Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Efe. 4:1-6
Nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani. Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja. Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote.
Wimbo Wa Katikati: Zab. 24:1-6
- Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana,
Dunia na wote wakaao ndani yake.
Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari,
Na juu ya mito ya maji aliithibitisha.
(K) Hiki ndicho kizazi cha wakutafutao, Ee Bwana.
- Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana?
Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?
Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe,
Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili,
Wala hakuapa kwa hila. (K) - Atapokea Baraka kwa Bwana,
Na haki kwa Mungu wa wokovu wake.
Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao,
Wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo. (K)
INJILI: Lk. 12:54-59
Yesu aliwaambia makutano pia, “Kila mwonapo wingu likizuka pande za magharibi mara husema, ‘Mvua inakuja’; ikawa hivyo. Na kila ivumapo kaskazi, husema, ‘Kutakuwa na joto’; na ndivyo ilivyo. Enyi wanafiki, mwajua kuutambua uso wa nchi na mbingu; imekuwaje, basi, kuwa hamjui kutambua majira haya? Na mbona ninyi wenyewe kwa nafsi zenu hamwamui yaliyo haki? Maana, unapofuatana na mshitaki wako kwenda kwa mwamuzi, hapo njiani fanya bidii kupatanishwa naye, asije akakuburuta mpaka mbele ya kadhi; yule kadhi akakutia mikononi mwake mwenye kulipiza, na yule mwenye kulipiza akakutupa gerezani.’” Nakuambia, “Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho.”
TAFAKARI
TUSOME ISHARA ZA NYAKATI: Katika Injili Yesu anatumia mifano ya kawaida kabisa ya hali ya hewa, kufundisha watu kuhusu muda walionao wa kuishi ulimwenguni. Ni kama msemo “Dalili ya mvua ni mawingu”. Kama ilivyo desturi ya watu kutafsiri hali ya hewa kwa manufaa ya kimwili, elimu hiyo inapaswa kutumika kwa yale ya kiroho. Kristo anatualika leo tuwe washtakiwa, washtaki na mahakimu wa haki tunapojipanga kwenda kukutana na Mungu. Tukielewa hivyo tunapaswa kufanya nini? Tuamue yaliyo ya haki yaani kutenda mema kwa wenzetu.Tuishi kulingana na kanuni ya dhahabu usilotaka kutendewa usimtendee mwenzako. Maisha yetu hapa duniani ni kama tupo safarini, hivyo tujipange sawasawa kwenda kukutana na Mungu wetu. Tujipatanishe vema na Mungu na jirani zetu ili tuondokapo hapa tusiwe na deni la kulipa. Muda wa kutengeneza mambo yetu na Mungu wetu ni sasa na siyo baadaye. Tutumie vizuri muda tulionao, tujitahidi kuishi kwa unyenyekevu, upendo na uvumilivu.
SALA: Ee Mungu, nipe neema na nguvu za kuwa mwamuzi wa haki.