JANUARI 22, 2023; JUMAPILI: JUMAPILI YA 3 YA MWAKA

Kijani
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Isa. 9:1-4
Bwana aliingiza nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali katika hali ya kudharauliwa, lakini zamani za mwisho ameifanya kuwa tukufu, karibu na njia ya bahari; ng’ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa. Watu wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu; Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, Nuru imewaangaza. Umeliongeza taifa, umezidisha furaha yao; Wanafurahi mbele zako, Kama furaha ya wakati wa mavuno, Kama watu wafurahivyo wagawanyapo nyara. Kwa maana umeivunja nira ya mzigo wake, na gongo la bega lake, na fimbo yake yeye aliyemwonea, kama katika siku ya Midani.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 27:1, 4, 13-14

  1. Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
    Nimwogope nani?
    Bwana ni ngome ya uzima wangu,
    Nimhofu nani?
    Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu. (K)
  2. Neno moja nimelitaka kwa Bwana,
    Nalo ndilo nitakalolitafuata,
    Nikae nyumbani mwa Bwana
    Siku zote za maisha yangu.
    Niutazame uzuri wa Bwana,
    Na kutafakari hekaluni mwake. (K)
  3. Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana
    Katika nchi ya walio hai.
    Umngoje Bwana, uwe hodari,
    Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana. (K)

SOMO 2: I Kor. 1:10-13, 17

Basi ndugu, nawasihi, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba nyote mnene mamoja; wala pasiwe kwenu faraka, bali mhitimu katika nia moja na shauri moja. Kwa maana, ndugu zangu, nimearifiwa habari zenu na wale walio wa nyumbani mwa Kloe, ya kwamba iko fitina kwenu. Basi, maana yangu ni hii, ya kwamba kila mtu wa kwenu husema, Mimi ni wa Paulo, na, Mimi ni wa Apolo, na, Mimi ni wa Kefa, na, Mimi ni wa Kristo. Je! Kristo amegawanyika? Je! Paulo alisulibiwa kwa ajili yenu? Au je! mlibatizwa kwa jina la Paulo? Maana Kristo hakunituma ili nibatize, bali niihubiri Injili; wala si kwa hekima ya maneno, msalaba wa Kristu usije ukabatilika.

SHANGILIO Mt. 4:23
Aleluya, aleluya,
Kristu alihubiri Injili ya ufalme
Na kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu.
Aleluya.

INJILI: Mt. 4:12-23

Basi Yesu aliposikia ya kwamba Yohane amefungwa, alikwenda zake mpaka Galilaya; akatoka Nazareti, akaja akakaa Kapernaumu, mji ulioko pwani, mipakani mwa Zabuloni na Naftali: ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, Njia ya bahari, ng’ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa, Watu wale waliokaa katika giza wameona mwanga mkuu, nao waliokaa katika nchi na uvuli wa mauti mwanga umewazukia. Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umakeribia. Naye alipokuwa akitembea kando ya bahari ya Galilaya, aliona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi. Akawaambia, Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu. Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Akaendelea mbele, akaona ndugu wengine wawili, Yakobo wa Zebadayo, na Yohane nduguye, ambao walikuwamo chomboni pamoja na Zebedayo baba yao, wakizitengeneza nyavu zao; akawaita. Mara wakakiacha chombo na baba yao, wakamfuata. Naye alikuwa akizunguka katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri Habari Njema ya Ufalme, na kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu.

TAFAKARI:
Mimi ni wa upande gani?: Leo Bwana Yesu anaanza utume wake ambao unatupa changamoto ys swali la Je, Mimi niko upande wa nani? Wakorintho wanatupatia picha ya tabia ya wanadamu waliojaa migawanyiko. “Mimi ni wa Paulo, mimi ni wa Apolo, mimi ni wa Kristo.” Paulo anatuzungumzia jinsi tutengenezavyo makundi kati yetu. Mojawapo ya kazi kuu ya padre ni kujaribu kuwaunganisha watu: watu wema, wenye vipaji mbalimbali, na wenye kujitoa, lakini wasiotaka kufanya kazi na wenzao. Migawanyiko inayowakumba Wakorintho wacha-Mungu, imo kati yetu pia, tufahamikao kama wafuasi wa Kristo. Kunayo migawanyiko Kanisani, katika maisha ya kitawa, parokiani, katika jumuiya, na kwenye familia zetu. Ndipo Paulo anatuuliza, “Je! Yesu amegawanyika? Je! Paulo alisulibiwa kwa ajili yenu? Mlibatizwa kwa jina la Paulo?” Migawanyiko hii imo hata kwenye nafsi zetu ndani. Migawanyiko hii hutufanya kukosa uwezo wa kuishi na kuiacha tabia fulani ili kumfuata Kristo. Tendo hili ni matokeo ya dhambi ya asili, ambalo linamtenga mtu na nafsi yake mwenyewe, linamtenga na wengine, linamtenga na ulimwengu na kumtenga na Mungu pia. Ni vyema basi nijiulize, mimi namfuata nani? Ni amri ya nani ninayoifuata? Ni muziki wa nani ninaoucheza? Tufahamu vyema kuwa, Yesu aliwaita mitume ambao walikuwa na biashara zao. Ila walipoitwa, waliacha vyombo vyao na baba yao na watu wa mshahara na kumfuata. Bwana aliyetuita kuwa wafuasi, ametuita pia tuwe jinsi tulivyo. Hivyo tunapaswa kuacha kwanza jambo au kitu fulani. Kuitwa kuwa mfuasi maana yake, tumeitwa kutoka katika vifurushi hivyo vya kuabudu sanamu ambavyo tunavifanya ndani kabisa ya mioyo yetu. Ufuasi ni wito kutoka kwa Bwana, wito ambao unatutaka tuachane na vyote vinavyotufanya tusijitoe kabisa kwa Bwana. Ni wito wa kumwabudu Mungu wa kweli na wa pekee. Kuwa mfuasi maana yake ni kumfuata Yesu, naye anakuwa wa kwanza na mengine yote huchukua nafasi ya pili.

SALA: Ee Yesu Kristo Mwanga wa mataifa, angaza mioyo yetu, na kuwaangazia wale wote wanaotutaka tufanye toba ikiwa tumeleta migawanyiko katika Kanisa lake, na tuungane na makanisa mengine kuupeleka mwanga kwa wengine.