Mt. Karoli Boromeo, Askofu
Kijani
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Fil. 3: 17 – 4: 1
Ndugu zangu, mnifuate mimi, mkawatazame wao waendao kwa kuufuata mfano tuliowapa ninyi. Maana wengi huenenda, ambao nimewaambieni mara nyingi habari zao, na sasa nawambia hata kwa machozi, kuwa ni adui za msalaba wa Kristo; Mwisho wao ni uharibifu, mungu wao ni tumbo, utukufu wao u katika fedheha yao, waniao mambo ya dunia. Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo; atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake. Basi ndugu zangu, wapendwa wangu, ninaowaonea shauku, furaha yangu, na taji yangu, hivyo simameni imara katika Bwana, wapenzi wangu.
Wimbo Wa Katikati: Zab. 122: 1-5
- Nalifahamu waliponiambia,
Na twende nyumbani kwa Bwana.
Miguu yetu imesimama
Ndani ya malango yako, Ee Yerusalemu.
(K) Nalifurahi waliponiambia, na twende nyumbani kwa Bwana.
- Ee Yerusalemu uliyejengwa
Kama mji ulioshikamana,
Huko ndiko walikopanda kabila,
Kabila za Bwana. (K) - Ushuhuda kwa Israeli,
Walishukuru jina la Bwana.
Maana huko viliwekwa viti vya hukumu,
Viti vya enzi vya mbari ya Daudi. (K)
INJILI: Lk. 16:1-8
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyekuwa na wakili wake; huyu alishitakiwa kwake kuwa anatapanya mali zake. Akamwita, akamwambia, ‘Ni habari gani hii ninayosikia juu yako? Toa hesabu ya uwakili wako, kwa kuwa huwezi kuwa wakili tena.’ Yule wakili akasema moyoni mwake, ‘Nifanyeje? Maana, bwana wangu ananiondolea uwakili. Kulima, siwezi; kuomba, naona haya. Najua nitakalotenda, ili nitakapotolewa katika uwakili, wanikaribishe nyumbani mwao.’ Akawaita wadeni wa bwana wake, kila mmoja; akamwambia wa kwanza, ‘Wawiwani na bwana wangu?’ Akasema, ‘Vipimo mia vya mafuta’. Akamwambia, ‘Twaa hati yako, keti upesi, andika hamsini.’ Kisha akamwambia mwingine, ‘Na wewe wawiwani?’ Akasema, ‘Makanda mia ya ngano. Akamwambia, ‘Twaa hati yako, andika themanini.’” Yule bwana akamsifu wakili dhalimu kwa vile alivyotenda kwa busara; kwa kuwa wana wa ulimwengu huu katika kizazi chao wenyewe huwa na busara kuliko wana wa nuru.
TAFAKARI
JENGA URAFIKI NA MSALABA WA KRISTO: Msalaba wa Kristo ni kielelezo cha uaminifu, upendo, utii, mwanga na wokovu wa binadamu. Kinyume na mambo ya dunia, hila, wizi au udhalimu. Katika sehemu ya Injili Bwana anamsifu wakili dhalimu kwa sababu ya werevu wake juu ya mambo ya duniani, hata kama angalikua na busara kwa mambo ya mbinguni. Je mtu aweza kuwa mwerevu kwa mambo ya mbinguni pia? Ndiyo Kristo anatuita kuwa wana wa mwanga na kujipanga kwa mambo yajayo ya ufalme wa Mungu. Yesu anatuambia anayetaka kumfuata ajikane mwenyewe achukue msalaba wake amfuate (Luka 9:23). Huyu wakili dhalimu anaonekana kuukwepa msalaba na hivyo kutumbukia katika udanganyifu na udhalimu. Mtu akijenga urafiki na msalaba wa Kristo Yesu, atapenda kutimiza wajibu umpasao kwa uaminifu akiziishi amri za Mungu huku akitumainia tuzo lijalo.
SALA: Ee Bwana unipe neema yako niyatimize majukumu yangu kwa uaminifu. Amina.