JANUARI 12, 2023; ALHAMISI: JUMA LA 1 LA MWAKA

Kijani
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Ebr 3:7-14
Roho Mtakatifu asema: Leo kama mtaisikia sauti yake, msifanye migumu mioyo yenu, kama wakati wa kukasirisha, siku ya kujaribiwa katika jangwa, hapo baba zenu waliponijaribu, wakanipima wakaona matendo yangu miaka arobaini. Kwa hiyo nalichukizwa na kizazi hiki, nikasema, Siku zote ni watu waliopotoka mioyo hawa; hawakuzijua njia zangu; kama nilivyoapa kwa hasira yangu, hawataingia rahani mwangu. Angalieni, ndugu zangu, usiwe katika mmoja wenu moyo mbovu wa kutokuamini, kwa kujitenga na Mungu aliye hai. Lakini mwonyane kila siku, maadamu iitwapo leo; ili mmoja wenu asifanywe mgumu kwa udanganyifu wa dhambi. Kwa maana tumekuwa washirika wa Kristo, kama tukishikamana na mwanzo wa uthabiti wetu kwa nguvu mpaka mwisho.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 95: 6-11

  1. Njoni, tuabudu, tusujudu,
    Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.
    Kwa maana ndiye Mungu wetu,
    Na sisi tu watu wa malisho yake,
    Na kondoo za mkono wake.
    (K) Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
    Msifanye migumu mioyo yenu.
  2. Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
    Msifanye migumu mioyo yenu,
    Kama vile huko Meriba, kama siku ya Masa jangwani.
    Hapo waliponijaribu baba zenu,
    Wakanipima wakayaona matendo yangu. (K)
  3. Miaka arobaini nalihuzunika na kizazi kile,
    Nikasema, Hao ni watu waliopotoka mioyo,
    Hawakuzijua njia zangu.
    Nikaapa kwa hasira yangu
    Wasiingie rahani mwangu. (K)

INJILI: Mk 1: 40-45
Siku ile mtu mwenye ukoma alikuja kwa Yesu, akamsihi na kumpigia magoti, na kumwambia, Ukitaka, waweza kunitakasa. Naye akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka, takasika. Na mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika. Akamkataza kwa nguvu, akamwondoa mara, akamwambia, Angalia, usimwambie mtu neno lolote, ila enenda zako ukajioneshe kwa kuhani, ukatoe alivyoamuru Musa kwa kutakasika kwako, iwe ushuhuda kwao. Lakini akatoka, akaanza kuhubiri maneno mengi, na kulitangaza lile neno, hata Yesu asiweze tena kuingia mjini kwa wazi; bali alikuwako nje mahali pasipokuwa na watu, wakamwendea kutoka kila mahali.

TAFAKARI:
KUKIRI DHAMBI NA KUTUBU KUNATUFANYA WAPYA: Somo la kwanza linatufundisha kutoifanya migumu mioyo yetu. Moyo mwepesi husamehe, hukubali kuonywa, kusahihishwa, na hupokea uponyaji. Yule mwenye ukoma kwenye Injili alikuwa na moyo mwepesi wa kukubali kutakasika. Alimwambia Yesu ukitaka waweza kunitakasa Yesu akasema nataka, takasika. Moyo usio mgumu ndio unaokubali udhaifu na kuomba kuponywa, ndio unaokiri dhambi na kutubu. Kuna watu wenye mioyo migumu hata hawawezi kumwomba Yesu ili wapate uponyaji kwa njia ya Sakrameni ya kitubio ambayo inatoa uponyaji. Tunawakumbusha watu kama hao kuwa Neno la Mungu linawaambia “Ingekuwa heri leo msikie sauti yake msifanye migumu mioyo yenu” (Zaburi 95: 1-11). Mzaburi anatuambia tuilegeze mioyo yetu ili tuponywe. Tusibakie na ugumu, bali tutoe ushirikiano kwa mpango wa Mungu kutimizwa na kuendelezwa katika maisha yetu. Tusikie sauti ya Yesu inayotuita kwake tufanye mioyo yetu iwe myepesi, tusiwe kama hao wa kwenye somo la kwanza waliosikia lile neno likakosa pa kustawi.

SALA: Ee Mungu ujalie watu wako moyo mwepesi wa kujua makosa yao na kuyatubu.