Desemba 3,2022; Jumamosi: Juma La 1 La Majilio

Mt. Fransisko Ksaveri, Padre
Kumbukumbu
Urujuani
SOMO 1: Isa. 30:19-21, 23-26

Bwana Mungu Mtakatifu wa Israeli asema: “Watu watakaa katika Sayuni huko Yerusalemu; wewe hutalia tena; hakika yake atakuonea rehema nyingi kwa sauti ya kilio chako; asikiapo ndipo atakapokujibu. Na ingawa Bwana atawapeni chakula cha shida na maji ya msiba, lakini walimu wako hawatafichwa tena, ila macho yako yatawaona waalimu wako; na masikio yako yatasikia neno nyuma yako, likisema, ‘Njia ni hii, ifuateni; mgeukapo kwenda mkono wa kulia, na mgeukapo kwenda mkono wa kushoto.”’ Naye atatoa mvua juu ya mbegu zako, upate kuipanda nchi hii; na mkate wa mazao ya nchi, nayo itastawi na kuzaa tele; katika siku hiyo ng’ome zako watakula katika malisho mapana. Ng’ombe pia na wana-punda wailimao nchi watakula chakula kilichokolea, kilichopepetwa kwa ungo na kwa pepeo. Na juu ya kila mlima mrefu, na juu ya kila kilima kilichoinuka, itakuwapo mito na vijito vya maji, katika siku ya machinjo makuu itakapoanguka minara. Na tena nuru ya mwezi itakuwa kama nuru ya jua, na nuru ya jua itaongezeka mara saba, kama nuru ya siku saba, katika siku ile Bwana atakapofunga mapigo ya watu wake, na kuliponya pigo la jeraha yao

Wimbo Wa Katikati: Zab. 147:1-6

 1. Msifuni Bwana, maana ni vema kumwimbia Mungu wetu
  Maana kwapendeza, kusifu ni kuzuri.
  Bwana ndiye aijengaye Yerusalemu,
  Huwakusanya waliotawanyika wa Israeli.

(K) Heri wote wamngojao Bwana.

 1. Huwaponya waliopondeka moyo,
  Na kuziganga jeraha zao.
  Huihesabu idadi ya nyota,
  Huzipa zote majina. (K)
 2. Bwana wetu ni mkuu na mwingi wa nguvu.
  Akili zake hazina mpaka,
  Bwana huwategemeza wenye upole,
  Huwaangusha chini wenye jeuri. (K)

INJILI: Mt. 9:35 – 10:1, 6-8

Siku ile: Yesu alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri habari njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Na alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji. Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, “Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake.” Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Akawaambia, “Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, ‘Ufalme wa mbinguni umekaribia. Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.”’

TAFAKARI
HURUMA YA KRISTO KWA WATU: Kristo alipowaona makutano aliufahamu uhitaji wao, akawahurumia. Kuwahurumia maskini na wagonjwa ni wajibu wa kila Mkristo. Tunaalikwa kuiga Kristo ambaye anatuonyesha mfano. Alipokuwa akihubiri aliwaponya wagonjwa wa aina mbalimabali na kuwaonea huruma kutokana na uchovu waliokuwa nao. Kila mbatizwa anastahili kumwiga mwalimu wetu ambaye ni Kristo aliye mponyaji wetu. Wagonjwa wanapata faraja pale ambapo wanafarijiwa. Tuwe karibu nao tusiwaache wagonjwa wateseka katika hali ya upweke bali tuwafikie, tuwaonee huruma, tuwasikilize na tuwahudumie kwa kadri ya uwezo wetu. Kristo anasema, “Mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake.”( Mt 9:38) Maneno haya yanatukumbusha wajibu wetu kuomba ili Mungu alijalie Kanisa lake wahudumu, watakaotoa huduma kwa wahitaji wa namna mbalimbali. Wahitaji hawa ni kama vile wagonjwa wa kiroho na wa kimwili, walemavu, na walegevu wa imani. Inatupasa pia kufundisha kuhusu imani. Tukiomba kwa imani, Mungu mwenye huruma atatusaidia.

SALA: Ee Mungu mwenye huruma nakuomba unijalie niwe na huruma kwa wahitaji. Amina.