Desemba 19,2022; Jumatatu: Juma La 4 La Majilio

Urujuani
Zaburi: Juma 3
SOMO I: Amu. 13:2-7, 24-25

Siku zile, palikuwa na mtu mmoja wa Sora, wa jamaa ya Wadani; jina lake akiitwa Manoa; na mkewe alikuwa tasa, hakuzaa watoto. Malaika wa Bwana akamtokea yule mwanamke, akamwambia, “Tazama, wewe sasa u tasa, huzai; lakini utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume. Basi sasa, jihadhari na kuomba, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi; kwani tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume; na wembe usipite juu ya kichwa chake; maana mtoto huyu atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye ataanza kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti.” Ndipo yule mwanamke akaenda akamwambia mume wake, akisema, “Mtu wa Mungu alinijia, na uso wake ulikuwa kama uso wa malaika wa Mungu, wa kutisha sana; nami sikumwuliza, ‘Umetoka wapi?’ Wala hakuniambia jina lake; lakini aliniambia, ‘Tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume; basi sasa, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi. Maana mtoto huyo atakuwa Mnadhiri wa Mungu tangu tumboni, hata siku ya kufa kwake.”’ Basi yule mwanamke akamzaa mtoto mwanamume akamwita jina lake Samsoni, mtoto huyu akakua, Bwana akambarikia. Roho ya Bwana ikaanza kumtaharakisha katika Mahanedani, katikati ya Sora na Eshtaoli.

Wimbo Wa Katikati: Zab 71: 3-6, 16-17

 1. Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu,
  Uniamuru niokolewe,
  Ndiwe genge langu na ngome yangu.
  Ee Mungu wangu, uniopoe mkononi mwa mkorofi.

(K) Kinywa changu kitajazwa sifa zako,
Na heshima yako mchana kutwa.

 1. Maana ndiwe taraja langu, Ee Bwana Mungu,
  Tumaini langu tokea ujana wangu.
  Nimekutegemea Wewe tangu kuzaliwa,
  Ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu. (K)
 2. Nitakuja na mambo ya ajabu ya Bwana Mungu,
  Nitawakumbusha watu haki yako wewe peke yako.
  Ee Mungu umenifundisha tokea ujana wangu;
  Nimekuwa nikitangaza miujiza yako hata leo. (K)

INJILI: Lk. 1: 5-25

Zamani za Herode, mfalme wa Uyahudi, palikuwa na kuhani mmoja, jina lake Zakaria, wa zamu ya Abiya, na mkewe alikuwa mmoja wapo wa uzao wa Haruni, jina lake Elisabeti. Na wote wawili walikuwa wenye haki mbele za Mungu, wakiendelea katika amri zote za Bwana na maagizo yake bila lawama. Nao walikuwa hawana mtoto, maana Elisabeti alikuwa tasa, na wote wawili ni wazee sana. Basi ikawa, alipokuwa akifanya kazi ya ukuhani katika taratibu ya zamu yake mbele za Mungu, kama ilivyokuwa desturi ya ukuhani, kura ilimwangukia kuingia katika hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba. Na makutano yote ya watu walikuwa wakisali nje saa ya kufukiza uvumba. Akatokewa na malaika wa Bwana, amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia. Zakaria alipomwona alifadhahika, hofu ikamwingia. Lakini yule malaika akamwambia, “Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yohane. Nawe utakuwa na furaha na shangwe, na watu wengi watakufurahia kuzaliwa kwake. Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana; hatakunywa divai wala kileo; naye atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye. Na wengi katika Waisraeli atawarejeza kwa Bwana Mungu wao. Naye atatangulia mbele zake katika roho ya Eliya, na nguvu zake, ili kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na kuwatilia waasi akili za wenye haki, na kumwekea Bwana tayari watu waliotengenezwa.” Zakaria akamwambia malaika, “Nitajuaje neno hilo? Maana mimi ni mzee, na mke wangu ni mkongwe wa siku nyingi.” Malaika akamjibu akamwambia, “Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu; nami nimetumwa niseme nawe, na kukupasha habari hizi njema. Na tazama! utakuwa bubu, usiweze kusema, mpaka siku ile yatakapotukia hayo, kwa sababu hukuyasadiki maneno yangu; nayo yatatimizwa kwa wakati wake.” Na wale watu walikuwa wakimngojea Zakaria, wakastaajabia kukawia kwake mle hekaluni. Alipotoka hali hawezi kusema nao, walitambua ya kuwa ameona maono ndani ya hekalu, naye aliendelea kuwaashiria akakaa bubu. Ikawa siku za huduma yake zilipokuwa zimetimia akaenda nyumbani kwake. Hata baada ya siku zile mkewe Elisabeti alichukuwa mimba akatawa miezi mitano, akisema, “Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana katika siku zile alizoniangalia ili kuniondolea aibu yangu mbele ya watu.”

TAFAKARI
MUNGU NI MWEMA: Wema wa Mungu hauna mipaka na haupimwi kwa mizani. Wema wake unatangazwa kwa tangazo la kuzaliwa kwake Samsoni na Yohana Mbatizaji na akina mama waliokuwa tasa. Wote wawili wanazaliwa na akina mama waliozeeka, waliokwishapoteza matumaini ya kuwa na mtoto kwa muda walioishi hapa duniani. Ilikuwa ni mpango wa Mungu audhihirishe wema wake kwa Malaika kumjulisha mke wa Manoa kuwa atapata mtoto Samsoni katika uzee wake. Huyo ndiye atakayewaokoa Waisraeli kutoka katika mikono ya Wafilisti. Neema ya Mungu inatangazwa pia kwa Mzee Zakaria ambaye naye mkewe ni mzee na tasa na ya kuwa atampata mtoto atakayewarejesha Waisraeli kwa Bwana Mungu wao. Nawe utakuwa na furaha na shangwe, na watu wengi watakufurahia kuzaliwa kwake. Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana; hatakunywa divai wala kileo; naye atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye. Ni vema kuupokea wema wa Mungu na kukua katika wema huo siku zote.

SALA: Ee Bwana niwezeshe kuutambua wema wako unaonishirikisha kila siku ya maisha yangu. Amina.