Mt. Hedwiga, Mtawa/ Mt. Margarita Alakok, Bikira
Kijani
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: Rum 1:1-7
Paulo, mtumwa wa Yesu Kristo Yesu, aliyeitwa kuwa mtume, na kutengwa aihubiri Injili ya Mungu; ambayo Mungu amekwisha kuiahidi kwa kinywa cha manabii wake katika Maandiko Matakatifu; yaani habari za mwanawe, aliyezaliwa katika ukoo wa Daudi kwa jinsi ya mwili. Na kudhihirishwa kwa uweza kuwa mwana wa Mungu, kwa jinsi ya roho ya utakatifu, kwa ufufuo wa wafu, Yesu Kristo Bwana wetu; ambaye katika yeye tulipokea neema na utume ili mataifa yote wapate kujitiisha kwa imani, kwa ajili ya jina lake; ambao katika hao ninyi mmekuwa wateule wa Yesu Kristo; kwa wote walioko Rumi, wapendwao na Mungu, walioitwa kuwa watakatifu. Neema na iwe kwenu na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo.
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 98:1-4
- Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
(K) Bwana ameufunua wokovu wake. - Bwana ameufunua wokovu wake,
Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K) - Miisho yote ya dunia imeuona
Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)
INJILI: Lk 11:29-32
Makutano walipokuwa wakimkusanyikia, Yesu alianza kusema, Kizazi hiki ni kizazi kibaya; kinatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya Yona. Maana, kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa Waninawi, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu kwa kizazi hiki. Malkia wa Kusini ataondoka siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa na hatia; kwa sababu yeye alikuja kutoka nchi za dunia aisikie hekima ya Sulemani; na hapa pana mkubwa kuliko Sulemani. Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na kizazi hiki, nao watakihukumu kuwa na hatia; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona, na hapa pana mkubwa kuliko Yona.
TAFAKARI:
MTAFUTENI MUNGU SIO MIUJIZA: Makutano wanamfuata Yesu baada ya kusikia matendo yake. Lakini kila mmoja anamfuata kwa sababu tofauti. Kati yao, wapo wanaohitaji kuponywa. Wengine wanashabikia, lakini wengine wanafika kwa kutarajia kushuhudia miujiza. Anawarejesha kwenye ishara ya nabii Yona kukaa ndani ya samaki kwa siku tatu. Hii inaashiria ishara ya Kristo mwenyewe kukaa chini ya ardhi siku tatu kabla ya ufufuko wake. Anatumia mfano wa toba ya watu wa Ninawi. Kwani baada ya kusikia ujumbe wa nabii Yona, walitubu na kupata rehema ya Mungu. Hata baada ya kushuhudia miujiza na matendo mengi ya Kristo, makutano haya hayakubadilika, ila yaliendelea kutaka kushuhudia miujiza zaidi. Yaliyotendeka mbele yao yalilenga kuwafumbulia Ufalme wa Mungu na kuwajengea imani kwa Mungu. Lakini walibaki katika ishara pekee. Mt. Paulo anapowaandikia Warumi anahimiza kwamba yote yalitendeka kwa lengo la kuwasidia watu kumjua Mungu, “Ambaye katika yeye tulipokea neema na utume ili mataifa yote wapate kujitiisha kwa imani.” Uhusiano wetu na Mungu unapaswa kukomaa na kuzidi kiwango cha kwenda kanisani kwa sababu tu ya kutafuta maslahi.
SALA: Utujalie Ee Bwana, kuja kwako kwa ajili upendo tulio nao kwako na sio kwa kutanguliza mahitaji yetu. Amina.