Desemba 11,2022;Jumapili: Jumapili Ya 3 Ya Mwaka

MWAKA A
Urujuani
Zaburi: Juma 3
SOMO I: Isa. 35:1-6,10

Nyika na mahali palipo ukiwa patafurahi; jangwa litashangilia na kuchanua maua kama waridi. Litachanua maua mengi, na kufurahi, naam, kwa shangwe na kuimba; litapewa uzuri wa Lebanoni, utukufu wa Karmeli na Sharoni; watauona utukufu wa Bwana, ukuu wa Mungu wetu. Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yafanyeni imara magoti yaliyolegea. Waambieni walio na moyo wa hofu, “Jipeni moyo msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi. Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa. Ndipo mtu aliye kilema ataruka-ruka kama kulungu, na ulimi wake aliye bubu utaimba. Na hao waliokombolewa na Bwana watarudi, watafika Sayuni wakiimba; na furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao; nao watapata kicheko na furaha, huzuni na kuugua zitakimbia.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 146: 6-10

 1. Huishika kweli milele.
  Huwafanyia hukumu walioonewa,
  Huwapa wenye njaa chakula;
  Bwana hufungua waliofungwa;

(K) Uje Bwana kutuokoa.

 1. Bwana huwafumbua macho waliopofuka;
  Bwana huwainua walioinama;
  Bwana huwapenda wenye haki;
  Bwana huwahifadhi wageni. (K)
 2. Huwategemeza yatima na mjane;
  Bali njia ya wasio haki huipotosha.
  Bwana atamiliki milele,
  Mungu wako, Ee Sayuni, kizazi hata kizazi. (K)

SOMO 2: Yak. 5: 7-10

Ndugu, vumilieni, hata kuja kwake Bwana. Tazama, mkulima hungoja mazao ya nchi yaliyo ya thamani, huvumilia kwa ajili yake hata yatakapopata mvua ya kwanza na ya mwisho. Nanyi vumilieni mthibitishe mioyo yenu, kwa maana kuja kwake Bwana kunakaribia. Ndugu, msinung’unikiane, msije mkahukumiwa. Angalieni, mwamuzi amesimama mbele ya milango. Ndugu, watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa uvumilivu.

SHANGILIO: Lk. 4:18

Aleluya, aleluya,
Roho wa Bwana yu juu yangu,
Amenituma kuwahubiri maskini habari njema;
Aleluya.

INJILI: Mt. 11: 2-11

Siku ile, Yohane aliposikia huko gerezani matendo yake Kristo, alituma wanafunzi wake, kumwuliza, “Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine?” Yesu akajibu akawaambia, “Nendeni mkamweleze Yohane mnayoyasikia na kuyaona; vipofu wanapata kuona, viwete wanakwenda, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa habari njema. Naye heri awaye yote asiyechukizwa nami.”

Na hao walipokwenda zao, Yesu alianza kuwaambia makutano habari za Yohane, “Mlitoka kwenda nyikani kutazama nini? Unyasi ukitikiswa na upepo? Lakini mlitoka kwenda kuona nini? Mtu aliyevikwa mavazi mororo? Tazama, watu wavaao mavazi mororo wamo katika nyumba za wafalme. Lakini kwa nini mlitoka? Ni kuona nabii?” Naam, nawaambia, “Na aliye mkuu zaidi ya nabii.” Huyo ndiye aliyeandikiwa haya, “Tazama, mimi namtuma mjumbe wangu mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako mbele yako.”

Amin, nawaambieni, “Hajaondokea mtu katika wazao wa wanawake aliye mkuu kuliko Yohane Mbatizaji; walakini aliye mdogo katika ufalme wa mbinguni ni mkuu kuliko yeye.”

TAFAKARI
TUIMARISHE MIGUU NA MAGOTI YALIYOLEGEA: Kumngojea Masiya halikuwa jambo rahisi. Ndipo Wayahudi wakaonekana kukosa subira na walimu wao kuchanganyikiwa. Hata Yohane Mbatizaji alipatwa na mashaka naye akawatuma watu kwenda kumuuliza Yesu, ili naye apate uhakika. Alipothibitiwa, Yohane alipata nguvu ingawa alikuwa gerezani, akajua kuwa ahadi imetimia na hakuna litakaloharibika hata akifa.
Injili imeandikwa katika mazingira ya Yohane Mbatizaji akiwa gerezani, kabla hajakatwa kichwa. Yohane alikuwa amefadhaishwa kwa kutokuwa na uhakika kama Yesu ndiye Masiya. Mashaka hayo yalichangiwa na mafundisho ya marabi kuwa Masiya hatajulikana atokako, atakuwa mkali, ataanzisha jeshi na pia vita vya ukombozi na hatimaye ufalme utakaokuwa na makao yake makuu mjini Yerusalemu. Licha ya Yohane kupatana na Yesu wangali tumboni, ufahamu huu ulitikiswa na yaliyokuwa yanaendelea, naye Yohane akataka thibitisho.
Maishani, tusipojua la kufanya tukiwemo dhikini, mafundisho ya wengi hutulegeza. Hata wale ambao huonekana shupavu na imara, hutikiswa. Tukiwa kwenye hali hiyo, tutende kama Yohane, twende kwa Yesu au tuzungumze na watu wengine watuelekeze kwa Yesu. Hapo tutapata thibitisho na kuwa imara tena. Kama aliowatuma Yohane, titazame ayatendayo Yesu maishani mwetu na katika maisha ya wengine: vipofu wa kimwili na kiroho wanapata kuona, viwete wa kimwili na kiroho wanatembea, wenye ukoma kimwili na kiroho wanatakaswa, viziwi kimwili na kiroho wanasikia, wafu kimwili na kiroho wanafufuliwa. Vivyo hivyo, walio maskini kimwili na kiroho wanahubiriwa Habari Njema. Tufanyapo hilo, tusisahau tahadhari kuwa mambo haya mema ni kwa walio na ushirikiano, si walio na kisirani na kiburi. Basi kama Yohane tuwe na maisha ya unyenyekevu na kujituliza.
Somo la kwanza linatupa taswira ya mazingira ya uhamishoni. Watu waliona giza, wakaondokewa na amani. Ujumbe wa nabii unawapa moyo, jangwa litashangilia na kuchanua maua kama waridi. Mungu anakuja kuwaokoa; kwa amani ya kimasiya, macho ya vipofu kimwili na kiroho yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi kimwili na kiroho yatazibuliwa, vilema kimwili na kiroho wataruka-ruka kama kulungu, na ndimi za walio bubu kimwili na kiroho zitaimba.
Somo la pili linatutahadharisha dhidi ya uchovu na ugumu wa kusubiri. Tunahimizwa kuvumilia hata kuja kwake Bwana. Tujifananishe na wakulima ambao hungoja mazao ya nchi yaliyo ya thamani, kwa uvumilivu mkubwa hata yatakapopata mvua ya kwanza na ya mwisho. Kuvumilia huthibitisha mioyo. Tusinung’unike, tusihukumu. Ili tuwe imara, tushikamane na Kristo.

SALA: Ee Mungu, unakaribia kutupatia Mwanao katika sherehe ya Noeli. Tusaidie azaliwe mioyoni mwetu, adumu nasi na aangalie wakati wa matatizo na mfadhaiko miguu na magoti yetu yasilegee kwa kukata tamaa. Amina.

2022 Desemba 12 Jumatatu: Juma La 3 La Majilio
Our Lady of Guadalupe F
Urujuani
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Hes. 24:2-7, 15-17

Siku zile Balaamu aliinua macho yake akawaona Israeli, wamekaa kabila kabila, roho ya Mungu ikamjia. Akatunga mithali yake akasema, “Balaamu mwana wa Beori asema, ‘Yule mtu aliyefumbwa macho asema;’ asema, ‘yeye asikiaye maneno ya Mungu, yeye aonaye maono ya Mwenyezi, akianguka kifudifudi, amefumbuliwa macho; mahema yako ni mazuri namna gani, ee Yakobo, maskani zako, ee Israeli! Mfano wa bonde zimetandwa, mfano wa bustani kando ya mto, mfano ya mishubiri aliyoipanda Bwana, mfano ya mierezi kando ya maji. Maji yatafurika katika ndoo zake, na mbegu zake zitakuwa katika maji mengi. Na mfalme wake ataadhimishwa kuliko Agagi, na ufalme wake utatukuzwa.”’ Akatunga mithali yake akasema, “Balaamu mwana wa Beori asema, ‘Yule mtu aliyefumbwa macho asema, asema, yeye asikiaye maneno ya Mungu, na kuyajua maarifa yake Aliye Juu. Yeye aonaye maono ya Mwenyezi, akianguka kifudifudi, amefumbuliwa macho, namwona, lakini si sasa; namtazama, lakini si karibu; nyota itatokea katika Yakobo; na fimbo ya enzi itainuka katika Israeli.”’

Wimbo Wa Katikati: Zab. 25:4-6, 7b-9

 1. Ee Bwana, unijulishe njia zako,
  Unifundishe mapito yako,
  Uniongoze katika kweli yako,
  Na kunifundisha.

(K) Ee Bwana unijulishe njia zako.

 1. Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako
  Maana zimekuweko tokea zamani.
  Unikumbuke kwa kadiri ya fadhili zako,
  Ee Bwana kwa ajili ya wema wako. (K)
 2. Bwana yu mwema, mwenye adili,
  Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.
  Wenye upole akawaongoza katika hukumu
  Wenye upole atawafundisha njia yake.

INJILI: Mt. 21:23-27

Siku ile Yesu alipokwisha kuingia hekaluni, wakuu wa makuhani na wazee wa watu wakamwendea alipokuwa akifundisha, wakasema, “Ni kwa amri gani unatenda mambo haya? Naye ni nani aliyekupa amri hii?” Yesu akajibu, akawaambia, “Na mimi nitawauliza neno moja; ambalo mkinijibu, nami nitawaambia ni kwa amri gani ninatenda haya. Ubatizo wa Yohana ulitoka wapi? Ulitoka mbinguni, au kwa wanadamu?” Wakahojiana wao kwa wao, wakisema, “Tukisema, Ulitoka mbinguni, atatuambia, ‘Mbona basi hamkumwamini?’ Na tukisema, ‘Ulitoka kwa wanadamu, twaogopa mkutano; maana watu wote wamwona Yohana kuwa ni nabii.”’ Wakamjibu Yesu wakasema, “Hatujui.” Naye akawaambia, “Wala mimi siwaambii ninyi ni kwa amri gani ninatenda haya.”

TAFAKARI
KUWATETEA WANYONGE: Israeli alikuwa akiishi maisha ya kinyonge jangwani bila ya kuwa na makazi ya kudumu na alionewa na makabila mbalimbali yaliyokuwa tajiri na yenye nguvu kuliko kabila la Israeli. Katika somo la kwanza tunamuona Balaam akitoa utabiri juu ya maisha mazuri ambayo Israeli ataenda kuishi. Katika unyonge wa Israeli tunaona namna ambayo Mungu alikuwa tegemeo lao maana Israeli ilikuwa taifa lake teule na wao walizidi kumkimbilia Mungu aliyewapigania. Tuungane siku zote kuwatetea wanyonge na sio kuwanyanyasa. Kwa kuwasaidia wanyonge tunapata baraka tele kutoka kwa Mungu. Yesu alipokuja duniani kama mwanadamu hakujikweza kwa namna yoyote ile bali alijinyenyekeza mbele ya Mungu na mbele ya wanadamu. Katika unyonge wake, watu walimdharau na kukataa kushirikiana naye na hivyo kukosa baraka. Je nasi maishani mwetu, ni kwa namna gani sisi hukosa kushirikiana naye?

SALA: Ee Bwana tusaidie tupate kuwatetea wanyonge. Amina.