NOVEMBA 1, 2023; JUMATANO: JUMA LA 30 LA MWAKA

WATAKATIFU WOTE
Sherehe
Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku

SOMO 1: Ufu. 7:2-4, 9-14
Mimi Yohane, niliona malaika mwingine, akipanda kutoka maawio ya jua, mwenye muhuri ya Mungu aliye hai; akawapigia kelele kwa sauti kuu wale malaika wanne waliopewa kuidhuru nchi na bahari, akisema, Msiidhuru nchi, wala bahari, wala miti, hata tutakapokwisha kuwatia muhuri watumwa wa Mungu wetu juu ya vipaji vya nyuso zao. Nikasikia hesabu yao waliotiwa muhuri katika kabila ya Waisraeli, watu mia na arobaini na nne elfu. Baada ya hayo nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za mwana-kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao; wakilia kwa sauti kuu wakisema, Wokovu una Mungu wetu aketiye katika kiti cha enzi, na mwana-kondoo. Na malaika wote walikuwa wakisimama upande zote za kile kiti cha enzi, na za hao wazee, na za wale wenye uhai wanne, na wakaanguka kifulifuli mbele ya kile kiti cha enzi, wakamsujudu Mungu, wakisema, Amina; baraka na utukufu na hekima na shukrani na heshima na uweza na nguvu zina Mungu wetu hata milele na milele. Amina. Akajibu mmoja wa wale wazee akiniambia, Je! Watu hawa waliovikwa mavazi meupe ni akina nani? Nao wametoka wapi? Nikamwambia, Bwana wangu, wajua wewe. Akaniambia, Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-kondoo.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 24:1-6

 1. Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana,
  Dunia na wote wakaao ndani yake.
  Maana ameiweka misngi yake juu ya bahari,
  Na juu ya mito ya maji aliithibitisha.
  (K) Hiki ndicho kizazi cha wakutafutao, Ee Bwana.
 2. Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana?
  Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?
  Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe,
  Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili. (K)
 3. Atapokea baraka kwa Bwana,
  Na haki kwa Mungu wa wokovu wake.
  Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao,
  Wakutafutao uso wako, E Mungu wa Yakobo. (K)

SOMO 2: 1 Yoh. 3:1-3
Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye. Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo. Na kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa; kama yeye alivyo mtakatifu.
SHANGILIO: Mt. 11 :28
Aleluya, aleluya,
Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao
Na wenye kulemewa na mizigo,
Nami nitawapumzisha,
Asema Bwana.
Aleluya.

INJILI: Mt. 5:1-12
Yesu alipowaona makutano, alipanda mlimani; na alipokwisha kuketi, wanafunzi wake walimjia; akafumbua kinywa chake, akawafundisha, akisema, Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri wenye huzuni; Maana hao watafarijika. Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi. Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa. Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema. Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu. Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu. Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.

TAFAKARI:
UTAKATIFU: Ni jambo jema kuishi maisha matakatifu kuliko kuzungumzia maisha matakatifu. Sherehe hii inanuia kutuhimiza kuuishi utakatifu. Ni baadhi tu ya watakatifu walioko mbinguni ambao wametangazwa na Kanisa. Kanisa linafanya hivyo likiangalia mambo makuu waliyoyafanya wakiwa humu duniani, kama vile kuishi maisha ya fadhila, kutenda miujiza, kuyaacha maisha ya anasa kwa ajili ya Mungu, kuishi maisha ya toba jangwani, kati ya mengine mengi. Si kwamba waliichukia jamii bali kwao waliipa kipaumbele tamaa ya kuyaishi maisha ndani ya mpango wa Mungu. Waliziishi Heri zilizotajwa leo, ambazo zinaelekezea utakatifu. Kwa hiyo walijikakamua zaidi kumjua na kumwishia Kristo. Kupitia kwa Heri, Roho Mtakatifu anatuongoza jinsi alivyowaongoza watakatifu. Tuwaige watakatifu, ambao walikuwa binadamu kama sisi, bali kwa juhudi zao na kujitolea kwao, walifaulu. Ila tusisahau kuwa Mkuu ni Yesu. Ndiye Nafsi ya Pili ya Mungu. Tujiulize Je! ni mara ngapi tumemwendea Yesu wa Ekaristi kuongea naye na kumweleza shida zetu? Je! tumewahi kukaa walau saa moja karibu na tabernakulo na kumweleza Yesu shida za familia zetu, watoto wetu, wake zetu au waume zetu? Wapendwa, watakatifu wako kwa ajili ya kutuombea. Tunalopaswa kufanya ni kuwaomba watakatifu watuombee kwa Mungu. Basi tumwombe Kristo atusaidie ili nasi kwa mifano ya watakatifu waliofuata nyayo zake tuweze kuufikia utakatifu.

SALA: Enyi watakatifu, zichukueni sala zetu na mzipeleke mbinguni kwa niaba yetu. Tamaa yetu Takatifu ikamilike kutokana na sala mnazozitoa kwa Baba. Amina.