Novemba 18,2022; Ijumaa: Juma La 33 La Mwaka

Kutabarukiwa Mabasilika ya Wat. Petro na Paulo, Mitume
Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO I: Ufu. 10:8-11

Mimi, Yohane, nilisikia sauti ile niliyoisikia kutoka mbinguni ilinena nami tena, ikisema, “Enenda, ukakitwae kile kitabu kilichofunguliwa katika mkono wa yule malaika, aliyesimama juu ya bahari na juu ya nchi”. Nikamwendea malaika yule nikamwambia kwamba anipe kile kitabu kidogo. Akaniambia, “Kitwae, ukile, nacho kitakutia uchungu tumboni mwako, bali katika kinywa chako kitakuwa kitamu kama asali.” Nikakitwaa kile kitabu kidogo katika mkono wa malaika yule, nikakila; nacho kikawa kitamu kama asali kinywani mwangu, na nilipokwisha kukila tumbo langu likatiwa uchungu. Wakaniambia, “Imekupasa kutoa unabii tena juu ya watu na taifa na lugha na wafalme wengi.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 119:14, 24, 72, 103, 111, 131

  1. Nimeifurahia njia ya shuhuda zako,
    Kana kwamba ni mali mengi.
    Shuhuda zako nazo ndizo furaha yangu,
    Na washauri wangu.

(K) Mausia yako ni matamu sana kwangu.

  1. Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu,
    Kuliko maelfu ya dhahabu na fedha.
    Mausia yako ni matamu sana kwangu,
    Kupita asali kinywani mwangu. (K)
  2. Shuhuda zako nimezifanya urithi wa milele,
    Maana ndizo changamko la moyo wangu.
    Nalifunua kinywa changu nikatweta,
    Maana naliyatamani maagizo yako. (K)

INJILI: Lk. 19:45-48

Yesu aliingia hekaluni, akaanza kuwatoa wale waliokuwa wakifanya biashara, akiwaambia, “Imeandikwa, Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi.” Naye akawa akifundisha kila siku hekaluni. Lakini wakuu wa makuhani, na waandishi, na wakuu wa watu walikuwa wakitafuta njia ya kumwangamiza; wasione la kutenda, kwa kuwa watu wote walikuwa wakiandamana naye, wakimsikiliza.

TAFAKARI
UFALME WA MBINGUNI NI MTAMU: Maisha yetu ya Ukristo yanatuahidi maisha mazuri ya ufalme wa mbinguni, lakini ni lazima yafanyiwe kazi kwa kujituma na majitoleo. Ukristo wetu unatutaka kufanya kazi ili kutimiza unabii wetu kwa ujasiri huku tukizipinga na kukataa ushawishi wa yule mwovu. Nabii inampasa kukataa uovu katika jamii, uharibifu au uchafuzi wa matakatifu. Tunaona katika injili Yesu anavyokemea matumizi mabaya ya hekalu. Ujasiri huo wa Yesu sio tu kitu cha kutamani bali ni kitu cha kuiga na kukiishi, ili tuutafute na kuufahamu mpango wake Mungu maishani mwetu. Tukishaupata mpango wa Mungu kwetu tuufuate. Hii ni hali ambayo inajumuisha kusali, kushikamana kwa upendo, kusoma Neno la Mungu, kulitafakari na kuliishi. Mkristo fanya juhudi za kutosha, ili utakatifu upate mahali pa kustawi ndani mwetu. Tukiyatekeleza hayo, tutayaishi yale yanatarajiwa sasa.

SALA: Ee Bwana, uniwezeshe kutunza matakatifu niliyokabidhiwa kwa sakramenti ya ubatizo.