Wat. Zakaria na Elizabeti
Kijani
Zaburi: Juma 3
SOMO I: Fil. 4:10-19
Nalifurahi sana katika Bwana, kwa kuwa sasa mwisho mmehuisha tena fikira zenu kwa ajili yangu, kama vile mlivyokuwa mkinifikiri hali yangu; lakini hamkupata nafasi. Si kwamba nasema haya kwa kuwa nina mahitaji; maana nimejifunza kuwa radhi na hali yoyote niliyo nayo. Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yoyote, na katika mambo yoyote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa. Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu. Lakini mlifanya vema, mliposhiriki nami katika dhiki yangu. Nanyi pia, ninyi wenyewe mnajua, enyi Wafilipi, ya kuwa katika mwanzo wa injili, nilipotoka Makedonia, hakuna kanisa lingine lililoshirikiana nami katika habari hii ya kutoa na kupokea, ila ninyi peke yenu. Kwa kuwa hata huko Thesalonike mliniletea msaada kwa mahitaji yangu, wala si mara moja. Si kwamba nakitamani kile kipawa, bali nayatamani mazao yanayozidi kuwa mengi, katika hesabu yenu. Lakini ninavyo vitu vyote na kuzidi, tena nimejaa tele; nimepokea kwa mkono wa Epafrodito vitu vile vilivyotoka kwenu, harufu ya manukato, sadaka yenye kibali, impendezayo Mungu. Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu.
Wimbo Wa Katikati: Zab. 112:1-2, 5-6, 8, 9
- Aleluya.
Heri mtu yule amchaye Bwana,
Apendwezaye sana maagizo yake.
Wazao wake watakuwa hodari duniani;
Kizazi wenye adili adili kitabarikiwa.
(K) Heri mtu yule amchaye Bwana.
- Heri atendaye fadhili na kukopesha;
Atengenezaye mambo yake kwa haki.
Kwa maana hataondoshwa kamwe;
Mwenye haki atakumbukwa milele. (K) - Moyo wake umethibitika hataogopa,
Amekirimu, na kuwapa maskini,
Haki yake yakaa milele,
Pembe yake itatukuzwa kwa utukufu. (K)
INJILI: Lk. 16:9-15
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Jifanyieni rafiki kwa mali ya udhalimu, ili itakapokosekana wawakaribishe katika makao ya milele. Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia. Bali, kama ninyi hamkuwa waaminifu katika mali ya udhalimu, ni nani atakayewapa amana mali ya kweli? Na kama hamkuwa waaminifu katika mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewapa iliyo yenu wenyewe? Hakuna mtumishi awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana, ama atamchukia huyu na kumpenda huyu, ama atashikamana na huyu na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali. Basi Mafarisayo, ambao wenyewe ni wapenda fedha, waliyasikia hayo yote, wakamdhihaki.” Akawaambia, “Ninyi ndinyi mnaojidai haki mbele ya wanadamu, lakini Mungu awajua mioyo yenu; kwa kuwa lililo tukuka kwa wanadamu huwa chukizo mbele za Mungu.”
TAFAKARI
KILA UZOEFU NI FURSA, TUITUMIE KWA WOKOVU: Fursa ni kutumia nafasi au hali iliyopo kwa manufaa binafsi na jamii. Habari Njema ya wokovu wetu ilihubiriwa katika maeneo na watu mbalimbali imetoa fursa kwa watu kuwa na ufahamu mpana wa yale yatarajiwayo na thamani ya wokovu. Mgonjwa mmoja aliyekuwa mahututi alisema “ninalo la kushirikisha, ninacho cha kutoa japo nipo kitandani siwezi kuinuka. Naishi usasa, kuisha wakati ujao haitakuwa na maana kwangu, hali niliyo nayo sasa ni ya thamani sana. Mungu anaendelea kujidhihirisha katika ubinadamu wetu na fursa tunazokutana nazo. Hali yoyote tunayokutana nayo ni nafasi ya utume wetu. Kwa Mkristo wakati wote ni wakati wa kutimiza utume, hapa nilipo sasa ndio wakati wa kutimiza utume, ndicho Kristo alichomaanisha aliposema ninyi ni chumvi na ni mwanga wa ulimwengu.” Tumekabithiwa mwanga wakati wa ubatizo wetu tukaambiwa tutembee kama watoto wa nuru na mwisho huko mbinguni tumlaki Bwana (Utaratibu wa Kikatoliki wa Ubatizo)
SALA: Ee Bwana Yesu unijaze ujasiri niendelee kuangaza kwa mwanga wako popote niwapo. Amina.