JANUARI 23, 2023; JUMATATU: JUMA LA 3 LA MWAKA

Mt. Visenti, Shemasi na Shahidi
Nyeupe
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Ebr. 9:15, 24-28
Kristo ni mjumbe wa agano jipya, ili, mauti ikiisha kufanyika kwa kukomboa makosa yaliyokuwa chini ya agano la kwanza, hao walioitwa waipokee ahadi ya urithi wa milele. Kwa sababu Kristu hakuingia katika patakatifu palipofanyika kwa mikono, ndio mfano wa patakatifu halisi; bali aliingia mbinguni hasa, aonekane sasa usoni pa Mungu kwa ajili yetu; wala si kwamba ajitoe mara nyingi, kama vile kuhani mkuu aingiavyo katika patakatifu kila mwaka kwa damu isiyo yake; kama ni hivyo, ingalimpasa kuteswa mara nyingi tangu kuwekwa msingi wa ulimwengu; lakini sasa mara moja tu, katika utimilifu wa nyakati, amefunuliwa, azitangue dhambi kwa dhabihu ya nafsi yake. Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu; kadhalika Kristo naye, akiisha kutolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi; atatokea mara ya pili, pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa wokovu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 98:1-6

 1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
  kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
  Mkono wa kuume wake mwenyewe,
  mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.

(K) Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
kwa maana ametenda mambo ya ajabu.

 1. Bwana ameufunua wokovu wake,
  machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
  Amezikumbuka rehema zake
  na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)
 2. Miisho yote ya dunia imeuona wokovu wa Mungu wetu.
  Mshangilieni Bwana, nchi yote,
  inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)
 3. Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi,
  kwa kinubi na sauti ya zaburi:
  kwa panda na sauti ya baragumu,
  shangilieni mbele za mfalme, Bwana. (K)

INJILI: Mk. 3:22-30
Waandishi walioshuka kutoka Yerusalemu wakasema, Ana Beelzebuli, na, kwa mkuu wa pepo huwatoa pepo. Yesu akawaita akawaambia kwa mifano, Awezaje Shetani kumtoa Shetani? Na ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, ufalme huo hauwezi kusimama; na nyumba ikifitinika juu ya nafsi yake, nyumba hiyo haiwezi kusimama. Na kama Shetani ameondoka juu ya nafsi yake, akafitinika, hawezi kusimama, bali huwa na kikomo. Hawezi mtu kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu, na kuviteka vitu vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu; ndipo atakapoiteka nyumba yake. Amin, nawaambia, Dhambi zote watasamehewa wanadamu, na kufuru zao watakazokufuru zote; bali mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hana msamaha hata milele; ila atakuwa ana dhambi ya milele; kwa vile walivyosema, Ana pepo mchafu.

TAFAKARI:
TUSIKILIZE NA KUELEWA, ILI TUEPUKE UZUSHI: Uzushi ni kuukataa ukweli au kusema isiyo kweli. Dhambi isiyosamehewa imetajwa katika Injili ya leo, ni dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu. Kwa kusema Kristo alitumia mkuu wa mapepo ni uzushi, ndiko kusingizia kusema Mungu ni shetani. Waandishi wanasema Yesu ana Beelizebuli mkuu wa mapepo, anatumia mkuu wa mapepo kutoa pepo. Kuhusu dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu ni ile hali ya kutokukubali kutubu, mtu kuongea kinyume kabisa na kilicho uhalisia, kwa mfano kusema Mungu ni shetani. Somo la kwanza linakazia uzuri wa Mungu, linaonyesha jinsi Yesu alivyoharibu dhambi kwa kumwaga damu yake. Dhambi ya kumsingizia Yesu ni kubwa mno na ni muhimu tuepukane nayo kabisa, kama Wakristo. Wapo waliopo magerezani na wengine kuuwawa kwa kuzushiwa mambo ya uongo. Tuache kuwa kama waandishi wanaomsingizia Yesu ati ana Beelzebuli, mkuu wa mapepo.

SALA: Tumwombe Mungu atupe roho ya kuwa wakweli na si kupindisha ukweli.