Oktoba 30,2022; Jumapili: Jumapili Ya 31 Ya Mwaka

Mwaka C
Kijani
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Hek. 11:22 – 12:2

Ulimwengu wote mbele zako Bwana, ni kama chembe moja katika mizani, na mfano wa tone moja la umande lishukalo asubuhi juu ya ardhi. Lakini Wewe unawahurumia watu wote, kwa sababu unao uweza wa kutenda mambo yote; nawe wawaachilia wanadamu dhambi zao, ili wapate kutubu. Kwa maana Wewe wavipenda vitu vyote vilivyopo, wala hukichukii kitu cho chote ulichokiumba. Kwa kuwa hungalifanya kamwe kitu cho chote kama ungalikichukia; tena kitu cho chote kingaliwezaje kudumu, ila kwa mapenzi yako? au kitu kisichoumbwa nawe kingaliwezaje kuhifadhika? Lakini Wewe unaviachilia vyote, kwa kuwa ni vyako, Ee Mfalme Mkuu, mpenda roho za watu; maana roho yako isiyoharibika imo katika vyote. Kwa hiyo wawathibitishia kidogo kidogo hatia yao, wale wanaokengeuka kutoka katika njia njema; wawaonya, ukiwakumbusha kwa mambo yale yale wanayokosa, ili waokoke katika ubaya wao, na kukuamini Wewe, Bwana.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 145:1-2, 8-11, 13-14

  1. Ee Mungu wangu, Mfalme, nitakutukuza,
    Nitalihimidi jina lako milele na milele.
    Kila siku nitakuhimidi,
    Nitalisifu jina lako milele na milele.

K: Ee Mungu Mfalme wangu, Nitalitukuza jina lako milele.

  1. Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma,
    Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema,
    Bwana ni mwema kwa watu wote.
    Na rehema zi juu ya viumbe vyake vyote. (K)
  2. Ee Bwana, viumbe vyako vyote vitakushukuru,
    Na wacha Mungu wako wote watakuhimidi.
    Waunena utukufu wa ufalme wako.
    Na kuuhadithia uweza wako. (K)
  3. Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote,
    Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote.
    Bwana huwategemeza wote waangukao,
    Huwainua wote walioinamia chini. (K)

SOMO 2: 2 Thes. 1:11 – 2:2

Kwa hiyo twawaombea ninyi siku zote, ili Mungu wetu awahesabu kuwa mmekustahili kuitwa kwenu, akatimiza kila haja ya wema na kila kazi ya imani kwa nguvu; jina la Bwana wetu Yesu litukuzwe ndani yenu, nanyi ndani yake, kwa neema ya Mungu wetu na ya Bwana Yesu Kristo. Basi, ndugu, tunakusihini, kwa habari ya kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, na kukusanyika kwetu mbele zake, kwamba msifadhaishwe upesi hata kuiacha nia yenu, wala msisitushwe, kwa roho, wala kwa neno, wala kwa waraka unaodhaniwa kuwa ni wetu, kana kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwapo.

SHANGILIO: Lk. 2:36

Aleluya, aleluya,
Kesheni ninyi kila wakati, mkiomba,
ili mpate kusimama mbele za Mwana wa Adamu.
Aleluya.
INJILI: Lk. 19:1-10

Yesu alipoingia Yeriko alipita katikati yake. Na tazama, palikuwa na mtu, jina lake Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye ni tajiri. Huyu alikuwa akitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani, asiweze kwa sababu ya umati wa watu, maana ni mfupi wa kimo. Akatangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu apate kumwona, kwa kuwa atakuja kuipitia njia ile. Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, “Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako.” Akafanya haraka, akashuka, akamkaribisha kwa furaha. Hata watu walipoona, walinung’unika wote, wakisema, “Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi.” Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, “Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang’anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne.”
Yesu akamwambia, “Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu. Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.”

TAFAKARI
TUJIONGEZE KIMO TUMWONE YESU: Zakayo mtoza ushuru alikuwa mfupi na ikambidi kujipandisha juu ya mti apate kumwona Yesu. Yesu alishapata umaarufu kutokana na mafundisho na matendo yake. La kushangaza ni kuwa Zakayo alikuwa bado hajamfahamu, labda kwa vile kwanza alikuwa mtu mwenye kazi ya tija sana, ndiyo kukusanya ushuru kwa ajili ya Warumi. Pili, kwa vile kazi ya utoza ushuru ilikuwa inaleta utajiri mkubwa. Huenda matajiri wale, kama walivyo wengine kati yetu, hawakuwa na haja ya kukutana na yeyote ambaye hangewaongezea chochote. Ila, Yesu alipoingia mjini Yeriko na watu wengi wakamsonga, Zakayo alipata hamu ya kumwona. Kwa vile alikuwa mfupi, na kutokana na umati mkubwa wa watu, aliamua kujiongeza kimo kwa kupanda juu ya mti. Afisa mkubwa na mtu tajiri kupanda juu ya mti ili amwone mtu anayepita, halikuwa jambo dogo. Kutokujali kwake, kujikosesha heshima na kutoona kwake aibu ni ushahidi wa hamu yake ya pekee.
Yesu naye aliitumia fursa hii kumvua. Alimwomba ashuke, na akaomba aingie nyumbani mwake. Huko, Zakayo aliongoka na akaahidi kurekebisha maisha yake kwa kuwagawia maskini nusu ya mali yake na kuwalipa aliowadhulumu mara nne nne. Jambo hili liliwasikitisha waliokuwa wanataka wadhambi wasisaidiwe. Kwake Yesu, alifurahia kurejea kwa mkosefu, “siku ile wokovu ulifika nyumbani kwa Zakayo mdhambi. Yeye Yesu alikuja duniani kwenye mradi wa kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.
Somo la kwanza linatangaza jinsi Mungu anavyoweza kuonekana na yeyote hata na wakosefu. Kunayo mazingira matatu yanayowezesha hili. Mosi, mazingira ya huruma yenye subira. Mungu anawahurumia watu wote kwa sababu ni wake na anapenda wawepo wasipotee. Kwa hiyo anawaachilia wanadamu dhambi zao, ili wapate kutubu. Anafanya hivyo kwa sababu anavipenda vitu vyote vilivyopo, wala hakichukii kitu cho chote alichokiumba. Pili, uwapo wa roho yake katika vitu vyote. Mungu ameweka roho yake katika vyote. Kwa hiyo anawatakia wote waifuate njia njema. Tatu, kazi ya uonyaji inayoendelea. Mungu hachoki kuwaonya wakosefu. Kwenye dhamiri kila mara anatukumbusha makosa, ili tuokoke na kumwamini. Mtu asiyeisikia dhamiri yake ikimwonya ameamua kujifanya zuzu. Kutokana na hayo matatu, Zakayo anapata nafasi ya kumwona Mwokozi na kuongoka. Laiti nasi tungalifanya juhudi kuyatilia maanani mazingira haya ya Mungu ili yatufae!
Somo la pili linaeleza vitu viwili muhimu: kuwaombea wengine, na kutobabaika. Akina Paulo waliwaombea Wathesalonike siku zote kusudi Mungu astahilishe kuitwa kwao. Waliwaombea ili jina la Bwana wetu Yesu litukuzwe ndani yao. Vilevile, Paulo anawasihi Wathesalonike wasifadhaishwe wala kusitushwa, kwa roho, kwa neno, wala kwa waraka. Kubabaika hutoa watu kwenye njia ya kuongoka.
Kutokana na yote, ujumbe ni kuwa, Mungu ametuwekea mazingira mwafaka ili tuweze kuishi vyema na hatimaye kuurithi Ufalme wake. Dhambi hutufupisha na kutuzuia kuufikia wema huu wa Mungu. Lakini, tukiyafuata vyema Maandiko Matakatifu, na Katekisimu ya Kanisa Katoliki, ikiwemo na kuwasikiliza mapadre na viongozi wa Kanisa, tutapata mchakato utakaozilisha roho zetu. Hili litatuwezesha kuombeana na kusaidiana. Tukifanya hivyo bila shaka tutakuwa Wakristo wema.

SALA: Ee Yesu Kristo, tutie hamu ya kujiongeza kimo kufuatia Maandiko Matakatifu, na Sakramenti. Amina.