Mt. Yohane, Mtume Na Mwinjili
Sikukuu
Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku
SOMO 1: 1Yoh. 1:1-4
Lile lililokuwako tangu mwanzo, tulilolisikia, tuliloliona kwa macho yetu, tulilolitazama, na mikono yetu ikalipapasa, kwa habari ya Neno la uzima; (na uzima huo ulidhihirika, nasi tumeona, tena twashuhudia, na kuwahubiri ninyi ule uzima wa milele uliokuwa kwa Baba, ukadhihirika kwetu); hilo tuliloliona na kulisikia, twawahubiri na ninyi; ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi: na ushirika wetu ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo. Na haya twayaandika, ili furaha yetu itimizwe.
Wimbo Wa Katikati: Zab. 97: 1-2, 5-6, 11-12
- Bwana ametamalaki, nchi na ishangilie,
Visiwa vingi na vifurahi.
Mawingu na giza vyamzunguka,
Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chake
(K) Enyi wenye haki, mfurahieni Bwana.
- Milima iliyeyuka kama nta mbele za Bwana,
Mbele za Bwana wa dunia yote.
Mbingu zimetangaza haki yake,
Na watu wote wameuona utukufu wake. (K) - Nuru imemzukia mwenye haki,
Na furaha wanyofu wa moyo.
Enyi wenye haki, mfurahieni Bwana,
Na kulishukuru jina lake takatifu. (K)
INJILI: Yn. 20:2-8
Siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalena alikwenda mbio, akafika kwa Simoni Petro na kwa yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia, “Wamemwondoa Bwana kaburini, wala hatujui walikomweka.” Basi Petro akatoka, na yule mwanafunzi mwingine, wakashika njia kwenda kaburini. Wakaenda mbio wote wawili; na yule mwanafunzi mwingine akaenda mbio upesi kuliko Petro, akawa wa kwanza wa kufika kaburini. Akainama na kuchungulia, akaviona vitambaa vya sanda vimelala; lakini hakuingia. Basi akaja na Simoni Petro akimfuata, akaingia ndani ya kaburi; akavitazama vitambaa vilivyolala; na ile leso iliyokuwako kichwani pake; haikulala pamoja na vitambaa, bali imezongwa-zongwa mbali mahali pa peke yake. Basi ndipo alipoingia naye yule mwanafunzi mwingine aliyekuwa wa kwanza kufika kaburini, akaona na kuamini.
TAFAKARI
TUSHUHUDIE KWA UPENDO: Mtu anapojawa na upendo anasukumwa na kuangazwa kwa pendo hilo kusema na kutenda. Pasipo na mashaka, mwandishi wa Barua ya Yohane kwa watu wote, anavyosema alisukumwa na upendo tangu mwanzo kuona, kusikia na kupapasa kuipata habari ya Neno la uzima analolishuhudia. Kwa upendo huo mwanafunzi yule aliyependwa na Kristo alikimbia mbio akawa wa kwanza kufika kaburini na akathibitisha na kuamini. Hutuna shaka kuwa aliamini kuwa Kristo amefufuka na akashuhudia hayo aliyoyaona kwa upendo. Katika sikukuu hii ya Mtakatifu Yohane Mwinjili, masomo tunayoyatafakari yanaunganisha kipindi hiki cha kutafakari fumbo la kuzaliwa Kristo na fumbo la Ufufuko wa Bwana. Hili linatufundisha kuwa Kanisa linamhubiri Kristo aliyechukuwa nafsi ya kibinadamu, akateswa, akafa, akazikwa na siku ya tatu akafufuka. Chimbuko la hayo yote ni Upendo wa Mungu kwa mwanadamu aliyetenda dhambi. Nasi tunapotambua kuwa tumesamehewa, tumpende Kristo kwa moyo wote kama Maria Magdalena alivyompenda Kristo kwa moyo.
SALA: Ee Bwana neema yako iniwezeshe kukupenda na kukushuhudia kwa Moyo wangu wote. Amina.