Oktoba 3, 2022; Jumatatu: Juma La 27 La Mwaka

Kijani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Gal. 1:6-12

Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine. Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo. Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe. Kama tulivyotangulia kusema, na sasa nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe. Maana, sasa je! Ni wanadamu ninaowashawishi, au Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa hata sasa nawapendeza wanadamu, singekuwa mtumwa wa Kristo. Kwa maana, ndugu zangu, injili hiyo niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu. Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 111:1-2, 7-10

 1. Aleluya.
  Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote,
  Barazani pa wanyofu wa moyo na katika mkutano.
  Matendo ya Bwana ni makuu,
  Ukawafunulia watoto wachanga.

K “Alikumbuka agano lake milele.”

 1. Matendo ya mikono yake ni kweli na hukumu,
  Maagizo yake yote ni amini.
  Yamethibitika milele na milele,
  Yamefanywa katika kweli na adili. (K)
 2. Amewapelekea watu wake ukombozi,
  Ameamuru agano lake liwe la milele.
  Jina lake ni takatifu la kuogopwa.
  Kumcha Bwana ndio mwanzo wa hekima,
  Wote wafanyao hayo wana akili njema,
  Sifa zake zakaa milele. (K)

INJILI: Lk. 10:25-37
Mwana-sheria mmoja alisimama akamjaribu Yesu, akisema, “Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” Akamwambia, “Imeandikwa nini katika torati? Wasomaje?” Akajibu akasema, “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako.” Akamwambia, “Umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi.”
Naye akitaka kujidai haki, alimwuliza Yesu, “Na jirani yangu ni nani?” Yesu akajibu akasema, “Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang’anyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa. Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipitia kando. Na Mlawi vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapitia kando.
Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza. Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, ‘Mtunze huyu, na cho chote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa.’
Waonaje wewe, katika hao watatu, ni yupi aliyekuwa jirani yake, yule aliyeangukia kati ya wanyang’anyi?’” Akasema, “Ni huyo aliyemwonea huruma.” Yesu akamwambia, “Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.”

TAFAKARI
HUDUMA YETU KWA WENYE MAHITAJI MBALIMBALI: Upendo wetu kwa Mungu unajidhihirisha na kukamilishwa katika kuwahudumia maskini. Katika Injili tumesikia mfano wa mtu aliyeangukia mikononi mwa wanyang’anyi na kuachwa bila msaada. Alipoachwa walipita watu watatu kwa nyakati tofauti, Kuhani, Mlawi na Msamaria. Mlawi na Kuhani hawakujali wala kujisumbua kumsaidia aliyepata shida. Msamaria ambaye kwa Wayahudi alionekana kutokuwa na heshima, ndiye aliyemsaidia. Yesu anamsifu. Kwetu sisi wakati mwingine tunakutana na watu katika hali mbalimbali mfano wameibiwa au kushambuliwa, wao ni maskini, yatima, wagonjwa, wanaodharauliwa au hata wale wanaonyimwa haki zao. Tujitahidi kuwa msaada kwao. Kama Msamaria, tumwone Mungu katika wahitaji na tuwasaidie bila kutazamia malipo. Kipaumbele chetu kiwe kuokoa maisha badala ya kung’ang’ania maneno ya sheria zisizojikita katika kuonyesha upendo kwa Mungu na jirani.

SALA: Ee Mungu, naomba unijalie kuishi fadhila za upendo kwa matendo.