Septemba 29,2022;Alhamisi: Juma La 26 La Mwaka

Wat. Mikaeli, Gabrieli Na Rafaeli, Malaika Wakuu
Sikukuu
Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku
SOMO 1: Dan. 7:9-10, 13-14

Nilitazama viti vya enzi vikawekwa, na mmoja aliye mzee wa siku ameketi; mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji, na nywele za kichwa chake kama sufu safi; kiti chake cha enzi kilikuwa miali ya moto, na gurudumu zake moto uwakao. Mto kama wa moto ukatoka ukapita mbele zake; maelfu-elfu wakamtumikia, na elfu kumi mara elfu kumi wakasimama mbele zake; hukumu ikawekwa, na vitabu vikafunuliwa. Nikaona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye. Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo haitapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 138:1-5

 1. Nitakushukuru kwa moyo wangu wote,
  Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.
  Nitakusujudu nikilikabili hekalu lako takatifu.

(K) Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.

 1. Kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako,
  Kwa maana umeikuza ahadi yako,
  Kuliko jina lako lote.
  Siku ile niliyokuita uliniitikia,
  Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu. (K)
 2. Ee Bwana, wafalme wote wa dunia watakushukuru,
  Watakapoyasikia maneno ya kinywa chako.
  Naam, watasiimba njia za Bwana,
  Kwa maana utukufu wa Bwana ni mkuu. (K)

INJILI: Yn. 1:47-51

Yesu alipomwona Nathanaeli anakuja kwake, akanena habari zake, “Tazama, Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake”. Nathanaeli akamwambia, “Umepataje kunitambua?” Yesu akajibu, akamwambia, “Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwapo chini ya mtini nilikuona.” Nathanaeli akamjibu, “Rabi, wewe u Mwana wa Mungu, ndiwe Mfalme wa Israeli.” Yesu akajibu, akamwambia, “Kwa sababu nilikuambia, ‘Nilikuona chini ya mtini’, waamini? Utaona mambo makubwa kuliko haya.” Akawaambia, “Amin, amin, nawaambia: Mtaziona mbingu zimefunguka na malaika wa Mungu wakikwea na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.”

TAFAKARI
KUKUTANA NA YESU KUNALETA MABADILIKO: Leo tunaadhimisha Sikukuu ya Malaika wakuu Gabriel, Michael na Rafaeli. Hawa waliumbwa na Mwenyezi Mungu na wakabaki kuwa wema. Hawakuasi kama malaika wabaya walivyoasi. Katika Injili tumesikia mazungumzo kati ya Yesu na Nathanaeli ambaye hapo mwanzo alikuwa na mashaka kama jambo jema linaloweza kutoka Nazareti. Yesu anapomwona Nathanaeli anakiri kuwa huyu ni Mwisraeli ambaye hana hila ndani yake. Neno la Mungu linatuambia, Yesu alimwona chini ya mtini, jambo ambalo ni ishara ya kuwa chini ya mpango wa Mungu. Mwisraeli asiye na hila ni yule ambaye yuko tayari kujiachanisha na mawazo yake binafsi pale anapogundua hayuko sahihi. Nathanaeli alitegemea Masiya ambaye angekuja kwa kadiri ya mafundisho ya wakati ule ndiyo maana alikataa kumpokea Yesu kama Masiha. Nathanaeli anapokutana na Yesu, anatambua alikuwa na mawazo potofu akabadili mawazo yake na kumpokea Yesu kama Masiha “Rabi, wewe u mwana wa Mungu, ndiwe mfalme wa Israeli”. Tujifunze utayari wa kubadili mawazo yetu na kukubali ya Kimungu. Yesu anabadili Maisha yetu kila tunapokutana naye.

SALA: Bwana Yesu naomba unijalie mabadiliko ya ndani. Amina.