Oktoba 19,2022; Jumatano: Juma La 29 La Mwaka

Wat. Yohane Brebe na Isaaki Yog, Mapadre na Wenzake Mashahidi /Mt. Paulo wa Msalaba, Padre
Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Efe. 3:2-12

Mmesikia habari ya uwakili wa neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu; ya kwamba kwa kufunuliwa nalijulishwa siri hiyo, kama nilivyotangulia kuandika kwa maneno machache. Kwa hayo, myasomapo, mtaweza kuutambua ufahamu wangu katika siri yake Kristo. Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho; ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili; Injili hiyo ambayo nalifanywa mhudumu wake, kwa kadiri ya kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa kadiri ya utendaji wa uweza wake. Mimi, niliye mdogo kuliko yeye aliye mdogo wa watakatifu wote, nalipewa neema hii ya kuwahubiri Mataifa utajiri wake Kristo usiopimika; na kuwaangaza watu wote wajue habari za madaraka ya siri hiyo, ambayo tangu zamani zote ilisitirika katika Mungu aliyeviumba vitu vyote; ili sasa, kwa njia ya kanisa, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho; kwa kadiri ya kusudi la milele alilolikusudia katika Kristo Yesu Bwana wetu. Katika yeye tunao ujasiri na uwezo wa kukaribia katika tumaini kwa njia ya kumwamini.

Wimbo Wa Katikati: Isa. 12:2-6

 1. Tazama,Mungu ndiye wokovu wangu;
  Nitatumaini wala sitaogopa;
  Maana Bwana Yehova ni nguvu zangu
  Na wimbo wangu;
  Naye amekuwa wokovu wangu.
  Basi, kwa furaha mtateka maji
  Katika visima vya wokovu.

(K) Kwa furaha mtateka maji
katika visima vya wokovu.

 1. Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake;
  Yatangazeni matendo yake kati ya mataifa,
  Litajeni jina lake kuwa kuwa limetukuka.
  Mwimbieni Bwana. (K)
 2. Kwa kuwa ametenda makuu,
  Na yajulikane haya katika dunia yote.
  Paza sauti, piga kelele, mwenyeji wa Sayuni;
  Maana Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako. (K)

INJILI: Lk. 12:39-48

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Fahamuni neno hili, Kwamba mwenye nyumba angalijua saa atakayokuja mwivi; angalikesha, wala asingaliacha nyumba yake kuvunjwa. Nanyi jiwekeni tayari, kwa kuwa saa msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu.” Petro akamwambia, “Bwana, mithali hiyo umetuambia sisi tu, au watu wote pia?” Bwana akasema, “Ni nani, basi, aliye wakili mwaminifu, mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya utumishi wake wote, awape watu posho kwa wakati wake? Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta anafanya hivyo.” Kweli nawaambia, “Atamweka juu ya vitu vyake vyote.” Lakini, mtumwa yule akisema moyoni mwake, “Bwana wangu anakawia kuja, akaanza kuwapiga wajoli wake, wanaume kwa wanawake, akila na kunywa na kulewa.” Bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyojua, atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wasioamini. Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana. Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi.

TAFAKARI
SIFA ZA MTUMISHI MWAMINIFU: Yesu anazungumza kuhusu watumishi wa aina mbili: mtumishi mwaminifu na asiyemwaminifu. Mtumishi hutazamwa kuwa mwaminifu na mwenye busara katika utendaji wake wakati Bwana wake yuko mbali naye. Kama atakuwa anatenda kadiri ya matakwa ya Bwana wake kwa uaminifu na busara, atapewa tuzo na mamlaka makubwa zaidi. Anayekwenda kinyume na matakwa ya Bwana wake atapata adhabu. Kwetu sisi Yesu ndiye Bwana wetu, ameshatufundisha yote na kutuelekeza lipi jema tulifanye na lipi ovu tuliepuke. Je, tunafanyaje ili kujiandaa na maisha ya kukutana naye siku ya kiama? Je, ninaishi kama maisha haya ya sasa ndio mwisho wa kila kitu? Tunaposubiri siku hiyo, tutende matendo ya huruma kwa wengine. Tuishi kiaminifu katika amri za Mwenyezi Mungu na tungojee siku hiyo kwa matumaini. Wokovu wetu unatutaka kushirikiana na Mungu ipasavyo. Sasa ndiyo muda wa kuonyesha ushirikiano huo tungalipo hapa duniani.

SALA: Ee Mungu, naomba uniandalie makao mema. Amina.