sheria walivyovipata walivirarua vipande vipande wakaviteketeza. Mtu ye yote aliyepatikana na kitabu au aliyeonekana anaifuata sheria, alihukumiwa kufa kama alivyoamuru mfalme.
Hata hivyo wengi katika Israeli walikaza nia zao kwa uthabiti wasile vitu vilivyo najisi. Waliona afadhali kufa kuliko kutiwa unajisi kwa vyakula au kulivunja agano takatifu. Wakafa. Kukawa hasira kuu juu ya Israeli.
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 119:53, 61, 134, 150, 155, 158
- Gadhabu imenishika kwa sababu ya wasio haki,
Waiachao sheria yako.
Kamba za wasio haki zimenifunga,
Sikuisahau sheria yako.
(K) Unihuishe kwa fadhili zako,
nami nitazishika shuhuda za kinywa chako.
- Unikomboe na dhuluma ya mwanadamu,
nipate kuyashika mausia yako.
Wanakaribia wanaonifuatia kwa chuki,
wamekwenda mbali na sheria yako. (K) - Wokovu u mbali na wasio haki,
kwa maana hawajifunzi amri zako.
Nimewaona watendao uhaini nikachukizwa,
kwa sababu hawakulitii neno lako. (K)
INJILI: Lk 18:35-43
Yesu alipokaribia Yeriko, mtu mmoja kipofu alikuwa ameketi kando ya njia, akiomba sadaka; na alipowasikia makutano wakipita, aliuliza, Kuna nini? Wakamwambia, Yesu wa Nazareti anapita. Akapiga kelele, akisema, Yesu Mwana wa Daudi, unirehemu. Basi wale waliotangulia wakamkemea ili anyamaze; lakini yeye alizidi sana kupaza sauti, Ee Mwana wa Daudi, unirehemu. Yesu akasimama, akaamuru aletwe kwake; na alipomkaribia, alimwuliza, Wataka nikufanyie nini? Akasema, Bwana, nipate kuona. Yesu akamwambia, Upewe kuona; imani yako imekuponya. Mara hiyo akapata kuona, akamfuata, huku akimtukuza Mungu. Na watu wote walipoona hayo walimsifu Mungu.
TAFAKARI:
KUWA NA MSIMAMO MZURI KUNA MANUFAA: Injili ya leo ina simulizi la mtu aliyetaka kusaidiwa. Mtu huyu alikuwa mwombaji kwa sababu ya tatizo lake la upofu. Lakini, pia, aliujua uwezo wa Yesu kwani alikuwa tayari amepata kusikia kumhusu. Watu walijaribu kumzuia asipate msaada kutoka kwa Yesu, lakini yeye alisimama imara na kuendelea kuweka msisitizo. Yesu kwa kujua hilo, aliamua kumtimizia haja yake. Kutoka kwa Yesu, aliomba apate kuona. Hili lilikuwa zaidi ya pesa na vyakula alivyokuwa anwaomba watu. Alifahamu vyema kuwa, mara akipata kuona, ataepukana na kuwa ombaomba kwani atajifanyia kazi. Yesu anamfanya aone. Ni mara ngapi sisi hupata nafasi ya kuomba kitu lakini tunaomba visivyo. Huenda sisi huomba mabaya yawapate wale waliotutendea sivyo. Pengine sisi huomba vitu vya anasa ili tuwaringie wenzetu. Tuwe watu wa kuwaza kindani kabla ya kuomba. Tena kama huyu mwombaji wa siku ya leo, tuwe na msimamo dhabiti tuombapo. Leo hii tunashuhudia watu wakiyumbayumba kiimani, akiingia kwenye dini hii, anatoka na kesho yu kwingine. Tuwe na msimamo tuombapo.
SALA: Bwana utuponye kutokana na vilema vyetu hasa vya kukosa msimamo wa imani. Amina.