Mt. Wilibrodi, Askofu na Mtawa
Zaburi: Juma 4
SOMO I: Tit. 1:1-9
Paulo, mtumwa wa Mungu, na mtume wa Yesu Kristo; kwa ajili ya imani ya wateule wa Mungu, na ujuzi wa kweli ile iletayo utauwa; katika tumaini la uzima wa milele, ambao Mungu asiyeweza kusema uongo aliuahidi tangu milele; akalifunua neno lake kwa majira yake katika ule ujumbe niliowekewa amana mimi kwa amri ya Mwokozi wetu Mungu; kwa Tito, mwanangu hasa katika imani tuishirikiyo. Neema na iwe kwako na amani zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Mwokozi wetu. Kwa sababu hii nalikuacha Krete, ili uyatengeneze yaliyopunguka, na kuweka wazee katika kila mji kama vile nilivyokuamuru; ikiwa mtu hakushitakiwa neno, naye ni mume wa mke mmoja, ana watoto waaminio, wasioshitakiwa kuwa ni wafisadi wala wasiotii. Maana imempasa askofu awe mtu asiyeshitakiwa neno, kwa kuwa ni wakili wa Mungu; asiwe mtu wa kujipendeza nafsi yake, asiwe mwepesi wa hasira, asiwe mlevi wala mgomvi, asiwe mpenda mapato ya aibu; bali awe mkaribishaji, mpenda wema, mwenye kiasi, mwenye haki, mtakatifu, mwenye kuthibiti nafsi yake; akilishika lile neno la imani vile vile kama alivyofundishwa, apate kuweza kuwaonya watu kwa mafundisho yenye uzima, na kuwashinda wenye kupinga.
Wimbo Wa Katikati: Zab. 24:1-6
- Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana,
Dunia na wote wakaao ndani yake.
Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari,
Na juu ya mito ya maji aliithibitisha.
(K) Hiki ndicho kizazi cha wakutafutao, Ee Bwana.
- Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana?
Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?
Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe,
Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili. (K) - Atapokea Baraka kwa Bwana,
Na haki kwa Mungu wa wokovu wake.
Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao,
Wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo. (K)
INJILI: Lk. 17:1-6
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja kwa sababu yake! Ingemfaa zaidi mtu huyo jiwe la kusagia lifungwe shingoni mwake, akatupwe baharini, kuliko kumkosesha mmojawapo wa wadogo hawa. Jilindeni. Kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe. Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, ‘Nimetubu,’ msamehe.’” Mitume wakamwambia “Bwana, Tuongezee imani.” Bwana akasema, “Kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, ng’oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii.”
TAFAKARI
TUELEKEZE WENGINE KWENYE MEMA: Tunaalikwa kuwa wapenda wema, kiasi, haki, matakatifu, na kuthibiti nafsi. Tukifanya hivi, tutalishika Neno na kuwaonya watu kwa mafundisho yenye uzima. Mbinu hii itatupa uwezo wa kukaribiana na Mungu ili tuweze kuwashinda wenye kupinga au kuharibu imani. Mzee mmoja alikuwa katika hali ya kufa akafungua kinywa chake akasema, “Nilipokuwa mtoto nlikuwa nacheza katika kiwanja kilicho karibu na makutano ya njia mbili. Mle pembezoni mwa barabara palikuwa na kibao kilichoelekeza njia ya kufuata. Siku moja nilikilenga kile kibao mshale, ila mshale huo ukaelekea kwengine. Ninapokufa sasa najiuliza ni watu wangapi niliwaelekeza katika njia isiyo sawa katika maisha kwa matendo yasiyofaa? Makwazo ni kuwaelekeza watu visivyp, hasa vijana na watoto. Yote tufanyayo au tusemayo, kunao wanaotutazama na kutusikiliza. Kwa wengi, hasa wale wachanga, watayaiga. Yawe mema au mabaya, kamwe hatutakosa mtu wa kuyaiga. Ingekuwa heri kama tungeyatenda mema ili wayaigapo, wawe watu wa kutenda mema!
SALA: Ee Bwana, unipe neema yako niwe mfano mwema na kuwaelekeza wengine kwenye wema. Amina.