NOVEMBA 17, 2023; IJUMAA: JUMA LA 32 LA MWAKA

Mt. Elizabeti wa Ungaria
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Hek 13:1-9
Bila shaka wanadamu wote kwa asili ni ubatili, ambao hawana akili za kumtambua Mungu; tena hawakupata uwezo wa kumjua yeye aliopo kwa kuvitazama viumbe vizuri vinavyoonekana, wala kwa kuyaangalia yaliyofanywa hawakufahamu yule fundi aliyeyafanya. Walakini moto, ama upepo, ama hewa nyepesi, ama mzunguko wa nyota, ama mafuriko ya maji, ama mianga ya mbinguni walidhania kuwa ni miungu inayoutawala ulimwengu! Huenda ilikuwa kwa kupendezwa na uzuri wake walivyodhania viumbe hivyo kuwa ni miungu, basi na wajue kadiri gani Bwana, Mfalme wao, avipitavyo; kwa maana yeye aliye asili ya uzuri ndiye aliyeviumba.
Lakini kama ilikuwa kwa kuzistaajabia nguvu zake na maongozi yake, na wafahamu kwa kuviangalia kadiri gani yeye aliyeviumba anayo nguvu zaidi; maana kwa jinsi uzuri hata wa viumbe vilivyoumbwa ulivyo mkuu, kwa kadiri iyo hiyo mwanadamu huyatunga mawazo yake juu ya Muumba.
Walakini watu hao hawana hatia nyingi. Madhali yawezekana kwamba hao wamekosea tu, pindi wanapomtafuta Mungu, na kutamani kumwona; kwa sababu huishi katikati ya viumbe vyake, huvichunguza kwa bidii, na mwisho hujitoa kwa maono yao, mradi vitu vyenyewe wanavyovitazama ni vizuri kweli kweli.
Walakini tena watu hao hawana udhuru. Kwa maana wakiwa walikuwa na uwezo wa kufahamu kadiri hiyo. Hata kuweza kuchungulia taratibu ya viumbe, imekuwaje ya kwamba hawakudiriki upesi kumtambua Mfalme Mkuu wa viumbe hivyo vyake?

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 19:1-4

 1. Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu,
  Na anga laitangaza kazi ya mikono yake.
  Mchana husemezana na mchana,
  Usiku hutolea usiku maarifa.
  (K) Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu.
 2. Hakuna lugha wala maneno,
  Sauti yao haisikilikani.
  Sauti yao imeenea duniani mwote,
  Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu. (K)

INJILI: Lk 17:26-37
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa Adamu, walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakioa na kuolewa, hata siku ile Nuhu aliyoingia katika safina, gharika ikashuka ikawaangamiza wote. Na kadhalika, kama ilivyokuwa katika siku za Lutu, walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakinunua na kuuza, wakipanda na kujenga; lakini siku ile Lutu aliyotoka Sodoma kulikunya moto na kibiriti kutoka mbinguni vikawaangamiza wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile atakayofunuliwa Mwana wa Adamu.
Katika siku ile, aliye juu ya dari, na vyombo vyake vimo ndani ya nyumba, asishuke ili kuvitwaa; na kadhalika, aliye shambani asirejee nyuma. Mkumbukeni mkewe Lutu. Mtu ye yote atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza; na ye yote atakayeiangamiza ataiponya. Nawaambia, usiku huo watu wawili watakuwa katika kitanda kimoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa. Wanawake wawili watakuwa wakisaga pamoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa.
Wakajibu, wakamwuliza, Wapi, Bwana? Akawaambia, Ulipo mzoga, ndipo watakapokutanika tai.

TAFAKARI:
HAKIKA MUNGU YUPO: Ukiangalia ulimwengu na vilivyomo, utapata tafakari kubwa na sio ajabu ukabaki ukishangaa. Kuna vinavyopendeza na kutisha kwa jinsi vilivyoratibishwa. Mfano wanyama wa porini, mapori, milima, bahari na hata uwezo wa mwanadamu anavyoweza kuunda mitambo mikubwa ya kutisha (viwanda, ndege, meli na vinginevyo). Haya yote ukiyatafakari utaona wazi kuwa kuna nguvu inayowezesha hayo kuwa hivyo. Ndio maana mwandishi wa somo la kwanza anasema, kama mwanadamu hatakiri kuwa kuna Mungu anayewezesha hayo yote, basi ni ubatili tu. Na Luka katika Injili anaelezea jinsi mwanadamu anavyohangaika na shughuli za ulimwengu huu na kama zitamfanya amsahau Mungu basi ataishia pabaya, ataangamia. Wahenga wanasema, “Ukiviona vyaelea ujue vimeundwa”. Huu ni mwaliko kwetu sote kuwa tukubali Mungu yupo na ndiye anayeratibisha yote. Tusiamini katika uwezo mwingine wowote. Kuna mtu mmoja alitoa kichekesho akasema ‘afadhali uamini kuwa Mungu yupo na ukifa ukakuta hayupo, hutakuwa umepoteza, kuliko uishi na kuamini kuwa Mungu hayupo halafu ukifa unaenda kuta yupo, itakuwa kazi tete’. Usemi huu waweza kuonekana kuwa kichekesho tu bali unao ujumbe mzito.

SALA: Mungu Mwenyezi, tujalie tuamini katika uwepo na uwezo wako. Amina.