JANUARI 25, 2023; JUMATANO: JUMA LA 3 LA MWAKA

KUONGOKA KWA MT. PAULO, MTUME
Sikukuu
Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku

SOMO 1: Mdo. 22:3-16
Paulo aliwaambia makutano, Mimi ni mtu wa Kiyahudi, nalizaliwa Tarso, mji wa Kilikia, ila nililelewa katika mji huu, miguuni pa Gamalieli, nikafundishwa sheria ya baba zetu kwa usahihi, nikawa mtu wa jitihada kwa Mungu kama nyinyi nyote mlivyo leo hivi; Nikawaudhi watu wa Njia hii hata kuwauwa, nikawafunga, nikiwatia gerezani, wanaume na wanawake. Kama kuhani mkuu naye anishuhudiavyo, na wazee wa baraza wote pia, ambao nalipokea barua kwao kuwapelekea ndugu wale, nikaenda Dameski, ili niwalete wale waliokuwa huko hata Yerusalemu, hali wamefungwa, ili waadhibiwe. Ikawa nilipokuwa nikisafiri, nikikaribia Dameski, wakati wa adhuhuri, ghafula nuru kuu ilitoka mbinguni, ikanimulikia pande zote. Nikaanguka chini, nikasikia sauti ikiniambia, Sauli, Sauli, mbona unaniudhi? Nikajibu, Wewe u nani, Bwana? Akaniambia, Mimi ni Yesu Mnazareti, ambaye wewe unaniudhi. Na wale waliokuwa pamoja nami waliiona ile nuru, lakini hawakuisikia ile sauti ya yule aliyesema nami. Nikasema, Nifanye nini, Bwana? Bwana akaniambia, Simama, uingie Dameski, na huko utaambiwa habari za mambo yote yaliyoamriwa uyafanye. Na nilipokuwa sioni kwa sababu ya fahari ya nuru ile, nikaongozwa na mikono yao waliokuwa pamoja nami, nikaingia Dameski. Basi mtu mmoja, Anania, mtauwa kwa kuifuata sheria, aliyeshuhudiwa wema na Wayahudi wote waliokaa huko, akanijia, akasimama karibu nami, akaniambia, Ndugu yangu Sauli, uone. Nikamwinulia macho yangu saa ile ile. Akasema, Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe upate kujua mapenzi yake, na kumwona yule mwenye haki, na kuisikia sauti itokayo katika kinywa chake. Kwa maana utakuwa shahidi wake kwa watu wote, wa mambo hayo uliyoyaona na kuyasikia. Basi sasa, unakawilia nini? Simama, Ubatizwe, ukaoshe dhambi zako, ukiliitia jina lake.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 117:1-2

  1. Aleluya!
    Enyi mataifa yote, msifuni Bwana,
    Enyi watu wote, mhimidini.

(K) Enendeni ulimwenguni mwote,
mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.

  1. Maana fadhili zake kwetu sisi ni kuu,
    Na uaminifu wa Bwana ni wa milele. (K)

INJILI: Mk. 16:15-18
Yesu alionekana na wale kumi na mmoja, akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihuburi Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.

TAFAKARI:
Mtu mmoja anaweza kuubadili ulimwengu: Katika historia ya Kanisa hakuna uongofu uliokuwa na matokeo makubwa, kama uongofu wa Paulo. Alilidhulumu sana Kanisa kabla ya kuongoka kwake. Je, ingekuwaje kama hilo lisingalitokea? Paulo angebaki kuwa Myahudi mwaminifu katika mapokeo ya Wayahudi. Hangeandika barua kwenye Biblia. Hangesafiri kwenda kufanya kazi ya umisionari. Ila Yesu alimgeuza Sauli. Aliangushwa chini na kuisikia sauti ya Yesu: Kwa nini unaniudhi?” Alimwudhi Yesu na Kanisa lake. Kulidhulumu Kanisa ni kumdhulumu Kristo aliye kichwa na Kanisa ni mwili. Uongofu wa Sauli unatukumbusha kwamba, Yesu anapokuja kwetu, huja na malaika zake, watakatifu, makuhani, na hata maaskofu. Anatujia akiwa na Bikira Maria, anatujia akiwa na Sakramenti zake, na mafundisho yake. Yesu anakuja na Kanisa kwa sababu Yeye na Kanisa ni wamoja. Nasi, tunapomwendea Yesu hatuendi peke yetu, tunamwendea kama wanakanisa wanaofanya mwili wa fumbo ambao tumebatizwa katika huo. Kumpenda Yesu ni kulipenda Kanisa na kulipenda Kanisa ni kumpenda Yesu.

SALA: Ee Bwana, tujalie ili kuongoka kwa Paulo, kutusaidie tunamposikia Bwana akisema nasi kama alivyosema nawe. Utujalie tuitikie kwa imani kubwa kila Bwana atualikapo.