JANUARI 17, 2023; JUMANNE: JUMA LA 2 LA MWAKA

Mt. Antoni, Abate
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: Ebr 6:10-20
Mungu si dhalimu hata aisahau kazi yenu, na pendo lile mlilolidhihirisha kwa jina lake, kwa kuwa mmewahudumia watakatifu, na hata hivi sasa mngali mkiwahudumia. Nasi twataka sana kila mmoja wenu aidhihirishe bidii ile ile, kwa utimilifu wa matumaini hata mwisho; ili msiwe wavivu, bali mkawe wafuasi wa hao wazirithio ahadi kwa imani na uvumilivu. Kwa maana Mungu, alipompa Ibrahimu ahadi, kwa sababu alikuwa hana mkubwa kuliko yeye mwenyewe wa kumwapa, aliapa kwa nafsi yake, akisema, Hakika yangu kubariki nitakubariki, na kuongeza nitakuongeza. Na hivyo kwa kuvumilia akaipata ile ahadi. Maana wanadamu huapa kwa yeye aliye mkuu kuliko wao; na kwao ukomo wa mashindano yote ya maneno ni kiapo, kwa kuyathibitisha. Katika neno hilo Mungu, akitaka kuwaonesha zaidi sana wairithio ile ahadi, jinsi mashauri yake yasivyoweza kubadilika, alitia kiapo katikati; ili kwa vitu viwili visivyoweza kubadilika, ambavyo katika hivyo Mungu hawezi kusema uongo, tupate faraja iliyo imara, sisi tuliokimbilia kuyashika matumaini yale yawekwayo mbele yetu; tuliyonayo kama nanga ya roho, yenye salama, yenye nguvu, yaingiayo hata mle mlimo ndani ya pazia, alimoingia Yesu kwa ajili yetu, mtangulizi wetu, amekuwa kuhani mkuu hata milele kwa mfano wa Melkizedeki.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 111:1-2, 4-5, 9-10

 1. Aleluya.
  Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote,
  Barazani pa wanyofu wa moyo na katika mkutano.
  Matendo ya Bwana ni makuu,
  Yafikiriwa sana na wapendezwao nayo.
  (K) Bwana atalikumbuka agano lake milele.
 2. Amefanya ukumbusho wa matendo yake ya ajabu;
  Bwana ni mwenye fadhili na rehema.
  Amewapa wamchao chakula,
  Atalikumbuka agano lake milele. (K)
 3. Amewapelekea watu wake ukombozi,
  Ameamuru agano lake liwe la milele,
  Jina lake ni takatifu la kuogopwa,
  Sifa zake zakaa milele. (K)

INJILI: Mk 2: 23-28
Ikawa Yesu alipokuwa akipita mashambani siku ya Sabato, wanafunzi wake walianza kuendelea njiani wakivunja masuke. Mafarisayo wakamwambia, Tazama, mbona wanafanya lisilokuwa halali siku ya Sabato? Akawaambia, Hamkusoma popote alivyofanya Daudi, alipokuwa ana haja, na kuona njaa, yeye na wenziwe? Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, zamani za kuhani mkuu Abiathari, akaila mikate ile ya Wonesho, ambayo si halali kuliwa ila makuhani, akawapa na wenziwe? Akawaambia, Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si mwanadamu kwa ajili ya Sabato. Basi Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato pia.

TAFAKARI:
SHERIA IHUDUMIE UPENDO: Mafarisayo wanamlaumu Yesu kwani wanafunzi wake wanavunja sheria ya Sabato. Yesu anao mtazamo tofauti juu ya Sabato: mwana wa adamu ndiye Bwana wa Sabato. Sheria hii inapaswa kumkomboa mwanadamu bali si kumkandamiza, Sheria itokayo kwa Mungu, imejikita kwenye upendo kwani Mungu ni upendo. Hili ndilo wasilolielewa Mafarisayo na hivyo kuibadili sheria na nia kamili ya Mungu. Yesu anatualika leo tusiwe watumwa wa sheria bali tuitumie ili kumsaidia na kumkomboa mwanadamu. Sheria itusaidie kupenda Mungu na mwanadamu zaidi. Hata wanaotunga sheria bungeni, walete tu yale yamsaidiayo mwanadamu na wala si kumkandamiza. Sheria mashuleni, kwenye taasisi na majumbani ziwe tu ni za kumsaidia mwanadamu kuutambua upendo na kuuishia. Tukiwa na upendo, yote mema yatatuandama. Kristo ametupa mfano wa Abiathari aliyeila mikate na kuwagawia wenziwe kama kielelezo cha upendo.

SALA: Ee Bwana uwape neema wanaotunga sheria na kuzitumia ziwasaidie kufikia upendo wako.