Novemba 10,2022; Alhamisi: Juma La 32 La Mwaka

Mt. Leo Mkuu, Baba Mt. na Mwalimu wa Kanisa
Kumbukumbu
Kijani
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: Flm. 7-20

Nalikuwa na furaha nyingi na faraja kwa sababu ya upendo wako, kwa kuwa mioyo ya watakatifu imeburudishwa nawe, ndugu yangu. Kwa hiyo, nijapokuwa nina ujasiri katika Kristo kukuagiza likupasalo; lakini, kwa ajili ya upendo nakusihi, kwa kuwa ni kama nilivyo, Paulo mzee, na sasa mfungwa wa Kristo Yesu pia. Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa katika vifungo vyangu, yaani, Onesimo; ambaye zamani alikuwa hakufai, bali sasa akufaa sana, wewe na mimi pia; niliyemtuma kwako, yeye mwenyewe, maana ni moyo wangu hasa; ambaye mimi nalitaka akae kwangu, apate kunitumikia badala yako katika vifungo vya injili. Lakini sikutaka kutenda neno lo lote isipokuwa kwa shauri lako, ili kwamba wema wako usiwe kwa lazima, bali kwa hiari. Maana, labda ndiyo sababu alitengwa nawe kwa muda, ili uwe naye tena milele; tokea sasa, si kama mtumwa, bali zaidi ya mtumwa, ndugu mpendwa; kwangu mimi sana, na kwako wewe zaidi sana, katika mwili na katika Bwana. Basi kama ukiniona mimi kuwa mshirika nawe, mpokee huyu kama mimi mwenyewe. Na kama amekudhulumu, au unamwia kitu, ukiandike hicho juu yangu. Mimi Paulo nimeandika kwa mkono wangu mwenyewe, mimi nitalipa. Sikuambii kwamba nakuwia hata nafsi yako. Naam, ndugu yangu, nipate faida kwako katika Bwana; uniburudishe moyo wangu katika Kristo.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 146 : 7-10

  1. Bwana huishika kweli milele,
    Huwafanyia hukumu walioonewa,
    Huwapa wenye njaa chakula,
    Hufungua waliofungwa.

(K) Heri ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake.

  1. Bwana huwafumbua macho waliopofuka,
    Bwana huwainua walioinama,
    Bwana huwapenda wenye haki,
    Huwahifadhi wageni. (K)
  2. Huwategemeza yatima na mjane,
    Bali njia ya wasio haki huipotosha.
    Bwana atamiliki milele,
    Mungu wako, Ee Sayuni, kizazi kwa kizazi.

INJILI: Lk. 17:20-25

Yesu alipoulizwa na Mafarisayo, “Ufalme wa Mungu utakuja lini?” Aliwajibu akawaambia, “Ufalme wa Mungu hauji kwa kuuchunguza; wala hawatasema, ‘Tazama, upo huku, au, kule,’ kwa maana, tazama, ufalme wa Mungu umo ndani yenu.” Akawaambia wanafunzi, “Siku zitakuja mtakapotamani kuona siku moja katika siku zake Mwana wa Adamu, msiione. Tena watawaambia, ‘Tazama, kule! Tazama, huku!’ Msiondoke mahali mlipo, wala msiwafuate; kwa kuwa, kama vile umeme umulikavyo toka upande huu chini ya mbingu hata upande huu chini ya mbingu, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu katika siku yake. Lakini kwanza, hana budi kupata mateso mengi, na kukataliwa na kizazi hiki.”

TAFAKARI
UFALME WA MUNGU UPO KATI YETU: Binti mdogo alimkuta babu yake penye kisima akiteka maji. Akamsalimu kisha akamwambia, “Babu naomba nikusaidie kubeba maji.” Babu akamjibu, “Asante mjukuu wangu, nikuulize swali dogo kama wewe, ‘Mungu anaishi wapi?’” Binti alijibu “Sijui babu nisaidie kufahamu.” Babu akamwinua akamweka kwa namna ambayo angejiona kwenye maji, akamwambia angalia kwenye maji. Akamuuliza, “Unaona nini?” Binti alijibu, “Najiona mwenyewe.” Babu akamwambia kuwa hapo ndipo Mungu anakoishi, Mungu anaishi ndani mwako. Tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu (Mwanzo 1:26-27). Ufalme wa Mungu uko hivyo pia, hauko hapa wala pale bali upo ndani na kati yetu, “mioyoni mwetu” (Luka 17:21). Tunapoishi kama ndugu, tunalifuata fundisho tunalopata kutoka kwa Paulo anapomsihi Filemoni amsamehe Onesmo na kumkaribisha kama ndugu na si mtumwa. Ufalme wa Mungu upo katika kutambua kuwa sisi sote ni watoto wa Mungu, na ya kuwa sisi ni ndugu. Tukaribishane na kutumikiana kwa upendo.

SALA: Ee Bwana, nipe neema ya kukutunza katika maisha yangu na watu wote. Amina.