2022 Desemba 31 Jumamosi: Oktava Ya Kuzaliwa / Sylvester I, pp

Nyeupe
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: 1 Yoh. 2:18-21

Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho. Walitoka kwetu lakini hawakuwa wa kwetu. Maana kama wangalikuwa wa kwetu, wangalikaa pamoja nasi. Lakini walitoka ili wafunuliwe kwamba si wote walio wa kwetu. Nanyi mmepakwa mafuta na yeye aliye Mtakatifu nanyi mnajua nyote. Sikuwaandikia ninyi kwa sababu hamwijui iliyo kweli, bali kwa sababu mwaijua, tena kwamba hapana uongo wo wote utokao katika hiyo kweli.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 96, 1-2, 11-13

 1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
  Mwimbieni Bwana, nchi yote.
  Mwimbieni Bwana, libarikini jina lake,
  Tangazeni wokovu wake siku kwa siku.

(K) Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie.

 1. Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie,
  Bahari na ivume na vyote viijazavyo,
  Mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo,
  Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha;
  Mbele za Bwana, kwa maana anakuja,
  Kwa maana anakuja aihukumu nchi. (K)
 2. Atauhukumu ulimwengu kwa haki,
  Na mataifa kwa uaminifu wake. (K)

INJILI: Yn. 1:1-18

Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza. Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana. Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote wapate kuamini kwa yeye. Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile nuru. Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu. Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua. Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu. Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli. Yohana alimshuhudia, akapaza sauti yake akasema, “Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Ajaye nyuma yangu amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu. Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema. Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo. Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua.”

TAFAKATRI
YU KATI YETU AKITUANGAZA: Tunapohitimisha mwaka wa 2022 Neno la Mungu linatukumbusha tunaijua iliyo kweli na iko kati yetu. Tumepakwa mafuta na yeye aliye Mtakatifu, ndiye Neno ambaye ni Mungu aliyekuja kukaa kwetu. Kwake twapata uzima. Ambao ni nuru ya watu, nayo nuru hiyo yaangaza gizani. Tunaangazwa na neno la Mungu kuwa tunazo nyenzo zote muhimu tunazohitaji maishani mwetu kuiishi imani. Kwamba tunaye Mungu kwa hivyo hatuna sababu ya kukosa udumifu katika yeye na kuanza kumtafuta asikopatikana. Yeye ni Nuru iangazayo penye giza la dhambi. Mzee mmoja alikuwa msahaulifu kwa sababu ya kuugua na kuzeeka. Siku moja akafunga nyumba yake akaweka ufunguo kwenye mfuko wa koti lake akaenda kwenye mazoezi. Aliporudi alizunguka na kutafuta funguo za nyumba yake, huku zikiwa kwenye koti alilokuwa amevalia. Mjukuu wake aliporudi kutoka shule alipomweleza, mjukuu alimwambia avue koti lake amsaidie kutafuta. Alipokuwa akivua funguo zile zilidondoka na wakazipata. Tuutambue uwepo wa Mungu na nuru yake inayotuangaza wakati wote.

SALA: Ee Bwana niwezeshe kukutambua ulivyo ndani mwangu na ninaposoma Neno lako. Amina.