Novemba 17,2022; Alhamisi: Juma La 33 La Mwaka

Mt. Elizabeti wa Ungaria
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO I: Ufu. 5:1-10

Mimi, Yohane, niliona katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi, kitabu kilichoandikwa ndani na nyuma, kimetiwa muhuri saba. Nikaona malaika mwenye nguvu akihubiri kwa sauti kuu, “N’nani astahiliye kukifungua kitabu, na kuzivunja muhuri zake?” Wala hapakuwa na mtu mbinguni, wala juu ya nchi, wala chini ya nchi, aliyeweza kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama. Nami nikalia sana kwa kuwa hapakuonekana mtu astahiliye kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama. Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, “Usilie; tazama, Simba aliye wa kabila ya Yuda, Shina la Daudi, yeye ameshinda apate kukifungua kile kitabu, na zile muhuri zake saba.” Nikaona katikati ya kiti cha enzi na wale wenye uhai wanne, na katikati ya wale wazee, Mwana-Kondoo amesimama, alikuwa kana kwamba amechinjwa, mwenye pembe saba na macho saba, ambazo ni Roho saba za Mungu zilizotumwa katika dunia yote. Akaja, akakitwaa kile kitabu katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi. Hata alipokitwaa kile kitabu, hao wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele za Mwanakondoo, kila mmoja wao ana kinubi, na vitasa vya dhahabu vilivyojaa manukato, ambayo ni maombi ya watakatifu. Nao waimba wimbo mpya wakisema, “Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 149:1-6, 9

  1. Aleluya.
    Mwaimbieni Bwana wimbo mpya,
    Sifa zake katika kusanyiko la watauwa.
    Israeli na amfurahie Yeye aliyemfanya,
    Wana wa Sayuni na wamshangilie mfalme wao.

(L) Ulitufanya kuwa wafalme na makuhani.

  1. Na walisifu jina lake kwa kucheza,
    Kwa matari na kinubi wamwimbie.
    Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake,
    Huwapambana wenye upole kwa wokovu. (K)
  2. Watauwa na washangilie utukufu,
    Waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao.
    Sifa kuu za Mungu na ziwe vinywani mwao,
    Hiyo ndio heshima ya watauwa wake wote.
    Aleluya. (K)

INJILI: Lk. 19:41-44

Yesu alipofika karibu Na Yerusalemu aliuona mji, akaulilia, akisema, “Laiti ungalijua, hata wewe, katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako. Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote; watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako.”

TAFAKARI
KWA KIFO CHAKE TULIKOMBOLEWA: Askari mashuhuri sana aliyepigana vita na mara nyingi alishinda akiwa kwenye harakati za kuiokoa nchi yake kutoka katika uvamizi aliuawa. Wakati wa mazishi yake mama mmoja alifika kuutazama mwili wa marehemu, huku akimbeba mwanawe wa kiume, alimwambia mwanawe, “Chukua muda, muda wa kutosha mwanangu mtazame huyu mtu. Ni shujaa aliyekufa kwa ajili yako.” Aliyoyasema huyo mama yanasemwa na kanisa leo kwa kila mtu juu ya Yesu Kristo, “Chukua muda, muda wa kutosha mwanangu mpedwa wangu, mtazame Kristo, alikufa kwa ajili yako.” Mtu asiyapuuze mafundisho ya Kanisa kwani hili hufanya utume uliokabidhiwa na Kristo. Kristo anaulilia mji wa Yerusalemu kwa kutofuatilia mafundisho ya Kimungu. Kristo ndiye Aliyechinjwa akamnunulia Mungu taifa teule, na watu wakamilifu kwa damu yake. Sasa sio tu wale wakaazi wa mji wa Yerusalemu bali watu wa kila kabila na lugha na jamaa na mataifa yote. Sote tu wana wa urithi.

SALA: Ee Bwana, uniangazie mwanga wako uniwezeshe kuelewa na kufafanua mafudisho yako. Amina.