OKTOBA 31, 2023; JUMANNE: JUMA LA 30 LA MWAKA

Mt. Marseli, Shahidi
Kijani
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Rum 8:18-25
Nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunulliwa kwetu. Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu. Kwa maana viumbe vyote pia vilitiishwa chini ya ubatili; si kwa hiyari yake, ila kwa sababu yake yeye aliyevitiisha katika tumaini; kwa kuwa viumbe vyenyewe navyo vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu, hata viingie katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.
Kwa maana twajua ya kuwa viumbe vyote pia vinaugua pamoja, navyo vina utungu pamoja hata sasa. Wala si hivyo tu; ila na sisi wenyewe tulio na malimbuko ya Roho, sisi pia tunaugua katika nafsi zetu, tukikutazamia kufanywa wana, yaani, ukombozi wa mwili wetu. Kwa maana tuliokolewa kwa taraja; lakini kitu kilichotarajiwa kikionekana, hakuna taraja tena. Kwa maana ni nani anayekitarajia kile akionacho? Bali tukikitarajia kitu tusichokiona, twakingojea kwa subira.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 126

  1. Bwana alipowarejeza mateka wa Sayuni,
    Tulikuwa kama waotao ndoto.
    Ndipo kinywa chetu kilipojaa kicheko,
    Na ulimi wetu kelele za furaha.
    (K) Bwana alitutendea mambo makuu.
  2. Ndipo waliposema katika mataifa,
    Bwana amewatendea mambo makuu.
    Bwana alitutendea mambo makuu,
    Tulikuwa tukifurahi. (K)
  3. Ee Bwana, uwarejeze watu wetu waliofungwa,
    Kama vijito vya Kusini.
    Wapandao kwa machozi,
    Watavuna kwa kelele za furaha. (K)
  4. Ingawa mtu anakwenda zake akilia,
    Azichukuapo mbegu za kupanda.
    Hakika atarudi kwa kelele za furaha,
    Aichukuapo miganda yake. (K)

INJILI: Lk 13:18-21
Yesu alisema, Ufalme wa Mungu umefanana na nini? Nami niufananishe na nini? Umefanana na punje ya haradali aliyotwaa mtu akaitupa katika shamba lake; ikamea, ikawa mti; ndege wa angani wakakaa katika matawi yake. Akasema mara ya pili, Niufananishe na nini ufalme wa Mungu? Umefanana na chachu aliyotwaa mwanamke akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachacha wote pia.

TAFAKARI:
TUMEPOKEA MATUNDA YA UFALME WA MUNGU: Kristo anaelezea Ufalme wa Mungu kwanza kwa kutumia punje ya haradali. Ikiota inamea na kuwa mti mkubwa wenye faida kwa ndege wa angani. Injili ilianza kama jambo dogo kati ya Kristo na mitume wake kumi na wawili. Baadaye jamuiya ya mitume na wafuasi. Injili ilikua na kuenea ulimwenguni kote. Humu Afrika Mashariki tunayo mifano ya Tanzania na Kenya. Humu Tanzania ilianzia mwaka wa 1868 kwa harakati za uinjilishaji za wamisionari wa Konsolata, Wamisionari wa Afrika na Wabenediktini. Bagamoyo ikawa chimbuko la injili. Huko Kenya, walikuwa ni wamisionari wa Roho Mtakatifu mwaka wa 1864. Leo hii, mbegu hiyo sasa ni mti mkubwa, ulio na matawi kuelekea kila eneo la nchi hizi. Kumekuwa na mashule, mahospitali na makanisa mengi yaliyojengwa ili kuwahudumia Wakristo. Kumekuwa na watawa wengi wa kiume na kike, mapadre wa jimbo, makatekista na Wakatoliki chungu nzima. Kweli haya ndiyo matunda ya wokovu wa mwanadamu na utukufu wa Mungu. Inatupasa kumshukuru Mungu kwa Injili iliyotufikia na tumwombe atusaidie kuikumbatia.

SALA; Baba Ufalme wako ufike.Amina.