JANUARI 15, 2023; JUMAPILI: JUMAPILI YA 2 YA MWAKA

Kijani
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: Isa. 49:3, 5-6
Bwana aliniambia; Wewe u mtumishi wangu, Israeli, ambaye katika wewe nitatukuzwa. Na sasa Bwana asema hivi, yeye aliyeniumba tangu tumboni niwe mtumishi wake, ili nimletee Yakobo tena, na Israeli wakusanyike mbele zake tena; (maana mimi nimepata heshima mbele ya macho ya Bwana, na Mungu wangu amekuwa nguvu zangu); naam, asema hivi, Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu kuziinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 40:1, 3, 6-9

 1. Nalimngoja Bwana kwa saburi,
  Akaniinamia akakisikia kilio changu.
  Akatia wimbo mpya kinywani mwangu
  Ndio sifa zake Mungu wetu.
  K: Ndipo niliposema, Tazama nimekuja,
  Kuyafanya mapenzi yako.
 2. Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo,
  Masikio yangu umeyazibua,
  Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.
  Ndipo niliposema, Tazama nimekuja. (K)
 3. Katika gombo la chuo nimeandikiwa,
  Kuyafanya mapenzi yako,
  Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu;
  Naam, sheria yako imo moyoni mwangu. (K)
 4. Nimehubiri habari za haki
  Katika kusanyiko kubwa,
  Sikuizuia midomo yangu;
  Ee Bwana, unajua. (K)

SOMO 2: 1 Kor. 1:1-3

Paulo, aliyeitwa kuwa mtume wa Yesu Kristo kwa mapenzi ya Mungu, na Sosthene ndugu yetu, kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, wale waliotakaswa katika Kristo Yesu, walioitwa wawe watakatifu, pamoja na wote wanaoliitia jina la Bwana wetu Yesu Kristo kila mahali, Bwana wao na wetu. Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo.

SHANGILIO: Yn. 12:13b
Aleluya, aleluya,
Walisema, ndiye mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana,
Aleluya.

INJILI: Yn. 1:29-34

Siku ya pili Yohane Mbatizaji alimwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwanakondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu! Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Yuaja mtu nyuma yangu; ambaye amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu. Wala mimi sikumjua; lakini kusudi adhihirishwe kwa Israeli ndiyo maana mimi nalikuja nikibatiza kwa maji. Tena Yohane akashuhudia akisema, Nimemwona Roho akishuka kama hua kutoka mbinguni; naye akakaa juu yake. Wala mimi sikumjua; lakini yeye aliyenipeleka kubatiza kwa maji, huyo aliniambia, Yeye ambaye utamwona Roho akishuka na kukaa juu yake, huyo ndiye abatizaye kwa Roho Mtakatifu. Nami nimeona, tena nimeshuhudia ya kuwa huyu ni Mwana wa Mungu.

TAFAKARI:
Majina ya Yesu: Majina ni muhimu sana kwa wanadamu. Na baadhi ya majina wanayopewa watu yanabeba maana. Mara nyingi majina ya utani ambayo wanapatiwa watu yanaeleza tabia fulani ya mtu. Tukitazama katika familia zetu, katika jamii zetu, na hata mashuleni tutaona kwamba majina tunayowapatia watu au yale wanayotupatia yanabeba wasifu wa mtu huyo. Wasifu huo unaweza ukawa ni mzuri au mbaya. Majina hayaishii kwetu bali hata kwa Yesu, yapo. (i) Mtumishi: Yesu Kristo ni mtumishi wa Mungu kama anavyoelezwa katika chuo cha nabii Isaya. Jina hili linaonyesha jinsi Yesu alivyowatumikia watu. Tunapokuwa katika shida, wapo watakao kutusaidia hima, wapo wanaotucheka, wayafurahiayo mateso yetu au hata watakao kututangaza tuaibike. Yesu Mtumishi, yuaja kutusaidia. Ndipo akatujalia Ukombozi Ndipo pia akaitwa (ii) Yesu Mkombozi. Je kwa haya yote mawili, sisi huukubali utumishi wa Yesu ndani mwetu? Je, sisi huukubali Ukombozi wa Yesu maishani mwetu? (iii) Mwanakondoo: Yesu Kristo ni mwanakondoo wa Mungu. Yohane Mbatizaji alisema; “Tazama Mwanakondoo wa Mungu.” Mwanakondoo alikwenda machinjoni mkimya, lakini akiwa na nguvu ya kuwakomboa wengi. Na hili ni jambo ambalo analifanya hata leo. Yesu alipokufa alituachia jina lake. Walio wafuasi wake huwasamehe wenzao, na wengine kuyatoa maisha yao kwa ajili ya wale wanaoteseka kwa umasikini, njaa na madhulumu. Mfano huu unadhihirishwa na wanandoa wawili waliokwenda katika kituo cha kulelea watoto yatima. Mkurugenzi alipoisikia nia yao alitamani awape watoto wawili anaodhani kwamba ni wazuri. Bali mama akamwambia, “Tafadhali usitupe wale wazuri, bali wale ambao hakuna mtu mwingine anayeweza kuwachukua.” (iv) Bwana: Yesu Kristo ni Bwana. Wamebarikiwa wote ambao kwa neema na amani wanaliitia jina la Bwana. Ndiye Bwana wa maisha yetu na hivyo, kamwe tusijitenge naye. Ndiye atukusanyaye tuwe kundi moja, Kanisa. Tusiyakubali yoyote yatuondoe Kanisani aliko Bwana Yesu Kristo.

SALA: Yesu Kristo Mtumishi wa Mungu, Ewe uliye Mkombozi, Mwanakondoo na Bwana, tuunganishe sote Wakristo, kwa maongozi yako.