JANUARI 14, 2023; JUMAMOSI: JUMA LA 1 LA MWAKA

Mt. Sava wa Serbia, Askofu
Kijani
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Ebr 4:12-16
Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu. Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hatuna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 19: 7-9, 14

 1. Sheria ya Bwana ni kamilifu, huiburudisha nafsi:
  Ushuhuda wa Bwana ni amini, humtia njinga hekima.
  (K)Wewe, Ee Bwana, unayo maneno ya uzima wa milele.
 2. Maagizo ya Bwana ni ya adili, huufurahisha moyo.
  Amri ya Bwana ni safi, huyatia macho nuru. (K)
 3. Kicho cha Bwana ni kitakatifu, kinadumu milele.
  Hukumu za Bwana ni kweli, zina haki kabisa. (K)
 4. Maneno ya kinywa changu,
  Na mawazo ya moyo wangu yapate kibali mbele zako,
  Ee Bwana, mwamba wangu na Mwokozi wangu. (K)

INJILI: Mk 2: 13-17
Yesu alitoka, akaenda kando ya bahari, mkutano wote ukamwendea, akawafundisha. Hata alipokuwa akipita, akamwona Lawi wa Alfayo, ameketi forodhani, akamwambia, Nifuate. Akaondoka akamfuata. Hata alipokuwa ameketi chakulani nyumbani mwake, watoza ushuru wengi na wenye dhambi waliketi pamoja na Yesu na wanafunzi wake; kwa maana walikuwa wengi wakimfuata. Na waandishi na Mafarisayo walipomwona anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi, waliwaambia wanafunzi wake, Mbona anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi? Yesu aliposikia aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi; sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.

TAFAKARI:
NENO LA MUNGU HULETA UHAI: Kristo anaelewa maumivu na mahangaiko yetu kwa kuwa yeye amekuwa kama sisi katika kila hali ila hakuwa na dhmbi. Anaufahamu udhaifu wetu, na kwa kuufahamu hivyo ametuwekea utaratibu wa kurudisha neema tunazopoteza kwa dhambi. Tunaporudisha neema, tumerudisha uzima, tumerudisha uhai. Somo la kwanza lemetuambia kuwa Neno la Mungu huleta uhai, linagusa mioyo yetu na kutubadilisha, linapokuja mioyoni mwetu. Tukilipokea kwa upendo, hilo Neno huleta usitawi na mabadiliko mazuri kwetu. Neno hilo ni Yesu mwenyewe, ambaye katika injili ya leo anapita na kumwona Lawi ameketi ofisini kwake na kumwambia “Nifuate”. Lawi anaondoka na kumfuata, akiwa ameguswa na Neno la Yesu. Ndipo anabadilika na kuachana na mambo aliyoyazoea. Anaanza maisha mapya ya kumfuata Yesu. Sisi pia tunapokutana na neno la Mungu, tukubali nguvu ya upendo wa Kimungu itubadilishe tuachane na yasiyompendeza Mungu kama vile ulevi, uzinzi, uasherati, rushwa n.k. Neno la Mungu lina uwezo wa kutubadilisha tukawa wapya na tukamfuata Kristo kwa uaminifu, kama Mathayo.

SALA: Ee Bwana utupe neema ya kuachana na yasiyokupendeza. Tuwe wafuasi wako kweli.