Mt. Leo Mkuu, Baba Mt. na Mwalimu wa Kanisa
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Rum 15:14-21
Ndugu zangu, nimehakikishwa mimi mwenyewe kwa habari zenu ya kuwa ninyi nanyi mmejaa wema, mmejazwa elimu yote, tena mwaweza kuonyana. Lakini nawaandikia, kwa ujasiri zaidi katika sehemu za waraka huu, kana kwamba kuwakumbusha, kwa neema ile niliyopewa na Mungu, ili niwe mhudumu wa Kristo Yesu kati ya watu wa Mataifa, niifanyie Injili ya Mungu kazi ya ukuhani, kusudi Mataifa wawe sadaka yenye kibali, ikiisha kutakaswa na Roho Mtakatifu. Basi, nina sababu ya kuona fahari katika Kristo Yesu mbele za Mungu. Maana sitadhubutu kutaja neno asilolitenda Kristo kwa kazi yangu, mataifa wapate kutii, kwa neno au kwa tendo, kwa nguvu za ishara na maajabu, katika nguvu za Roho Mtakatifu; hata ikawa tangu Yerusalemu, na kando kando yake, mpaka lliriko nimekwisha kuihubiri Injili ya Kristo kwa utimilifu; kadhalika nikijitahidi kuihubiri Injili, nisihubiri hapo ambapo jina la Kristo limekwisha kutajwa, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine; bali kama ilivyoandikwa, Wale wasiohubiriwa habari zake wataona, Na wale wasiojasikia watafahamu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 98:1-4
- Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtenda wokovu.
(K) Bwana ameufunua wokovu wake. - Bwana ameufunua wokovu wake,
Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K) - Miisho yote ya dunia imeuona,
Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)
INJILI: Lk 16:1-8
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyekuwa na wakili wake; huyu alishitakiwa kwake kuwa anatapanya mali zake. Akamwita, akamwambia, Ni habari gani hii ninayosikia juu yako? Toa hesabu ya uwakili wako, kwa kuwa huwezi kuwa wakili tena. Yule wakili akasema moyoni mwake, Nifanyeje? Maana, bwana wangu ananiondolea uwakili. Kulima, siwezi; kuomba, naona haya. Najua nitakalotenda, ili nitakapotolewa katika uwakili, wanikaribishe nyumbani mwao. Akawaita wadeni wa bwana wake, kila mmoja; akamwambia wa kwanza, Wawiwani na bwana wangu? Akasema, Vipimo mia vya mafuta. Akamwambia, Twaa hati yako, keti upesi, andika hamsini. Kisha akamwambia mwingine, Na wewe wawiwani? Akasema, Makanda mia ya ngano. Akamwambia, Twaa hati yako, andika themanini.
Yule bwana akamsifu wakili dhalimu kwa vile alivyotenda kwa busara; kwa kuwa wana wa ulimwengu huu katika kizazi chao wenyewe huwa na busara kuliko wana wa nuru.
TAFAKARI:
MADARAKA NI YA MPITO: Paulo alijaribu kutumia ipasavyo bahati aliyojaliwa na Mungu ya kuhubiri Injili. Anatenda tu lile aliloagizwa na Kristo. Katika Injili, Yesu katika mfano wake amemwelezea huyu wakili kama mtu aliyejisahau akatumia sivyo madaraka yake na hivi kibarua chake kikafika ukingoni. Anatualika na sisi tuangalie jinsi tunavyotumia fursa tunazokutana nazo. Kuna watu ambao hupata vyeo na mara wanajisahau na kujiona kuwa mungu mtu. Hawa hawaambiliki, hawawasikilizi wengine, hawapokei ushauri wa wengine, bali wanajiona wao ndio wao. Siku inapokuja kuwa sasa wameondolewa katika ofisi husika, huwa shida kwao kuchangamana na jamii. Kunaye tajiri mmoja aliyejisahau hata akafanya kufuru ya kulimwagia gari pombe. Alifanya hivyo eti anamshukuru Mungu kwani hana tena umasikini. Inasemekana kuwa haikupita miaka miwili, huyu bwana akafilisika na kuwa masikini hohehahe. Kila tulicho nacho kimetoka kwa Mungu. Yote tumepewa na Mungu kwa kuwafaa wasiobahatika kama sisi. Tusijisahau kamwe kwa ajili ya uhai, afya, vyeo, na mali tulizojaliwa. Tunaalikwa tutembee na Mungu katika kila hatua ya maisha, tusijione tunajiweza. Mweza ni yeye peke yake.
SALA: Mungu Baba Mwenyezi, tunaomba utuwezeshe kutumia vyema madaraka tunayokabidhiwa. Amina.