OKTOBA 7, 2023; JUMAMOSI: JUMA LA 26 LA MWAKA

Bikira Maria Mt. wa Rosari
Kumbukumbu
Nyeupe
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: Kut. 23:20-23
Bwana asema hivi: Tazama, mimi namtuma malaika aende mbele yako, ili akulinde njiani na kukupeleka mpaka mahali pale nilipokutengenezea. Jitunzeni mbele yake, mwisikize sauti yake; wala msimtie kisirani; maana, hatawasamehe makosa yenu; kwa kuwa jina langu limo ndani yake. Lakini ukiisikiza sauti yake kweli, na kuyatenda yote ninenayo mimi; ndipo mimi nitakuwa ni adui wa adui zako, na mtesi wa hao wakutesao. Kwa kuwa malaika wangu atatangulia mbele yako, na kukufikisha kwenye Mwamori na Mhiti, na Mperizi na Mkanaani, na Mhivi, na Myebusi; nami nitawakatilia mbali.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 91: 1-6, 10-11

  1. Aketiye mahali pa siri pake Aliye juu
    Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi.
    Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu,
    Mungu wangu nitakayemtumainia.
    (K) Amekuagizia malaika zake wakulinde katika njia zako zote.
  2. Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji,
    Na katika tauni iharibuyo.
    Kwa manyoya yake atakufunika,
    Chini ya mbawa zake utapata kimbilio. (K)
  3. Hutaogopa hofu ya usiku,
    Wala mshale urukao mchana,
    Wala tauni ipitayo gizani.
    Wala uele uharibuo adhuhuri, (K)
  4. Mabaya hayatakupata wewe,
    Wala tauni haitaikaribia hema yako.
    Kwa kuwa atakuagizia malaika zake
    Wakulinde katika njia zako zote. (K)

TAFAKARI:
NENO LINAHIMIZA NA KUTIA MATUMAINI: (Bar 4;5-12, 27-29). Baruku baada ya kuonyesha hofu ya taifa lililogawanyika kati ya wapagani, sasa anawatangazia matumaini mapya. Anawaambia kwamba japo walifikia kusambaratika baada ya kumchukiza Mungu kwa uasi wao, haikuwa kwa lengo la kuwaangamiza. Walimsahau Mungu aliyewalisha na kuwatunza. Hata kama Mungu aliwakweza na kuwapa hadhi ya taifa taule, bado walimuasi. Hivyo akawaacha katika majonzi yao kwa muda. Yeye aliyewaelekeza katika hali hiyo atawaondoa. Hili ni himizo kwamba dhambi sio tu kukiuka taratibu zilizowekwa, bali ni kuvunja uhusiano wa kiroho na Mungu. Hata hivyo, Mungu hachoki kutuita katika ufahamu wa hali yetu na katika toba. Mwaliko kwa toba unatolewa kwa hiari ya kila mmoja. Kristo anawatahadharisha mitume wake kwamba huenda kukawa na kutopokelewa wanapoingia miji mingine. Sio kila mmoja aliye tayari kupokea Neno la toba na Ufalme wa Mungu. Wanaokataa wanaonywa kwa maneno na ishara kali. Neno la Mungu linashauri. Pia linaangazia maisha ya mwanadamu na kuyakemea maovu. Neno linapendekeza mwendelezo unaofaa. Kila siku tunapolisikia Neno likielekeza, tujaliwe kulisikia.

SALA: Tujaliwe kulisikia neno linalotuasa, lakini pia tuwe na wepesi wa kubadilika linapotushauri, na kutuwezesha kudumisha matumaini ya siku njema zaidi. Amina.