Mt. Luka, Mwinjili
Sikukuu
Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Efe. 2:12-22
Msisahau kwamba zamani zile mlikuwa hamna Kristo, mmefarakana na jamii ya Israeli, wageni wasio na maagano ya ahadi ile. Mlikuwa hamna tumaini, hamna Mungu duniani. Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo. Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga. Naye akiisha kuuondoa ule uadui kwa mwili wake; ndio sheria ya amri zilizo katika maagizo; ili afanye hao wawili kuwa mtu mpya mmoja ndani ya nafsi yake; akafanya amani. Akawapatanisha wote wawili na Mungu katika mwili mmoja, kwa njia ya msalaba, akiisha kuufisha ule uadui kwa huo msalaba. Akaja akahubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali, na amani kwao wale waliokuwa karibu. Kwa maana kwa yeye sisi sote tumepata njia ya kumkaribia Baba katika Roho mmoja. Basi tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu. Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana. Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho.
Wimbo Wa Katikati: Zab. 85:9-14
- Nisikie atakavyosema Bwana,
Maana atawaambiwa watu wake amani.
Hakika wokovu wake u karibu na wamchao,
Utukufu ukae katika nchi yetu.
(K) Bwana anawaambia watu wake amani.
- Fadhili na kweli vimekutana,
Haki na amani zimebusiana.
Kweli imechipuka katika nchi,
Haki imechungulia kutoka mbinguni. (K) - Bwana atatoa kilicho chema,
Na nchi yetu itatoa mazao yake.
Haki itakwenda mbele zake,
Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia.
INJILI: Lk. 12:35-38
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka; nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara. Heri watumwa wale, ambao bwana wao ajapo atawakuta wanakesha.” Amin, nawaambieni, “Atajifunga na kuwakaribisha chakulani, atakuja na kuwahudumia. Na akija zamu ya pili, au akija zamu ya tatu, na kuwakuta hivi, heri watumwa hao.”
TAFAKARI
TUJIWEKE TAYARI KWA UJIO WA BWANA: Neno la Mungu linatualika kujiweka tayari kwa ajili ya ujio wa Bwana. Tujiwekeje tayari? Yesu anasema “Iweni kama watu wanaomngojea Bwana wao atakaporudi kutoka harusini wamfungulie mara”. Tuwe tayari kwa kurudi kwa Bwana Yesu kuwahukumu wazima na wafu. Hakuna ajuaye siku wala saa. Kwa hiyo Yesu anatuasa tena, viuno vyenu viwe vimefungwa na taa zenu ziwe zinawaka. Yatupasa kushughulika kujenga Ufalme wa Mungu kati ya watu. Kuwa karibu na waliokata tamaa maishani, kuwasikiliza wenye shida, kuwatembelea wagonjwa, wafungwa na kuwahudumia wenye shida mbalimbali. Tuwe watu wa kukesha kwa njia ya sala kusoma Neno la Mungu na kupokea sakramenti mbalimbali za kanisa. Hasa sakramenti za Upatanisho na Ekaristi Takatifu ili Bwana atakaporudi atukute tukiwa na neema ya utakaso. Tujiulize pia tumejiandaa au tunajiandaaje kwa siku ya ujio wa Bwana? Je, kama Bwana Mungu angeniambia leo ndio siku yangu ya kufa ningekuwa tayari na kufurahi kutwaliwa au kuna ya kurekebisha? Tutumie nafasi ya sasa kujiandaa vizuri.
SALA: Ee Mungu naomba unijalie kifo chema. Amina.