Novemba 26,2022; Jumamosi: Juma La 34 La Mwaka

Mt. Yohani Berkmans, Mtawa
Zaburi: Juma 2
SOMO I: Ufu. 22:1-7

Malaika alinionyesha, mimi Yohane, mto wa maji ya uzima, wenye kung’aa kama bilauri, ukitoka katika kiti cha enzi cha Mungu, na cha Mwanakondoo, katikati ya njia kuu yake. Na upande huu na upande huu wa ule mto, ulikuwepo mti wa uzima, uzaao matunda, aina kumi na mbili, wenye kutoa matunda yake kila mwezi; na majani ya mti huo ni ya kuwaponya mataifa. Wala hapatakuwa na laana yoyote tena. Na kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwanakondoo kitakuwamo ndani yake. Na watumwa wake watamtumikia; nao watamwona uso wake, na jina lake litakuwa katika vipaji vya nyuso zao. Wala hapatakuwa na usiku tena; wala hawana haja ya taa wala ya nuru ya jua; kwa kuwa Bwana Mungu huwatia nuru, nao watatawala hata milele na milele. Kisha akaniambia, Maneno haya ni amini na kweli. Naye Bwana, Mungu wa roho za manabii, alimtuma malaika wake kuwaonyesha watumwa wake mambo ambayo hayana budi kuwako upesi. Na tazama, naja upesi; heri yeye ayashikaye maneno ya unabii wa kitabu hiki.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 95:1-7

 1. Njoni, tumwimbie Bwana,
  Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.
  Tuje mbele zake kwa shukrani,
  Tumfanyie shangwe kwa zaburi.

(K) Maranatha, Uje Bwana Yesu.

 1. Kwa kuwa Bwana ni Mungu mkuu
  Na mfalme juu ya miungu yote.
  Mkononi mwake zimo bonde za dunia.
  Hata vilele vya milima ni vyake.
  Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya,
  Na mikono yake iliumba nchi kavu. (K)
 2. Njoni, tuabudu, tusujudu,
  Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.
  Kwa maana ndiye Mungu wetu,
  Na sisi tu watu wa malisho yake,
  Na kondoo za mkono wake. (K)

INJILI: Lk. 21:34-36
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo; kwa kuwa ndivyo itakavyowajilia watu wote wakaao juu ya uso wa dunia nzima. Basi, kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika hayo yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu.”

TAFAKARI
KUNYWA MAJI YA MTO WA UZIMA: Neno kunywa au kula yanaeleweka kawaida ni kuweka kinacholiwa mdomoni ili kifikishwe tumboni. Mto mahali maji yanapotiririka, siku hizi za leo kuna mito inayosambaza maji kwa muda tu na mingine inasambaza muda wote. Tafakari yetu hapa ya kunywa kutoka katika mto wa maji ya uzima inalenga kutufahamisha Neema ya Mungu ni Maji yanayotufikia kupitia miito mbali mbali kama ilivyoainisha katika Neno la Mungu na mafundisho ya Kanisa. Kristo ametualika tukeshe kila wakati tukiomba, jiulize wewe wakati mwingine hukeshi bila kusali? Twaona wengine wanakesha kwenye kumbi za starehe, ulevi, ulafi, uasherati, wengine wameshikilia silaha na wengine kwenye lindo, wanasahau pia, “Bwana asipoulinda mji aulindaye akesha bure” (Zaburi 127: 1-2). Je! nampa Mungu nafasi katika maisha yangu na shughuli zangu wakati wote? Mungu ndiye chanzo cha mto wa neema tunakoalikwa kila mmoja aunge hapo kwenye hicho chanzo na anywe maji hayo ya uzima na kuwasambazia wengine?

SALA: Ee Bwana. neema yako iniwezeshe kushinda dhambi, nimeungana nawe muda wote.