OKTOBA 15, 2023; DOMINIKA YA 28 YA MWAKA

Kijani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Isa. 25:6-10
Katika mlima huu Bwana wa majeshi atawafanyia mataifa yote karamu ya vitu vinono, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, karamu ya vinono vilivyojaa mafuta, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, iliyochujwa sana. Naye katika mlima huu atauharibu uso wa sitara iliyowekwa juu ya watu wote, na utaji ule uliotandwa juu ya mataifa yote. Amemeza mauti hata milele; na Bwana Mungu atafuta machozi katika nyuso zote; na aibu ya watu wake ataiondoa katika ulimwengu wote; maana Bwana amenena hayo. Katika siku hiyo watasema, “Tazama, huyu ndiye Mungu wetu, Ndiye tuliyemngoja atusaidie; Huyu ndiye Bwana tuliyemngoja, Na tushangilie na kuufurahia wokovu wake.” Kwa maana mkono wa Bwana utatulia katika mlima huu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 105: 2-7

  1. Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi,
    Zitafakarini ajabu zake zote.
    Jisifuni kwa jina lake takatifu,
    Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana. (K)
    (K) Bwana analikumbuka agano lake milele.
  2. Mtakeni Bwana na nguvu zake,
    Utafuteni uso wake sikuzote.
    Zikumbukeni ajabu zake alizozifanya,
    Miujiza yake na hukumu za kinywa chake. (K)
  3. Enyi wazao wa Ibrahimu, mtumishi wake,
    Enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
    Yeye, Bwana, ndiye Mungu wetu;
    Duniani mwote mna hukumu zake. (K)

SOMO 2: Flp. 4:12-14, 19-20
Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa. Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu. Lakini mlifanya vema, mliposhiriki nami katika dhiki yangu. Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachohitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu. Sasa atukuzwe Mungu, Baba yetu, milele na milele. Amina.

SHANGILIO: Yn. 14:6
Aleluya, aleluya,
Mimi ndini Njia, na Kweli, na Uzima, asema Bwana;
Mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Aleluya.

INJILI: Mt. 22:1-14
Yesu alijibu, akawaambia tena kwa mithali, akisema “Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyemfanyia mwanawe arusi. Akawatuma watumwa wake wawaite walioalikwa kuja arusini; nao wakakataa kuja. Akatuma tena watumwa wengine, akisema, ‘Waambieni wale walioalikwa, Tazameni, nimeandaa karamu yangu; ng’ombe zangu na vinono vimekwisha kuchinjwa, na vyote vimekuwa tayari, njoni arusini.’ Lakini hawakujali, wakaenda zao, mmoja shambani kwake, mmoja kwenye biashara yake; nao waliosalia wakawakamata watumwa wake, wakawatenda jeuri, na kuwaua. Basi yule mfalme akaghadhibika; akapeleka majeshi yake, akawaangamiza wauaji wale, akauteketeza mji wao. Kisha akawaambia watumwa wake, ‘Arusi i tayari, lakini wale walioalikwa hawakustahili. Basi enendeni hata njia panda za barabara, na wote mwaonao waiteni arusini.’ Watumwa wale wakatoka wakaenda njia kuu, wakakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema; arusi ikajaa wageni. Lakini alipoingia yule mfalme ili kuwatazama wageni wake, akaona mle mtu mmoja asiyevaa vazi la arusi. Akamwambia, ‘Rafiki, uliingiaje humu nawe huna vazi la arusi?’ Naye akatekewa. Mfalme akawaambia watumishi, Mfungeni mikono na miguu, mchukueni mkamtupe katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache.”

TAFAKARI:
KUMVAA KRISTO KATIKA MAISHA YETU: Licha ya mambo yote yatokeayo, Mungu daima anao mpango mwema kwetu na kwa ajili ya ulimwengu. Mungu anajua ataufanya nini huu ulimwengu. Lengo lake ni kutupeleka sote katika Ufalme wake ambapo sote tutakuwa kitu kimoja; Ufalme wa amani, furaha, na umoja. Mlima Sioni aliouona nabii Isaya, unawakilisha ulimwengu huo ujao. Unawakilisha ukarimu wa Mwenyezi Mungu, unawakilisha Ufalme usiokuwa na njaa, wala machozi, wala mauti. Humo, Mwenyezi Mungu anayafuta machozi yetu kama mama ayafutavyo machozi kwenye uso wa mtoto wake. Yesu anapoufananisha Ufalme wa Mungu na sherehe ya harusi, anamwonyesha Mungu akiwa kazini, akitaka kutupeleka sote katika Ufalme wake ambapo hakuna atakayejisikia ameachwa nje. Mara kwa mara, Injili kama ya leo, huwa ngumu sana kuitangaza hadi mwisho. Hii ni kwa sababu, kunao wanaotolewa katika sherehe na wanatupwa katika giza la nje kutakakokuwepo kilio na kusaga meno. Licha ya hii Habari Njema, tunafahamishwa ukweli jinsi hasira ya Mungu inavyokuwa.
Katika somo la kwanza nabii Isaya anatuambia jambo lile lile la harusi. Katika mlima huu, Bwana wa majeshi atawaandalia watu wote, karamu ya vitu vinono, karamu ya divai iliyokaa katika urojorojo wake. Hapa tunaiona furaha ya Mungu iliyo ya pekee kabisa. Tatizo ni kwamba sio wote wanaopokea mwaliko wa kuja harusini. Injili inatuambia kwamba mfalme anaendelea kuwatuma watu waende na kuwaalika watu karamuni, lakini hakuna anayekuja. Kisha anawatuma watumishi wake wawaalike tena watu katika karamu, hakuna anayekuja. Kila mtu yuko katika shughuli zake: mwingine analima shamba lake, na wengine wanafanya mambo yao na hawaoni sababu ya kuja kufurahi pamoja na Mungu. Kisha Mungu anawatuma watumishi wake tena. Mungu anamwalika kila mmoja, wema na wabaya. Watu wengi wanakuja na kuujaza ukumbi. Bali mfalme anapokuja na kuingia, anamkuta mgeni mmoja ambaye hakuwa na vazi la harusi. Huyu anatupwa nje gizani, kuliko na kilio na kusaga meno. Jambo hili linaingia katika mazingira yetu ya Kikristo. Vazi lile la harusi ni Kristo, kumvaa Kristo. Paulo anazungumzia hilo katika waraka wake kwamba tunapaswa kumvaa Kristo katika maisha yetu. Paulo leo katika waraka wake kwa Wafilipi, anaeleza jinsi gani maisha yanavyokuwa tunapomvaa Kristo. Anasema tunapokuwa na njaa au tukiwa tumeshiba, hilo sio kitu, kwa sababu tumemvaa Kristo, na tupo kwa sababu tupo naye. Sisi sote leo tunaalikwa kulisikiliza Neno na kumvaa Kristo katika maisha yetu. Tunapaswa kutiwa moyo na Mt. Paulo. Tunapofanya hayo katika maisha yetu, tunapomvaa Kristo, na kuwa na uhusiano mwema naye, tutajua kwa hakika yeye ni Mchungaji Mwema ambaye anatuongoza katika maisha yaliyojaa vitu vingi vilivyo vinono.

SALA: Ee Mungu, uliye na mpango wa kuubadili ulimwengu wetu uwe taifa moja, utujalie nasi tushirikiane nawe katika mpango huo, tukiwa na matumaini kwamba wewe utakuwa nguvu yetu. Amina.