JANUARI 7, 2023; JUMAMOSI: OKTAVA YA KUZALIWA BWANA

Raymundi wa Penyafort, Padre
Nyeupe
Zaburi: Juma 1

Somo: 1 Yn 5:14-21
Wapenzi: Huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba. Mtu akimwona ndugu yake anatenda dhambi isiyo ya mauti, ataomba, na Mungu atampa uzima kwa ajili ya hao watendao dhambi isiyo ya mauti. Iko dhambi iliyo ya mauti. Sisemi ya kwamba ataomba kwa ajili ya hiyo. Kila lisilo la haki ni dhambi, na dhambi iko isiyo ya mauti. Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi; bali yeye aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala yule mwovu hamgusi. Twajua ya kuwa sisi tu wa Mungu; na dunia yote pia hukaa katika yule mwovu. Nasi twajua kwamba Mwana wa Mungu amekwisha kuja, naye ametupa akili kwamba tumjue yeye aliye wa kweli, nasi tumo ndani yake yeye aliye wa kweli, yaani, ndani ya Mwana wake Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na uzima wa milele. Watoto wadogo, jilindeni nafsi zenu na sanamu.

Wimbo wa Katikati: Zab.149:1-2, 3-4, 5- 6a and 9b

 1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
  Sifa zake katika kusanyiko la watauwa.
  Israeli na amfurahie Yeye aliyemfanya,
  Wana wa Sayuni na wamshangilie mfalme wao.
  (K) Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake.
 2. Na walisifu jina lake kwa kucheza,
  Kwa matari na kinubi wamwimbie.
  Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake,
  Huwapamba wenye upole kwa wokovu. (K)
 3. Watauwa na waushangilie utukufu,
  Waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao.
  Sifa kuu za Mungu na ziwe vinywani mwao,
  Hiyo ndiyo heshima ya watauwa wake wote. (K)

INJILI: Yn. 2:1-11
Na siku ya tatu palikuwa na arusi huko Kana, mji wa Galilaya; naye mama yake Yesu alikuwapo. Yesu naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake. Hata divai ilipowatindikia, mamaye Yesu akamwambia, Hawana divai. Yesu akamwambia, Mama, tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia. Mamaye akawaambia watumishi, Lolote atakalowaambia, fanyeni. Basi kulikuwa huko mabalasi sita ya mawe, nayo yamewekwa huko kwa desturi ya Wayahudi ya kutawadha, kila moja lapata kadiri ya nzio mbili tatu. Yesu akawaambia, Jalizeni mabalasi maji. Nao wakayajaliza hata juu. Akawaambia, Sasa tekeni, mkampelekee mkuu wa meza. Wakapeleka. Naye mkuu wa meza alipoyaonja yale maji yaliyopata kuwa divai (wala asijue iliko, lakini watumishi walijua, wale walioyateka yale maji), yule mkuu wa meza alimwita bwana arusi, akamwambia, Kila mtu kwanza huandaa divai iliyo njema; hata watu wakiisha kunywa sana ndipo huleta iliyo dhaifu; wewe umeiweka divai iliyo njema hata sasa. Mwanzo huo wa ishara Yesu aliufanya huko Kana ya Galilaya, akaudhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini. Baada ya hayo akashuka mpaka Kapernaumu, yeye na mama yake na ndugu zake na wanafunzi wake; wakaa huko siku si nyingi.

TAFAKARI
TUISHI IMANI YETU KWA UPENDO NA FURAHA: Divai iliyo nzuri, huifurahisha roho, na ni ishara ya kushirikisha upendo kwa furaha. Yesu anapenda mabadiliko yawepo kwenye dini kandamizi ya Kiyahudi, watu waishi sheria ya upendo. Tukiwaona Wakristo wenye huzuni, mapadre na watawa wenye nyuso zilizokunjamana, tunaweza kubashiri kuwa hawa ni watu wenye unafiki, wayaishiyo matendo ya nje na kufuata dini kama walivyosisitiza mafarisayo na waandishi. Huku ni kuiishia Injili iliyo na makatazo mengi, sheria na vitisho vya adhabu. Je, divai (chochote kile) inayowagawanya Wakristo, ni divai inayotoka kwa Kristo kweli? Machungu hayawezi kutika kwa watu wema. Divai anayotupa Kristo ni nzuri na ndiyo inayomfanya hata mkuu wa karamu akasema “kila mtu huandaa kwanza divai nzuri, na wakiisha kunywa na kutosheka huandaa divai hafifu, bali wewe umeacha divai nzuri mpaka sasa” (Yn 2: 10). Kristo anataka Moyo ufurahi. Paulo anawaandikia Wafilipi akiwaasa furahini siku zote katika Bwana, tena nasema furahini, Mioyo yenu naijae furaha (Fil. 4:4).

SALA: Ee Bwana tuwezeshe tujawe na furaha na tuwapelekee wengine Injili ya furaha.