JANUARI 11, 2023; JUMATANO: JUMA LA 1 LA MWAKA

Kijani
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Ebr 2:14-18
Kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi, awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utuMwa Maana ni hakika, hatwai asili ya malaika, ila atwaa asili ya mzao wa Ibrahimu. Hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye suluhu kwa dhambi za watu wake. Na kwa kuwa mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wao wanaojaribiwa.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 105: 1-4, 6-9

  1. Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake,
    Wajulisheni watu matendo yake.
    Mwimbieni kwa zaburi,
    Zitafakarini ajabu zake zote.
    (K) Bwana analikumbuka agano lake milele.
  2. Jisifuni kwa jina lake takatifu,
    Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana.
    Mtakeni Bwana na nguvu zake,
    Utafuteni uso wake siku zote. (K)
  3. Enyi wazao wa Ibrahimu, mtumishi wake;
    Enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
    Yeye Bwana, ndiye Mungu wetu;
    Duniani mwote mna hukumu zake. (K)
  4. Analikumbuka agano lake milele,
    Neno lile aliloviamuru vizazi elfu.
    Agano alilofanya na Ibrahimu,
    Na uapo wake kwa Isaka. (K)

INJILI: Mk 1: 29-39
Siku ile, Yesu alipotoka katika sinagogi, walifika nyumbani kwa Simoni na Andrea, pamoja na Yakobo na Yohane. Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa kitandani, hawezi homa; na mara wakamwambia habari zake. Akamkaribia, akamwinua kwa kumshika mkono, homa ikamwacha, akawatumikia. Hata kulipokuwa jioni, na jua limekwisha kuchwa, walikuwa wakimletea wote waliokuwa hawawezi, na wenye pepo. Na mji wote ulikuwa umekusanyika mlangoni. Akaponya wengi waliokuwa na maradhi mbalimbali, akatoa pepo wengi, wala hakuwaacha pepo kunena, kwa sababu walimjua. Hata alfajiri na mapema sana akaondoka, akatoka akaenda zake mahali pasipokuwa na watu, akaomba huko. Simoni na wenziwe wakamfuata; nao walipomwona wakamwambia, Watu wote wanakutafuta. Akawaambia, Twendeni mahali pengine, mpaka vijiji vilivyo karibu, nipate kuhubiri huko nako; maana kwa hiyo nalitokea. Akaenda akihubiri katika masinagogi yao, katika nchi yote ya Galilaya, na kutoa pepo.

TAFAKARI:
SALA NA KAZI: Marko anamwonyesha Yesu akijishughulisha na kazi ya utume. Yesu anamponya mama mkwe wa Simon aliyekuwa kitandani kwa sababu ya homa. Yesu anaendelea kuponya, kufukuza pepo na kuhubiri. Hata usiku ulipofika alikuwa bado ana kazi nyingi zilizokuwa zikimsubiri kesho yake. Ila mara kwa mara, huku akirauka mapema, anaukwepa umati uliokuwa ukimsubiri. Anaipa nafsi yake kipaumbele. Ndipo anaenda kusali kwanza. Hapa anatufundisha umuhimu wa kusali kabla ya kuanza kazi yoyote. Siku zote anza siku kwa sala. Kabla ya kwenda kazini, tukutanishe familia zetu tusali. Mtanguso wa pili wa Vatikano unatuambia familia inayosali pamoja hukaa pamoja. Kama Yesu alitenga muda kwa sala, mbona sisi wanadamu tunaohitaji sala hata na zaidi, tusitenge nafasi ya kujielekeza na kujieleza kwake katika sala? Mbona tusitenge muda wa kumsikiliza Kristo? Pamoja na sala za pamoja ni vema kila mmoja kutenga muda binafsi wa sala.

SALA: Ee Mungu wawezeshe watu wengi kufahamu nguvu ya sala na kutengea muda wa kukutana nawe kwenye sala.