Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Mit. 31:10-13, 19-20, 30-31
Mke mwema, ni nani awezaye kumwona? Maana kima chake chapita kima cha marijani. Moyo wa mumewe humwamini, Wala hatakosa kupata mapato. Humtendea mema wala si mabaya, Siku zote za maisha yake. Hutafuta sufu na kitani; Taa yake haizimiki usiku. Hutia mikono yake katika kusokota; Na mikono yake huishika pia. Huwakunjulia maskini mikono yake; Naam, huwanyoshea wahitaji mikono yake. Upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili; Bali mwanamke amchaye Bwana, ndiye atakayesifiwa. Mpe mapato ya mikono yake, Na malangoni.
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 128:1-5
- Heri kila mtu amchaye Bwana
Aendaye katika njia yake.
Heri yao wale wamchao Bwana,
Utakuwa mwenye heri na baraka tele.
(K) Taabu ya mikono yako hakika utaila. - Mkeo kama mzabibu uzaao,
Vyumbani mwa nyumba yako.
Wanao kama miche ya mizeituni,
Wakiizunguka meza yao. (K) - Tazama, atabarikiwa hivyo, yule amchaye Bwana,
Bwana akubariki toka Sayuni,
Uone uheri wa Yerusalemu
Siku zote za maisha yako. (K)
SOMO 2: 1 Thes. 5:1-6
Ndugu zangu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie. Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku. Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa. Bali ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi. Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza. Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi.
SHANGILIO: Mt, 24 : 42, 44
Aleluya, aleluya,
Kesheni basi na kujiweka tayari,
Kwa maana hamjui saa atakayokuja,
Mwana wa Adamu.
Aleluya.
INJILI: Mt. 25:14-30
Ufalme wa mbinguni utafanana na mtu atakaye kusafiri, akawaita watumwa wake, akaweka kwao mali zake. Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri. Mara yule aliyepokea talanta tano akaenda, akafanya biashara nazo, akachuma faida talanta nyingine tano. Vile vile na yule mwenye mbili, yeye naye akachuma nyingine mbili faida. Lakini yule aliyepokea moja alikwenda akafukua chini, akaificha fedha ya bwana wake. Baada ya siku nyingi akaja bwana wa watumwa wale, akafanya hesabu nao. Akaja yule aliyepokea talanta tano, akaleta talanta nyingine tano, tazama talanta nyingine tano nilizopata faida. Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako. Akaja na yule aliyepokea talanta mbili, akasema, Bwana, uliweka kwangu talanta mbili, tazama, talanta nyingine mbili nilizopata faida. Bwana wake akamwambia, Vema mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako. Akaja na yule aliyepokea talanta moja, akasema, Bwana, nalitambua ya kuwa wewe u mtu mgumu, wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya; bali nikaogopa, nikaenda nikaificha talanta yako katika ardhi; tazama, unayo iliyo yako. Bwana wake akajibu, akamwambia, Wewe mtumwa mbaya na ulegevu, ulijua ya kuwa navuna nisipopanda, nakusanya nisipotawanya; basi, ilikupasa kuiweka fedha yangu kwa watoao riba; nami nikija ningalipata iliyo yangu na faida yake. Basi, mnyang’anyeni talanta hiyo, mpeni yule aliye nazo talanta kumi. Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele, lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa. Na mtumwa yule asiyefaa, mtupeni mbali katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.
TAFAKARI:
UMOJA KATIKA NDOA: Mafanikio katika ndoa, yamejikita juu ya kiasi ambacho ndoa imejengeka juu ya upendo, na ni kwa kiasi gani upendo huu unafanana na upendo wa Mungu. Mt. Paulo anaeleza sifa mbali mbali za upendo huo. Upendo hauhusudu, hautakabali, haukosi kuwa na adabu, hautafuti faida yake mwenyewe (1Kor 13:1-13). Kila mmoja wetu anazo sifa nyingi na nzuri alizojaliwa bure na Mungu. Hizi ndizo talanta ambazo bwana mwenye nyumba aliwapatia watumwa wake kabla hajasafiri. Matarajio yake Mwenyezi Mungu ni kuwa kila mmoja wetu anaendelea kuzikuza talanta alizokabidhiwa. Kuikuza huko ni kuzitumia kwa manufaa ya Mungu, na kwa kuwafaa wenzetu. Ndivyo anavyofanya mwanamke katika kitabu cha Mithali. Mwanamke huyu anasifiwa kwa vile anavitumia vipaji vyake kumletea mumewe furaha. Anashona nguo kwa ajili ya watoto wake, na anawasaidia masikini.
Dunia imejaa watu wa kila aina. Je, tunaye mke au mume ambaye ni mkamilifu? Kwenye ndoa, mume na mke wameapa kukamilishana. Ukamilisho huu huleta umoja ambao ni mkuu zaidi ya kila mmoja wao akiwa peke yake. Umoja huu huleta uhai, kila mmoja katika ndoa akimhuisha mwenzake. Kwa pamoja, viumbe vipya vinapata uhai pia. Kati ya wote wawili, hakuna aliye kamili peke yake. Ndiyo maana kila mmoja anamhitaji mwenzake, ndipo wakamilishane kupitia kwenye ahadi za ndoa. Useimi mkuu ni kuwa, “Nitakupenda leo na kesho na kesho kutwa. Nitakupenda hadi kifo kitakapotutenganisha. Nitatafuta faida yako na sio faida yangu hata kama utakuwa na tabia gani.” Hapa ndipo ukamilifu hupatikana. Kila mmoja, mke na mume, anazo talanta. Huu ndio utajiri ulio ndani ya kila mmoja. Kila mmoja amepewa bure. Je tuko tayari kuutambua utajiri tulio na na kuutumia kwa maslahi ya Mungu, Kanisa, jamii, na wenzetu?
Ufalme wa Mbinguni ndio uhusiano uliopo kati ya Mungu (mtoaji talanta), nami (mpokeaji talanta). Unapoishi vyema Sakramenti ya ndoa Takatifu, unaumba utume. Unasafiri katika utakatifu na ukamilifu. Katika upendo wa kimungu, heshima inazalisha talanta. Hatimaye sauti itasikika ikinena, “Njooni mshiriki furaha ya Bwana wenu.”
SALA: Tumeitwa na Mungu kuendeleza vipaji tulivyovipokea bure. Tuvitumie vyema kuwafaa wenzetu ili mwishowe tuje kuusikia mwaliko usemao, “Njooni mshiriki furaha yangu” Amina.