OKTOBA 19, 2023; ALHAMISI: JUMA LA 28 LA MWAKA

Wat. Yohane Brebe na Isaaki Yog, Mapadre na Wenzake Mashahidi /Mt. Paulo wa Msalaba, Padre
Kijani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Rum 3:21-30
Haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na torati na manabii; ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti; kwa sababu wote wamefanya dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake, ili aoneshe haki yake. Kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa Mungu dhambi zote zilizotangulia kufanywa; apate kuonesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yeye amwaminiye Yesu. Ku wapi, basi, kujisifu? Kumefungiwa nje. Kwa sheria ya namna gani? Kwa sheria ya matendo? La! Bali kwa sheria ya imani. Basi, twaona ya kuwa mwanadamu huhesabiwa haki kwa imani pasipo matendo ya sheria. Au je? Mungu ni Mungu wa Wayahudi tu? Siye Mungu wa Mataifa pia? naam, ni Mungu wa Mataifa pia; kama kwa kweli Mungu ni mmoja.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 130:1-6

  1. Ee Bwana, toka vilindini nimekulilia.
    Bwana, uisikie sauti yangu.
    Masikio yako na yaisikilize
    Sauti ya dua zangu.
    (K) Kwa Bwana kuna fadhili na ukombozi mwingi.
  2. Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu,
    Ee Bwana, nani angesimama?
    Lakini kwako kuna msamaha,
    Ili Wewe uogopwe. (K)
  3. Nimemngoja Bwana, roho yangu imengoja;
    Na neno lake nimelitumainia.
    Nafsi yangu inamngoja Bwana,
    Kuliko walinzi waingojavyo asubuhi,
    Naam, walinzi waingojao asubuhi. (K)

INJILI: Lk 11:47-54
Yesu aliwaambia wanasheria: Ole wenu, kwa kuwa mwajenga maziara ya manabii, na baba zenu ndio waliowaua. Basi, mwashuhudia na kuziridhia kazi za baba zenu; kwa kuwa wao waliwaua nanyi mwawajengea maziara. Na kwa sababu hiyo hekima ya Mungu ilisema, Tazama, nitatuma kwao manabii na mitume, nao watawaua baadhi yao na kuwafukuza, ili kwa kizazi hiki itakwe damu ya manabii wote, iliyomwagika tangu kupigwa msingi wa ulimwengu; tangu damu ya Habili hata damu ya Zakaria, aliyeuawa kati ya madhabahu na hekalu. Naam, nawaambieni ya kwamba itatakwa kwa kizazi hiki. Ole wenu, enyi wana-sheria, kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa maarifa; wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia. Alipotoka humo, waandishi na Mafarisayo walianza kumsonga vibaya, na kumchokoza kwa maswali mengi, wakimvizia, ili wapate neno litokalo kinywani mwake.

TAFAKARI:
TWAHESABIWA HAKI KWA NEEMA YA MUNGU: Ulimwengu wote umegubikwa na binadamu wadhambi. Lakini, neema ya wokovu kwa njia ya Kristo imezidi uzito wa dhambi. Wayahudi waliamini kwamba mwanadamu anaweza kujistahilisha mwenyewe neema za Mungu kwa kuzingatia torati. Hata hivyo, juhudi za mwanadamu zinategemea zaidi rehema ya Mungu kama zawadi ili kupata neema. Mtume Paulo anahimiza sana kupitia barua kwa Warumi kuwa, ukombozi unategemea neema za Mungu. Hata kama Mungu ana uwezo wa kufanya hivyo, hamkomboi mwanadamu pasipo ushiriki wake. Vile vile, mwanadamu kwa juhudi zake zote hawezi kujikomboa mwenyewe bila rehema kama zawadi kutoka kwa Mungu. Amri na sheria zinapaswa kumwandaa mwanadamu kupokea neema za Mungu. Katika injili, Kristo anawalaumu wanasheria kwa jinsi wanavyoitumia sheria kama lengo na sio kama njia ya kufikia lengo. Waumini wanahimizwa kufanya kila juhudi iwezekanayo ili kujitakatifuza. Sala, ibada na matendo ya huruma vinamwandaa muumini na kumsaidia kumkaribia Mungu. Lakini yote kutoka kwa Mungu yanapokelewa kama zawadi za kiroho na sio kwa mastahili.

SALA: utujalie Ee Bwana kujitayarisha ipasavyo kuzipokea neema zako. Amina.