OKTOBA 24, 2023; JUMANNE: JUMA LA 29 LA MWAKA

Mt. Antoni Maria Clare, Askofu
Kijani
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Rum 5:12, 15, 17-21
Kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi.
Kwa maana ikiwa kwa kukosa kwake yule mmoja wengi walikufa, zaidi sana neema ya Mungu, na kipawa kilicho katika neema yake mwanadamu mmoja Yesu Kristo kimezidi kwa ajili ya wale wengi. Kwa maana ikiwa kwa kukosa mtu mmoja mauti ilitawala kwa sababu ya yule mmoja, zaidi sana wao wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki watatawala katika uzima kwa yule mmoja, Yesu Kristo basi tena, kama kwa kosa moja watu wote walihukumiwa adhabu, kadhalika kwa tendo moja la haki watu wote walihesabiwa haki yenye uzima. Kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki. Lakini sheria iliingia ili kosa lile liwe kubwa sana; na dhambi ilipozidi, neema ilikuwa nyingi zaidi; ili kwamba, kama vile dhambi ilivyotawala katika mauti, vivyo hivyo kwa njia ya haki neema itawale hata uzima wa milele kwa Yesu Kristo Bwana wetu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 40:6-9, 17

 1. Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo,
  Masikio yangu umeyazibua,
  Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.
  Ndipo niliposema, Tazama nimekuja.
  (K) Tazama nimekuja, Ee Bwana. Kuyafanya mapenzi yako.
 2. Katika gombo la chuo nimeandikwa;
  Kuyafanya mapenzi yako,
  Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu;
  Naam, sheria yako imo moyoni mwangu. (K)
 3. Nimehubiri habari za haki katika kusanyiko kubwa,
  Sikuizuia midomo yangu; Ee Bwana, najua. (K)
 4. Nami ni maskini na mhitaji,
  Bwana atanitunza.
  Ndiwe msaada wangu na Mwokozi wangu,
  Ee Mungu wangu, usikawie. (K)

INJILI: Lk 12:35-38
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka; nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara. Heri watumwa wale, ambao bwana wao ajapo atawakuta wanakesha. Amin, nawaambieni, atajifunga na kuwakaribisha chakulani, atakuja na kuwahudumia. Na akija zamu ya pili, au akija zamu ya tatu, na kuwakuta hivi, heri watumwa hao.

TAFAKARI:
NEEMA YA MUNGU INAYAZIDI MADHAIFU YETU: Hali ya mwanadamu wa sasa imejikita upande mmoja, kwa ukosefu wa Adamu na upande mwingine kwa utii wa Kristo. Kwa kosa la Adamu, wanadamu wote waliingia katika dhambi. Na kwa tendo la utii wa Kristo hadi kufa, mwanadamu alikombolewa kwa neema kubwa. Hata hivyo, ukombozi wa mwanadamu unajengeka kwenye imani yake kwa Mungu. Hata kama imani yake ni kubwa, inategemea neema kutoka kwa Mungu. Hayapo mashindano yoyote kati ya dhambi ya mwanadamu na neema za Mungu, kwani neema ya Mungu ni kuu kuliko dhambi ya mwanadamu. Simulizi la dhambi ya Adamu kwa mafundisho ya Mtume Paulo linaambatana na neema ya huruma ya Mungu kwa kifo cha Kristo. Hili ni fundisho kwa kila muumini. Ulimwengu wa sasa unashuhudia maasi ya mwanadamu, na kwa wanadamu. Waumini wasije wakajisalimisha kwenye mikono ya yule mwovu. Dhambi haijaizidi neema ya Mungu. Maisha ya kila muumini yanapaswa kushuhudia kwamba nguvu za Mungu zinauzidi udhaifu wa mwanadamu.

SALA: Ee Mungu Baba, utujalie hekima ya kutambua wingi wa rehema zako juu yetu. Amina.