Novemba 6,2022; Jumapili: Jumapili Ya 32 Ya Mwaka

Mwaka C
Kijani
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: 2 Mak. 7:1-2, 9-14

Ilitokea ya kuwa ndugu saba, pamoja na mama yao, walikamatwa kwa amri ya mfalme na kuteswa sana kwa mijeledi na mapigo ili kuwashurutisha kuonja nyama marufuku ya nguruwe. Mmoja akajifanya mnenaji wao, akasema, “Wataka kuuliza nini na kujua nini juu yetu? Sisi tu tayari kufa kuliko kuzivunja amri za wazee wetu.” Wa pili alipokuwa kufani alisema, “Wewe, mdhalimu, unatufarikisha na maisha ya sasa, lakini Mungu wa ulimwengu atatufufua sisi tuliokufa kwa ajili ya amri zake, hata tupate uzima wa milele.” Na baada yake alidhihakiwa yule wa tatu. Naye mara alipoagizwa, alitoa ulimi wake, akanyosha mikono yake bila hofu, akasema kwa ushujaa, “Kutoka mbinguni nalipewa hivi, na kwa ajili ya amri za Mungu navihesabu kuwa si kitu, na kwake natumaini kuvipokea tena.” Hata mfalme na watu wake walishangazwa kwa roho ya kijana huyu, kwa jinsi alivyoyadharau maumivu yake. Akiisha kufa huyu, walimtesa wa nne na kumtendea mabaya yale yale. Naye alipokaribia kufa alisema hivi; “Ni vema kufa kwa mikono ya wanadamu na kuzitazamia ahadi zitokazo kwa Mungu, kuwa tutafufuliwa naye. Lakini kwako wewe hakuna ufufuo.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 17:1, 5-6, 8, 15

  1. Ee Bwana, usikie haki, usikilize kilio changu
    Utege sikio lako kwa maombi yangu.
    Yasiyotoka katika midomo ya hila.

(K) Ee, Bwana niamkapo nitashibishwa kwa sura yako.

  1. Nyayo zangu zimeshikamana na njia zako,
    Hatua zangu hazikuondoshwa.
    Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika,
    Utege sikio lako ulisikie neno langu. (K)
  2. Unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako;
    Bali mimi nikutazame uso wako katika haki.
    Niamkapo nishibishwe kwa sura yako. (K)

SOMO 2: 2Thes. 2:16-3:1-5

Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe, na Mungu Baba yetu, aliyetupenda akatupa faraja ya milele na tumaini jema, katika neema, awafariji mioyo yenu, na kuwafanya imara katika kila neno na tendo jema. Hatimaye, ndugu, tuombeeni, neno la Bwana liendelee, na kutukuzwa vile vile kama ilivyo kwenu; tukaokolewe na watu wasio haki, wabaya; maana si wote walio na imani. Lakini Bwana ni mwaminifu, atakayewafanya imara na kuwalinda na yule mwovu. Nasi tumemtumaini Bwana kwa mambo yenu, kwamba mnayafanya tuliyowaagiza, tena kwamba mtayafanya. Bwana awaongoze mioyo yenu mkapate pendo la Mungu, na saburi ya Kristo.

SHANGILIO Yn. 1:12, 14

Aleluya, aleluya,
Naye neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu.
Aleluya.

INJILI: Lk. 20:27-38

Baadhi ya Masadukayo, wale wasemao ya kwamba hakuna ufufuo, walimwendea Yesu, wakamwuliza, wakisema, “Mwalimu, Musa alituandikia ya kuwa, mtu akifiwa na ndugu yake mwenye mke, lakini hana mtoto, na amtwae huyu mke, ampatie ndugu yake mzao. Basi, kulikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa mke, akafa hana mtoto; na wa pili akamtwaa yule mke, akafa hana mtoto; hata wa tatu akamwoa, na kadhalika wote saba, wakafa, wasiache watoto. Mwisho akafa yule mke naye. Basi, katika ufufuo atakuwa mke wa yupi? Maana aliolewa na wote saba.” Yesu akawaambia, “Wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa; lakini, wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi, wala hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuo. Lakini, ya kuwa wafu hufufuliwa, hata na Musa alionyesha katika sura ya Kijiti, hapo alipomtaja Bwana kuwa ni Mungu wa Ibrahimu na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Naye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai; kwa kuwa wote huishi kwake.”

TAFAKARI
UFUFUKO UTAWEZESHA MAISHA YETU YA MILELE: Yesu ananena na Masadukayo, akitoa uhakika wa ufufuko wa wafu. Kati ya Wayahudi kulikuwa na makundi kama saba hivi: Mafarisayo, waandishi wa sheria, Masadukayo (makuhani pamoja na makuhani wakuu), Wasamaria, Waeseni, Maherodi na Wazeloti. Kuendana na mgawanyiko huu walitofautiana katika vipengele vingi vya imani. Kati ya tofauti hizo, tofauti kati ya Mafarisayo na waandishi wa sheria, kwa upande moja na Masadukayo kwa upande mwingine, zilitingisha sana jamii. Mafarisayo na rafiki zao waandishi wa sheria walikuwa dhidi ya Masadukayo kiasi kwamba walichukiana. Ndiyo maana Yesu alipokuwa anawashinda watu wa upande mmoja wale wa upande wa pili walifurahi (Mt 22:34).
Tunaokutana nao leo ni Masadukayo. Hawa hawakusadiki ufufuko wa wafu, wala uwepo wa malaika, uwepo wa roho. Mafarisayo na waandishi wa sheria waliyasadiki hayo yote (Mdo 23:6-11). Masadukayo wanataka kukejeli ufufuko mbele ya Yesu. Wanaanza kwa kusimulia tukio la Sara binti Ragueli aliyesimuliwa katika kitabu cha Tobiti, binti ambaye aliolewa na wanaume saba lakini wote wakafa pasipo kumwacha mtoto yoyote. Kadiri ya imani ya Wayahudi, ushahidi wa mtoto au watoto wawili (mmoja wa kike na mwingine wa kiume), ulikuwa mwema. Ili kuweza kuupata ushahidi wa ndoa, ndipo ilipozalika tabia ya ndugu kumrithi mjane.
Katika mazingira hayo walianza ndugu wa damu wa kaka aliyeacha mke. Waliulizwa mmoja mmoja kama walitaka kumrithi shemeji yao au la. Kama mtu alikubali alimrithi shemeji yake na kujitahidi kumzalia mtoto. Mtoto wa kiume wa kwanza wa huyo mjane na ndugu wa marehemu mumewe aliyemrithi alihesabiwa mali ya kaka yake aliyefariki duniani na hivyo kumpatia yeye na mkewe aliyemwoa ushahidi wa ndoa yao. Pale ilipoondokea mtu kumkataa shemeji yake, basi shauri hili lililetwa barazani ambapo palifanyika madhehebu rasmi ya kukataa kumrithi mjane. Hapo barazani yule mwanamke aliyekataliwa kurithiwa aliamriwa kumvua kiatu huyo asiyetaka kumrithi na kisha kumtemea mate utosini huku akisema, “Hayo ndiyo yanayompata mtu aliyekataa kutimiza wajibu wa kaka yake.” Matendo haya ndiyo yalijulikana kwa jumla ibada ya “kuvuliwa kiatu” (Kum 25:5-10).
Simulizi waliloleta Masadukayo lilikuwa la mazingira haya. Wanamwambia Yesu kwamba mbinguni huenda kukawa na vurugu wafufuka wakigombania wake. Kwa kuijibu keheli hii, Yesu anawaonyesha kuwa wamefeli. Mbinguni hakuna vurugu za kugombania wake kwani kwanza huko hawaoi na kuolewa. Pili, ufufuko ni halisi kwa sababu kama Mungu anaitwa wa fulani na fulani, watu ambao wamekufa duniani, maana yake watu hao sasa wanaishi kwake. Hii maana yake roho za marehemu zinaishi kwa Mungu na mwishoni mwa historia ufufuko wa miili yao utawezesha maisha ya milele makamilifu.
Ujumbe wa somo la kwanza ni kuwa tumaini katika ufufuko linashinda kila tisho duniani, ikiwemo tisho la kifo. Watoto saba wa mama mmoja wanapokea kifodini kwa kuwa wamejaa tumaini. Wanamtangazia mfalme mambo manne. Kwanza, walikuwa tayari kufa kuliko kuzivunja amri za wazee wao na walikuwa tayari kutenganishwa na maisha ya dunia, kwa vile walikuwa na hakika Mungu wa ulimwengu atawafufua wafu na wapate uzima wa milele. Pili, walisema walikuwa tayari kutoa ndimi zao na mikono yao kwa sababu walipewa vitu hivyo na Mungu na kwa ajili ya amri za Mungu walivihesabu kuwa si kitu kwa vile walitumaini kuvipokea tena. Tatu, walisema waliona vema kufa kwa mikono ya wanadamu na kuzitazamia ahadi zitokazo kwa Mungu, kuwa watafufuliwa naye. Hatimaye, nne, kwa upande wa mfalme, pasipo kumwogopa, walimwambia hatajaliwa ufufuo kwa uzima wa milele kwa sababu ya uovu wake. Je, sisi tuko tayari kujitoa kwa ajili ya imani yetu? Tunayo imani halisi kuwa tuondokapo ulimwenguni humu tunayo maisha ya milele?

SALA: Ee Mungu Mwenyezi, tunatamani roho zetu zikusanyike kwako na siku ya kiyama utukamilishe kwa kutufufulia na kutupatia miili yetu. Siku zote utudumishe katika imani na matarajio haya. Usituache tunaaibika katika matumaini yetu. Amina.