JANUARI 18, 2023; JUMATANO: JUMA LA 2 LA MWAKA

Mt. Agnes, Bikira na Shahidi
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: Ebr 7:1-3, 15-17
Melkizedeki huyo, mfalme wa Salemu, kuhani wa Mungu aliye juu, aliyekutana na Ibrahimu alipokuwa akirudi katika kuwapiga hao wafalme, akambariki; ambaye Ibrahimu alimgawia sehemu ya kumi ya vitu vyote ; (tafsiri ya jina lake kwanza ni mfalme wa haki, tena, mfalme wa Salemu, maana yake, mfalme wa amani; hana baba, hana mama, hana wazazi, hana mwanzo wa siku zake, wala mwisho wa uhai wake, bali amefananishwa na Mwana wa Mungu) ; huyo adumu kuhani milele. Tena hayo tusemayo ni dhahiri sana zaidi, ikiwa ametokea kuhani mwingine mithili ya Melkizedeki ; asiyekuwa kuhani kwa sheria ya amri iliyo ya jinsi ya mwili, bali kwa nguvu za uzima usio na ukomo; maana ameshuhudiwa kwamba, wewe u kuhani milele kwa mfano wa Melkizedeki.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 110:1-4

 1. Neno la Bwana kwa Bwana wangu
  Uketi mkono wangu wa kuume,
  Hata niwafanyapo adui zako kuwa chini ya miguu yako.
  (K)Ndiwe kuhani hata milele kwa mfano wa Melkizedeki.
 2. Bwana atainyosha toka Sayuni fimbo ya nguvu zako.
  Uwe na enzi kati ya adui zako. (K)
 3. Watu wako wanajitoa kwa hiari,
  Siku ya uwezo wako,
  Kwa uzuri wa utakatifu,
  Tokea tumbo la asubuhi,
  Unao umande wa ujana wako. (K)
 4. Bwana ameapa, wala hataghairi,
  Ndiwe kuhani hata milele
  Kwa mfano wa Melkizedeki. (K)

INJILI: Mk 3: 1-6
Yesu aliingia katika sinagogi; na palikuwako huko mtu mwenye mkono uliopooza; wakamvizia ili kuona kama atamponya siku ya Sabato; wapate kumshitaki. Akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, Simama katikati. Akawauliza, Ni halali siku ya Sabato kutenda mema, au kutenda mabaya? Kuponya Roho au kuiua? Wakanyamaza. Akawakazia macho pande zote kwa hasira, akiona huzuni kwa ajili ya ugumu wa mioyo yao, akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Naye akaunyosha; mkono wake ukawa mzima tena. Mara wakatoka wale Mafarisayo, wakawa wakifanya shauri juu yake pamoja na Maherodi, jinsi ya kumwangamiza.

TAFAKARI:
TUWE NA FURAHA NA SHUKRANI KWA MAFANIKIO YA WENGINE: Yesu alitenda miujiza alipouona uhitaji wa watu. Aliwaonea huruma. Leo anaingia kwenye sinagogi siku ya Sabato na kukutana na mtu mwenye mkono uliopooza, anamwonea huruma, anamponya. Kuponywa kwa huyu mtu kunawafanya Mafarisayo walalamike kwa vile wanamsuta Yesu kwa kutozingatia sheria ya Sabato. Mafarisayo waliona kilochokuwa cha muhimu kwao ni sheria bali si uhai wa mtu. Sheria waliyoizingatia haikuwa kwa ajli ya uzuri wa wanadamu. Mafarisayo hawakuridhika wala kushukuru kwa vile Yesu aliokoa uhai wa mtu kwa kumponya. Walichoweza kuona ni makosa ya Yesu kutoiheshimu sheria ya Sabato. Yesu anawajibu kwa kuwaonyesha kwamba watu wanahitaji huduma kuliko sheria. Wapendwa katika Kristo, tujifunze kuwa watu wa kufurahi na kushukuru kwa mafanikio ya wengine. Mmoja wetu anapofanya jambo zuri la kumpa Mungu sifa, tusiwe kama Mafarisayo wanaotafuta tu makosa na kuwa na mtizamo hasi dhidi ya wengine. Tuufurahie uzuri, na tuwapongeze wanaofanya vizuri.

SALA: Ee Bwana Yesu tupe moyo wa huruma kwa wenzetu wanaoteseka, na tuwahudumie.