Mt. Martino wa Porres, Mtawa
Kijani
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Rum 9: 1-5
Nasema kweli katika Kristo, sisemi uongo, dhamiri yangu ikinishuhudia katika Roho Mtakatifu, ya kwamba nina huzuni nyingi na maumivu yasiyokoma moyoni mwangu. Kwa maana ningeweza kuomba mimi mwenyewe niharimishwe na kutengwa na Kristo kwa ajili ya ndugu zangu, jamaa zangu kwa jinsi ya mwili; ambao ni Waisraeli, wenye kule kufanywa wana, na ule utukufu, na maagano, na kupewa torati, na ibada ya Mungu, na ahadi zake; ambao mababu ni wao, na katika hao alitoka Kristo kwa jinsi ya mwili. Ndiye aliye juu ya mambo yote, Mungu, mwenye kuhimidiwa milele.
WIMBO WA KATIKATI: Zab 147: 12-13. 14-15. 19-20
- Msifu Bwana, Ee Yerusalemu;
Msifu Mungu wako, Ee Sayuni.
Maana ameyakaza mapingo ya malango yako,
Amewabariki wanao ndani yako.
(K) Msifu Bwana Ee Yerusalemu. - Ndiye afanyaye amani mipakani mwako,
Akushibishaye kwa unono wa ngano.
Huipeleka amri yake juu ya nchi,
Neno lake lapiga mbio sana. (K) - Humhubiri Yakobo neno lake,
Na Israeli amri zake na hukumu zake.
Hakulitendea taifa lo lote mambo kama hayo,
Wala hukumu zake hawakuzijua.
Aleluya. (K)
INJILI: Lk 14: 1-6
Yesu alipoingia ndani ya nyumba ya mtu mmoja miongoni mwa wakuu wa Mafarisayo siku ya Sabato, ale chakula, walikuwa wakimvizia. Na tazama, mbele yake palikuwa na mtu mwenye ugonjwa wa safura. Yesu akajibu, akawaambia wana-sheria na Mafarisayo, je! Ni halali kuponya siku ya Sabato, ama sivyo? Wao wakanyamaza. Akamshika, akamponya, akamruhusu aende zake. Akawaambia, Ni nani miongoni mwenu, ikiwa ng’ombe wake au punda wake ametumbukia kisimani, asiyemwopoa mara hiyo siku ya Sabato? Nao hawakuweza kujibu maneno haya.
TAFAKARI:
UTU UNAVUKA MIPAKA YA SHERIA: Mwanadamu ni kiumbe anayependa kuongozwa na kusimamiwa na sheria. Sheria au taratibu zinakuwepo ili zilete haki na hivyo haipaswi tuwe watumwa wa sheria hizo, mahali pengine inatakiwa iwepo tafsiri sahihi ya sheria husika na hasa inapohusu uhai wa mtu. Sheria yaweza kukataza lakini kwa mazingira fulani inabidi iangaliwe kipekee. Mfano, wewe ni dereva wa bosi fulani na kwa mujibu wa taratibu zako za ajira huruhusiwi kumpa mtu lifti. Sasa imetokea uko njiani na umekutana na watu wana mgonjwa na wanahitaji msaada wa kufikishwa hospitalini. Hapa ni suala la kuokoa maisha ya huyu mgonjwa, katika mazingira kama haya. Sheria ya bosi wako ya kutokumpa mtu lifti inabidi ikiukwe. Waweza kuhatarisha hata ajira yako kama Yesu alivyohatarisha maisha yake kwa kukiuka utaratibu wa jamii ile kama Injili. Nia ni kuokoa uhai na kuujali utu. Nasi tunaalikwa kujali uhai wa wenzetu hata kama itapelekea kuingia katika matatizo au kutoeleweka.
SALA: Bwana Yesu tupe Neema zako tuweze kuwajali wenye shida.Amina.