Novemba 24,2022; Alhamisi: Juma La 34 La Mwaka

Wat. Flora na Maria, Mashahidi
Kijani
Zaburi: Juma 2
SOMO I: Ufu. 18:1-2, 21-23; 19:1-3, 9

Mimi, Yohane, naliona malaika mwingine, akishuka kutoka mbinguni, mwenye mamlaka kuu; na nchi ikaangazwa kwa utukufu wake. Akalia kwa sauti kuu, akisema, “Umeanguka, umeanguka Babeli ule mkuu; umekuwa maskani ya mashetani, na ngome ya kila roho mchafu, na ngome ya kila ndege mchafu mwenye kuchukiza.” Na malaika mmoja mwenye nguvu akainua jiwe, kama jiwe kubwa la kusagia, akalitupa katika bahari, akisema, “Kama hivi, kwa nguvu nyingi, utatupwa Babeli, mji ule mkuu, wala hautaonekana tena kabisa. Wala sauti ya wapiga vinanda, na ya wapiga zomari, na ya wapiga filimbi, na ya wapiga baragumu, haitasikiwa ndani yako tena kabisa; wala fundi awaye yote wa kazi yoyote hataonekana ndani yako tena kabisa; wala sauti ya jiwe la kusagia haitasikiwa ndani yako tena kabisa; wala nuru ya taa haitamulika ndani yako tena kabisa; wala sauti ya bwana-arusi na bibi-arusi haitasikiwa ndani yako tena kabisa; maana hao wafanya biashara wako walikuwa wakuu wa nchi, kwa kuwa mataifa yote walidanganywa kwa uchawi wako.” Baada ya hayo nikasikia sauti kama sauti ya makutano mengi, sauti kubwa mbinguni, ikisema, “Aleluya; Wokovu na utukufu na nguvu zina Bwana Mungu wetu; kwa kuwa hukumu zake ni za kweli na za haki; maana amemhukumu yule kahaba mkuu aliyeiharibu nchi kwa uasherati wake, na kuipatiliza damu ya watumwa wake mkononi mwake.” Wakasema mara ya pili, “Aleluya, na moshi wake hupaa juu hata milele na milele.” Naye akaniambia, “Andika, Heri walioalikwa karamu ya arusi ya Mwanakondoo.” Akaniambia, “Maneno haya ni maneno ya kweli ya Mungu.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 100

 1. Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote,
  Mtumikieni Bwana kwa furaha;
  Njoni mbele zake kwa kuimba.

(K) Heri walioalikwa karamu ya arusi ya Mwanakondoo.

 1. Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu;
  Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake;
  Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake. (K)
 2. Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru;
  Nyuani mwake kwa kusifu;
  Mshukuruni, lihimidini jina lake. (K)
 3. Kwa kuwa Bwana ndiye mwema;
  Rehema zake ni za milele;
  Na uaminifu wake vizazi na vizazi. (K)

INJILI: Lk. 21:20-28

Yesu aliwaambia wanafunzi wake:” Hapo mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, ndipo jueni ya kwamba uharibifu wake umekaribia. Ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani, na walio katikati yake wakimbilie nje, na walio katika mashamba wasiuingie. Kwa kuwa siku hizo ndizo za mapatilizo, ili yatimizwe yote yaliyoandikwa. Ole wao wenye mimba na wanaonyonyesha katika siku hizo! Kwa kuwa kutakuwa na shida nyingi katika nchi, na hasira juu ya taifa hili. Wataanguka kwa ukali wa upanga, nao watatekwa nyara na kuchukuliwa katika mataifa yote; na Yerusalemu utakanyagwa na Mataifa, hata majira ya Mataifa yatakapotimia. Tena, kutakuwa na ishara katika jua; na mwezi, na nyota; na katika nchi dhiki ya mataifa wakishangaa kwa uvumi wa bahari na msukosuko wake; watu wakivunjika mioyo kwa hofu, na kwa kutazama mambo yatakayoupata ulimwengu. Kwa kuwa nguvu za mbinguni zitatikisika. Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika wingu pamoja na nguvu na utukufu mwingi. Basi mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia.”

TAFAKARI
USIPOTUBU UTASAHAULIKA: Somo la kwanza linatuambia kuhusu Babeli mji maarufu ambao utatupwa na kusahaulika, kama jiwe lililotupwa baharini kama watu wake hawatatubu. Uharibifu kama huo unatangazwa juu ya Yerusalemu pia. Mwanadamu mwenye uweza wa kufikiri anajitawala na kujielekeza. Hali ya ugonjwa inapomfika mwanadamu huyu mwenye nguvu atakuwa mdhaifu na kifo kinamtenga na aliyoyazoea ulimwenguni. Yaani kifo kinamchukua ambapo ni kutengana mwili na roho. Mwili twauhifadhi lakini roho inaenda ahera. Ujumbe wa Neno la Mungu wa siku hii ya leo unamtahadharisha mwandamu asijepotea kwa kuharibikiwa bali aanze kujipanga kwa siku ya mwisho. Wakristo tumebahatika kuwekewa na Kristo Sakramenti ya Maungamo ambayo mama Kanisa anaitumia kumsafisha kila mbatizwa aliyetumbukia katika dimbwi la dhambi. Kwa kuwa mtu anaitenda dhambi akijua, tufahamu kuwa hiyo dhambi inatuzuia kuongoka. Sharti tuyafanye hayo mabadiliko la sivyo tutapotea.

SALA: Ee Bwana, unijalie neema zako niweze kushinda dhambi, roho yangu isipotee. Amina.