Mt. Godfrei wa Amiens, Askofu
Kijani
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Rum 13:8-10
Msiwiwe na mtu cho chote, isipokuwa kupendana; kwa maana ampendaye mwenzake ameitimiza sheria. Maana kule kusema, Usizini, Usiue, Usiibe, Usitamani, na ikiwapo amri nyingine yo yote, inajumlishwa katika neno hili, ya kwamba, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Pendo halimfanyii jirani neno baya; basi pendo ndilo utimilifu wa sheria.
WIMBO WA KATIKATI Zab.112:1-2, 4-5, 9
- Aleluya.
Heri mtu yule amchaye Bwana,
Apendezwaye sana na maagizo yake.
Wazao wake watakuwa hodari duniani;
Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa.
(K) Heri atendaye fadhili na kukopesha. - Nuru huwazukia wenye adili gizani;
Ana fadhili na huruma na haki.
Heri atendaye fadhili na kukopesha;
Atengenezaye mambo yake kwa haki. (K) - Amekirimu, na kuwapa maskini,
Haki yake yakaa milele,
Pembe yake itakuzwa kwa utukufu. (K)
INJILI: Lk 14:25-33
Makutano mengi walipokuwa wakifuatana na Yesu, aligeuka, akawaambia, Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume kwa wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza. Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini? Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule akali mbali. Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
TAFAKARI:
UPENDO NDIO UTIMILIFU WA YOTE: Ukisoma somo la kwanza na Injili, kwa haraka haraka unaweza kudhani kuwa yanapingana. Somo la kwanza linadai tupendane, nayo katika Injili Yesu anasema tuwachukie wazazi na hata ndugu kwa ajili yake. Amri ya nne ya Mungu inatutaka tuwaheshimu wazazi. Itakuwaje tuwaheshimu, na leo tena tunaaambiwa tuwachukie! Paulo akiwaandikia Warumi (13:8-10) ameeleza vizuri kuwa upendo wetu kwa jirani uwe kama ule tulio nao kwetu sisi wenyewe. Kristo anaposema tuchukue msalaba na kumfuata yeye, anahimiza kwa kina ujumbe wake. Kaika kumfuata Kristo, yeye tu awe kielelezo chetu, bali si wazazi, ndugu au marafiki. Kuna wakati mwingine tunapojikuta tunafanya mambo ili kuwaridhisha wazazi, ndugu na marafiki. Wanakuwa ndio kigezo cha kutenda. Tunashauriwa leo kuwa, kipimo chetu cha utendaji mwema, kiwe Kristo. Tusiwaridhishe wenzetu na kumuudhi Kristo. Kinyume na hayo, tumridhishe Kristo hata ikiwa kwa kutenda hayo tutawaudhi wenzetu.
SALA: Yesu wa mapendo, tujalie tupendane bila unafiki. Amina.