Kijani
Zaburi: Juma 2
SOMO 1: Gal. 5:18-25
Mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria. Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo; katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu. Lakini tunda na Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria. Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake. Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho.
Wimbo Wa Katikati: Zab. 1: 1-4, 6
- Heri mtu yule asiyekwenda
Katika shauri la wasio haki;
Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,
Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.
(K) Wanaokufuata, Ee Bwana,
Watakuwa na nuru ya uzima.
- Naye atakuwa kama mti uliopandwa
Kandokando ya vijito vya maji,
Uzaao matunda yake kwa majira yake,
Wala jani lake halinyauki;
Na kila alitendalo litafanikiwa. (K) - Sivyo walivyo wasio haki;
Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki,
Bali njia ya wasio haki itapotea. (K)
INJILI: Lk. 11:42-46
Yesu aliwaambia Mafarisayo: “Ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwatoa zaka za mnanaa na mchicha na kila mboga, na huku mwaacha mambo ya adili, na upendo wa Mungu; iliwapasa kuyafanya hayo ya kwanza, bila kuyaacha hayo ya pili. Ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwapenda kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni. Ole wenu, kwa kuwa mmefanana na makaburi yasiyoonekana, ambayo watu wapitao juu yake hawana habari nayo.”
Mtu mmoja katika wana-sheria akajibu, akamwambia, “Mwalimu, kwa kusema hayo umetushutumu sisi nasi.” Akasema, “Nanyi wanasheria, Ole wenu, kwa sababu mwawatwika watu mizigo isiyochukulika, wala ninyi wenyewe hamwigusi mizigo hiyo hata kwa kimoja cha vidole vyenu.”
TAFAKARI
TUFANYE YOTE KWA MOYO SAFI BILA UNAFIKI: Leo Yesu anawakaripia Mafarisayo na Wanasheria kwa vile walikuwa wanajisifia au kutaka kuonekana safi mbele za watu kumbe kwa ndani mioyo yao na mawazo yao ni tofauti kabisa. Ni kama mbwa mwitu aliyevaa ngozi ya kondoo. Yesu anawapa tahadhari kuwa wasipojirekebisha watapata hukumu na kukosa upendo, haki na uadilifu wa Mungu. Sisi wabatizwa tunaalikwa kutenda bila unafiki yale yanayotakiwa kutendwa. Tusijaribu hata mara moja kuonekana tofauti na namna tulivyo. Katika somo la kwanza, Paulo anawaasa Wagalatia waachane na matendo ya kidunia ambayo ni pamoja na uchafu, mwenendo mpotovu, ibada ya sanamu, uadui, mizozo, wivu na hasira. Anawataka watafute daima furaha, upendo, amani, uvumilivu, ukarimu, uaminifu na upole. Tuombe kuongozwa na Roho Mtakatifu tuweze kuachana na uoga unaoleta unafiki na hali ya vuguvugu katika kumtafuta Kristo kwa karibu.
SALA: Ee Mungu, tunaomba utukinge dhidi ya unafiki. Amina.