OKTOBA 17, 2023; JUMANNE: JUMA LA 28 LA MWAKA

Mt. Inyasi wa Antiokia, Askofu na Shahidi
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Rum 1:16-25
Siionei haya Injili, kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia. Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa, mwenye haki ataishi kwa imani.
Kwa maana ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni juu ya uasi wote na uovu wa wanadamu waipingao kweli kwa uovu. Kwa kuwa mambo ya Mungu yanayojulikana yamekuwa dhahiri ndani yao, kwa maana Mungu aliwadhihirishia. Kwa sababu mambo yake yasiyoonekana tangu kuumbwa ulimwengu yameonekana, na kufahamika kwa kazi zake; yaani, uweza wake wa milele na Uungu wake; hata wasiwe na udhuru; kwa sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza. Wakijinena kuwa wenye hekima walipumbazika; wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege, na ya wanyama, na ya vitambaavyo. Kwa ajili ya hayo Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao, waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima miili yao. Kwa maana waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakikusudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 19:1-4

  1. Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu,
    Na anga laitangaza kazi ya mikono yake.
    Mchana husemezana na mchana,
    Usiku hutolea usiku maarifa.
    (K) Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu.
  2. Hakuna lugha wala maneno,
    Sauti yao haisikilikani.
    Sauti yao imeenea duniani mwote,
    Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu. (K)

INJILI: Lk 11:37-41
Yesu alipokuwa akinena, Farisayo mmoja alimwita aje kwake ale chakula; akaingia, akaketi chakulani. Farisayo huyo alipomwona, alistaajabu kwa sababu hakunawa kabla ya chakula. Bwana akamwambia, Ninyi Mafarisayo mwasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani yenu mmejaa unyang’anyi na uovu. Enyi wapumbavu; aliyevifanya vya nje, siye yeye aliyevifanya vya ndani pia? Lakini, toeni sadaka vile vya ndani, na tazama, vyote huwa safi kwenu.

TAFAKARI:
ISHARA ZIANDAMANE NA IBADA YA KWELI: Maneno ya Yesu huenda yakasikika kuwa makali kwa mwenyeji wake. Wanapomshangaa kwamba hajanawa kama ilivyokuwa desturi ya Kiyahudi, Kristo anawajibu kwa lugha iliyonyooka. Kwamba Wafarisayo walisafisha vyombo kwa nje lakini ndani mwao kulijaa uchafu na uovu. Anawaita wapumbavu kwa misimamo yao yanayoegemea zaidi ishara na matendo ya nje yasioambatana na ibada ya mioyoni mwao. Mtume Paulo anatumia lugha sawia anaposema, “Walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza.” Kristo hakuvumilia unafiki, hasa ulipotoka kwa viongozi waliostahili kuwa mfano mwema. Hili ni fundisho kwa waumini na kwa Kanisa. Tuna ibada nyingi na maadhimisho tunayoyafanya ndani ya mwaka mzima wa Kanisa. Itakuwa huzuni sana kama maadhimisho yote ya ibada, Sakramenti na visakramenti itaishia nje tu. Sharti ishara zote za nje ziambatane na ibada ya kweli ya waumini. Vinginevyo, yatabaki maigizo na tutaishia kwenye kundi la wanaolaumiwa na Kristo.

SALA: tunapoadhimisha ibada zetu, tujaliwe kuambatanisha mioyo yetu na ibada hizo. Amina.