Novemba 27,2022; Jumapili: Jumapili Ya 1 Ya Majilio

MWAKA A
Urujuani
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Isa. 2:1-5

Hili ni neno aliloliona Isaya mwana wa Amozi katika habari za Yuda na Yerusalemu. Na itakuwa katika siku za mwisho, mlima wa nyumba ya Bwana utawekwa imara juu ya milima, nao utainuliwa juu ya vilima; na mataifa yote watauendea makundi makundi. Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani kwa Bwana, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake; maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la Bwana katika Yerusalemu.

Naye atafanya hukumu katika mataifa mengi, atawakemea watu wa kabila nyingi; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe. Enyi wa nyumba ya Israeli, njoni, twende katika nuru ya Bwana.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 122: 1-4, 8-9

  1. Nalifurahi waliponiambia,
    Na twende nyumbani kwa Bwana.
    Miguu yetu imesimama
    Ndani ya malango yako, Ee Yerusalemu
    (K) Nalifurahi waliponiambia, Na twende nyumbani kwa Bwana.
  2. Ee Yerusalemu uliyejengwa
    Kama mji ulioshikamana,
    Huko ndiko walikopanda kabila,
    Kabila za Bwana. (K)
  3. Kwa ajili ya ndugu zangu na rafiki zangu
    Niseme sasa, “Amani ikae nawe.”
    Kwa ajili ya nyumba ya Bwana, Mungu wetu,
    Nikutafutie mema. (K)

SOMO 2: Rum. 13:11-14

Ndugu zangu, tukiujua wakati, kwamba saa ya kuamka katika usingizi imekwisha kuwadia; kwa maana sasa wokovu wetu u karibu nasi kuliko tulipoanza kuamini. Usiku umeendelea sana, mchana umekaribia; basi na tuyavue matendo ya giza, na kuzivaa silaha za nuru. Kama ilivyohusika na mchana na tuenende kwa adabu; si kwa ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu. Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo, wala msiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake.

SHANGILIO: Zab. 85:7

Aleluya, aleluya,
Ee Bwana utuonyeshe rehema zako, Utupe na wokovu wako,
Aleluya.

INJILI: Mt. 24: 37-44

Siku ile, Yesu aliwaambia wafuasi wake kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Kwa kuwa kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina, wasitambue, hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni, mmoja atwaliwa, mmoja aachwa; wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa.

Kesheni basi, kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu. Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa. Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja.

TAFAKARI
TUSIACHE NYUMBA ZETU KUVUNJWA: Hii ndiyo njia ya kukabiliana vyema na ujio wa Yesu Kristo. Leo ni Dominika ya kwanza ya Majilio. Majilio maana yake ni ujio, kuja; kipindi ya kujiandaa kumpokea mioyoni mwetu Bwana Yesu Kristo anayekuja kuanzisha mradi wa Ukombozi wetu. Mradi huu utafikia kilele chake msalabani, pale atakapokufa kwa ajili ya kutupatanisha wanadamu na Mungu. Anaanza mradi huo kwa kujimwilisha kusudi apate damu na nyama, vitu ambavyo atavitolea msalabani kama sadaka azizi ya kumpendeza Mungu.
Desturi ya kuwa na kipindi cha Majilio ilianza katika Kanisa Katoliki la Mashariki (Dola la Kirumi). Huko lugha mama ya liturujia ni Kigiriki au Kiyunani, na makao yake makuu ni Konstantinople (siku hizi Instanbul, Uturuki). Kunakoitwa Kanisa Katoliki la Magharibi, na ambako lugha mama ya liturujia ni Kilatini, makao yake makuu ni Roma (Italia). Kanisa hili la Mashariki, walikuwa na desturi ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Bwana Yesu Kristo tarehe 6 Januari. Walijiandaa kwa adhimisho hili kwa imani, matumaini na mapendo. Waliutafakari ujio huu wa kuzaliwa Bwana pamoja na ule wa mwisho (kiyama).
Kipindi cha Majilio kimegawanyika sehemu mbili. Wiki mbili za mwanzo, tunakumbushana juu ya ujio wa pili, ujio ambao tunapaswa kuutarajia kwa tahadhari kubwa usije ukatufyatukia ghafla na kutunasa. Hapa tunakumbushwa “KUKESHA”. Injili inakazia wazo la kukesha. Inasema kuwa siku hiyo itakuja wakati watu wakiendelea na maisha yao kama kawaida. Mambo yatakuwa kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu. Kama vile siku zile kabla ya gharika. Watu watakuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku Nuhu alipoingia katika safina. Pasipo kutambua, kama gharika itakuja na kuwachukua wote. Yesu anasisitiza kuwa Mungu atachanganua ipasavyo; mwenye kustahili thawabu atabainishwakati ya wengine. Watu wawili wakiwa kondeni mwenye haki atatwaliwa na mwovu ataachwa; hata wakiwa wanawake wawili wanaofanya kazi moja kama ya kusaga; mwema atatwaliwa na mwovu ataachwa. Hatimaye Yesu anatutahadharisha kwa maneno haya, “Laiti mwenye nyumba angaliijua zamu mwivi atakayokuja, asingalikuwa mvivu wala mzembe bali angalikesha, asiiache nyumba yake kuvunjwa.” Nayo majuma mawili ya mwisho ya Majilio yanatualika kumpokea Yesu Kristo katika ujio wake wa kwanza, ujio wa neema. Ujio huu ni wa Habari Njema ya furaha, kwani mtoto anayezaliwa anatuletea neema ya Ukombozi, kama itakavyoimba kwaya ya malaika.
Somo la kwanza linafafanua kuhusu kukesha ambako ni kuangalia tusiache nyumba zetu kuvunjwa. Ni mwaliko wa watu wa ulimwengu wote kwa sababu hukumu ya Bwana itawahusu wote. Bwana Mungu anawaalika watu wote kuacha dhambi na kuwa watu wema kusudi waupate uzima wa milele. Toba na msamaha ni kwa wote. Ndipo tunapoambiwa kwamba Bwana atafanya hukumu kwa watu wa mataifa, atawakemea watu wa kabila nyingi; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe.
Somo la pili nalo linasisitiza kujiweka tayari kwa ujio wa pili wa Bwana, ujio unaozungumzia hukumu. Ndipo tunapoambiwa, tuujue wakati, kwamba saa ya kuamka katika usingizi imekwisha kuwadia; kwa maana sasa wokovu wetu U karibu nasi kuliko tulipoanza kuamini. Yatupasa tujue jinsi usiku ulivyoendelea sana na mchana ulivyokaribia. Kutokana na hayo, tuyavue matendo ya giza, na kuzivaa silaha za nuru na tuenende kwa adabu. Tusiwe walafi na walevi, wala wafisadi na waasherati, wala wagomvi na wenye wivu. Kinyume chake tumvae Kristo tukibaki kwenye mawaidha ya Maandiko Matakatifu.

SALA: Ee Bwana Yesu Kristo, tumeusikia mwaliko wako. Unatutaka tukeshe na kujiweka tayari kwa ujio wako. Tusaidie, pamoja nawe, tukeshe kwa ufanisi, tupate kupona katika hukumu yako. Amina.