Kijani
Zaburi: Juma 2
SOMO 1: Gal. 4:22-24, 26-27, 31; 5:1
Imeandikwa ya kuwa, “Ibrahimu alikuwa na wana wawili, mmoja kwa mjakazi, na mmoja kwa mwungwana. Lakini yule wa mjakazi alizaliwa kwa mwili, yule wa mwungwana kwa ahadi.” Mambo haya husemwa kwa mfano; kwa maana hawa ndio kama maagano mawili, moja kutoka Sinai, lizaalo kwa utumwa, ambalo ni Hajiri. Bali Yerusalemu wa juu ni mwungwana, naye ndiye mama yetu sisi. Kwa maana imeandikwa, “Furahi, wewe uliye tasa, usiyezaa; paza sauti, ulie, wewe usiye na utungu; maana watoto wake aliyeachwa pekee ni wengi kuliko wa huyo aliye na mume.” Ndiposa, ndugu zangu, sisi si watoto wa mjakazi, bali tu watoto wa huyo aliye mwungwana. Katika ungwana huo Kristo alituandika huru; kwa hiyo simameni, wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa.
Wimbo Wa Katikati: Zab. 113: 1-7
- Aleluya. Enyi watumishi wa Bwana, sifuni,
Lisifuni jina la Bwana.
Jina la Bwana lihimidiwe
Tangu leo na hata milele.
(K) Jina la Bwana lihimidiwe milele.
- Toka maawio ya jua hata machweo yake
Jina la Bwana husifiwa.
Bwana ni mkuu juu ya mataifa yote,
Na utukufu wake ni juu ya mbingu. (K) - Ni nani aliye mfano wa Bwana,
Mungu wetu aketiye juu;
Anyenyekeaye kutazama,
Mbinguni na duniani?
Humwinua mnyonge kutoka mavumbini,
Na kumpandisha maskini kutoka jaani. (K)
INJILI: Lk. 11:29-32
Makutano walipokuwa wakimkusanyikia, Yesu alianza kusema, “Kizazi hiki ni kizazi kibaya; kinatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya Yona. Maana, kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa Waninawi, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu kwa kizazi hiki. Malkia wa Kusini ataondoka siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa na hatia; kwa sababu yeye alikuja kutoka nchi za dunia aisikie hekima ya Sulemani; na hapa pana mkubwa kuliko Sulemani. Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na kizazi hiki, nao watakihukumu kuwa na hatia; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona, na hapa pana mkubwa kuliko Yona.”
TAFAKARI
TUSIJIAMINI KWA SABABU YA UBATIZO WETU NA IMANI YA KIKRISTO: Katika Injili ya leo Yesu anatoa tahadhari kwa kizazi cha wakati wake. Tahadhari hii ni kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao. Watu wengi waliokuwa wanakusanyika kumsikiliza hawakuwa tayari kuamini aliyokuwa anatenda. Walitegemea zaidi kuona miujiza na ishara mbalimbali ndipo wamwamini. Yesu anawakumbusha wakati wa Yona aliyekaa katika tumbo la nyangumi kwa siku tatu na kutapikwa, akawa ishara kwa watu wa Ninawi kwa kutangaza hukumu ya Mungu na kuhimiza watu watubu. Nia ya Yesu ni kuwaalika wasikilizaji wake watubu na waongoke. Pamoja na ugumu huo Yesu anawahakikishia ukamilifu wa mahubiri yake ungetimilika katika ufufuko. Neno la Mungu linatualika kila wakati tugeuke na kumwongokea Mungu. Yawezekana wakati mwingine tumeshupaa au tunasitasita na kushindwa kufanya maamuzi sawa. Hili linatufanya tuwe na nia mbili. Tumwombe Mungu azibue masikio yetu kwa neno lake na atuondolee ugumu wa mioyo na kumfuata Kristo kikamilifu.
SALA: Bwana Yesu, naomba neema ya kuishi vema katika fumbo la Pasaka.